Dos santos wa Angola kung'atuka 2018
11 Machi 2016Jose Eduardo dos Santos, mwenye umri wa miaka 73, ameyasema hayo katika hotuba yake mbele ya wanachama wa chama chake tawala MPLA katika hotuba iliyorushwa moja kwa moja katika radio bila ya kutoa ufafanuzi wowote kwa kuchukua hatua hiyo.
Kuporomoka kwa uchumi
Angola, taifa lililo katika shirikisho la mataifa yanayosafirisha kwa wingi mafuta, OPEC na la pili kwa kusafirisha mafuta kwa wingi barani Afrika baada ya Nigeria, limekabiliwa na hali mbaya ya kuporomoka kwa bei ya mafuta ghafi duniani. Usafirishaji wa bidhaa hiyo inaliingizia taifa hilo zaidi ya asilimia 90 ya fedha za kigeni.
Nchi hiyo ambayo zamani ilikuwa koloni la Ureno inatarajiwa kufanya uchaguzi wake wa bunge mwaka 2017 na kiongozi wa chama kitakachoshinda atakuwa rais ajae wa taifa hilo. Kiongozi wa MPLA Dos Santos alichaguliwa tena kuwa rais wa taifa hilo katika kipindi cha muhula wa miaka mitano katika uchaguzi uliofanyika Agosti 2012 baada ya chama chake kushinda kwa kishindo katika uchaguzi huo.
Mpaka sasa haijawa wazi kama Dos Santos ataendelea kuwa kiongozi wa MPLA katika uchaguzi ujao au atashiriki katika harakati za kampeni. Udhaifu wa kiuchumi umeikumba Angola kama taifa la tatu kwa nguvu za kiuchumi barani Afrika na serikali yake ipo katika majadiliano na benki ya dunia juu ya uwezekano wa kupatiwa msaada wa kifedha.
Hata hivyo wapinzani wamemkosoa Dos Santos kwa utawala mbovu na matumizi mabaya ya rasilimali ya mafuta ya taifa hilo na kufanya jamii ya wasomi, wengi wao kutoka katika familia yake na washirika wake kisiasa wananufaika na utajiri katika taifa hilo lilowekwa katika orodha ya mataifa yaliogubikwa zaidi na vitendo vya rushwa duniani.
Dos Santos ni kiongozi wa pili kwa kuwa madarakani kwa muda mrefu barani Afrika baada ya rais wa Guinea ya Ikweta, Teodoro Obiang Nguema Mbasogo, akifuatiwa na Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe.
Mwandishi: Sudi Mnette/RTR
Mhariri: Daniel Gakuba