1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waliokamatwa Tanzania wakati wa vurugu waachiwe huru

19 Novemba 2025

Mawakili wanaowatetea watuhumiwa wa kesi za uhaini waliokamatwa katika vurugu za uchaguzi wa Oktoba 29 wamemuomba Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kutekeleza agizo la Rais Samia Suluhu, kuwaachia mara moja watuhumiwa hao.

Tansania Daressalam 2025 | Maandamano ya kupinga uchaguzi
Polisi wakijaribu kudhibiti maandamano ya vijana wakati wa Ichaguzi wa Oktoba 29Picha: Onsase Ochando/REUTERS

Jopo la mawakili 10 wanaowatetea watuhumiwa hao wa kesi za uhaini, wamemuomba  Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) Sylivester Mwakitalu kutekeleza agizo la Rais Samiana kuwaachia watuhumiwa hao.

Mawakili hao wameyasema hayo baada ya kesi hizo kusikilizwa katika makundi matatu, na kuahirishwa. Kesi ya kundi la kwanza ni ile inayomkabili Paulina Palangyo na wenzake 25 ambayo imeahirishwa hadi  Novemba 25, kesi inayomkabili Jennifer Jovin maarufu Niffer na wenzake 21 iliyoahirishwa hadi Novemba 25  na nyingine ni kesi ya uhaini na kula njama za uhainiinayowakabili watuhumiwa 38 nayo imeahirishwa hadi Disemba 3.

Kuahirishwa kwa kesi hizi kumekuja wakati ambapo tayari Rais alitoa maagizo mnamo Novemba 11 wakati akilihutubia bunge na kutaka mahakama iwaachie kwa kuangalia uzito wa makosa yao. Akizungumzia kuendelea kushikiliwa kwa watuhumiwa hao Wiliam Maduhu wakili kutoka chama cha wanasheria Tanganyika (TLS), amesema.

“Sasa Na sisi leo tulikuwa na matumiani kwamba baadhi ya watuhumiwa wangeachiwa kulingana na utekelezaji wa gizo la Rais, lakini hapakuwa na utekelezaji, lakini tukaamini kwamba pengine utekelezaji huo unahitaji uchambuzi”

Washitakiwa hawakufikishwa mahakamani

Mashauri hayo yote yamesikilizwa kwa njia ya mtandao mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Beda Nyaki, ambapo washtakiwa hawakufikishwa mahakamani na upande wa Jamhuri ukijitetea kuwa wanaendelea na uchunguzi.

Mashauri yote yamesikilizwa kwa njia ya mtandao bila washtakiwa kufikishwa mahakamani Picha: Ericky Boniphase/DW

Upande wa utetezi, uliwakilishwa na mawakili 10 wakiongozwa na Sisty Massawe, Paul Kisabo, William Maduhu, na Peter Kibatala.

Kadhalika mawakili hao waliibua hoja ya kuongezeka kwa watuhumiwa wengine 35 katika kundi hilo la watuhumiwa ambao walifikishwa mahakamani Novemba 10 bila upande wa utetezi kujulishwa. Wakili Kibatala ameelezea mwenendo wa kesi hiyo.

“Ni mamlaka ya DPP kama ambavyo ana mamlaka ya kuwafikisha watuhumiwa mahakamani, kama ambavyo anaweza pia muda wote ule kesi inapokuwa na uhai, kabla ya hukumu kusoma anaweza kuiambia mahakama kuwa hana kusudi la kuendelea na kesi hiyo, kwa sababu yeye ndo ana mamlaka.”

Ama wakati hayo yakijiri, kadhalika Jeshi la polisi Mkoa wa Geita limethibitisha kumshikilia na kumhoji, Dk Kibaba Furaha mkazi wa Geita, akihusishwa na tuhuma za jinai. Taarifa hiyo ya polisi imekuja baada ya kuwepo kwa taarifa kwenye mitandao ya kijamii zikidai kuwa daktari huyo ametekwa na watu wasiojulikana.