Mwaka moja baadae, DRC bado yapambana na hali yake
24 Januari 2020Katika hatua iliyoleta ahueni kwa DRC na zaidi ya mipaka yake, makabadhiano ya madaraka kati ya Joseph Kabila na Felix Tshisekedi yalizima hofu kwamba taifa hilo kubwa zaidi katika eneo la Afrika Kusini mwa Sahara lingetumbukia tena katika machafuko ya kivita.
Lakini ahadi za Tshisekedi za kuharakisha mabadiliko, kwa kufanya mageuzi makubwa kupunguza umaskini na kukabliana na rushwa, pia yamefifia. Kabila anasalia kuwa mtu mwenyu nguvu sana nyuma ya pazia, akiwa na washirika katika jeshi na wafuasi wa kisiasa walio na wingi bungeni.
Kuunda muungano wa serikali kulichukuwa miezi tisa ya mazungumzo, na kupelekea kuundwa baraza kubwa la mawaziri lenye wajumbe 67, ambapo theluthi mbili kati yao ni washirika wa Kabila. Baraza hilo linaendelea kuwa chanzo cha mzozo.
Siku ya Jumapili, Tshisekedi alizungumzia hadharani uwezekano wa kuwafuta kazi mawaziri - onyo lililoulenga muungano wa Kabila wa Common Front for the Congo (FCC) -- au hata kulivunja bunge la taifa ili kutatua mkwano unaoendelea.
Wazo la mwisho lilipingwa kwa nguvu na moja wa wahsirika wake mwenyewe, Jeanine Mabunda, spika wa bunge, alieonya kuwa "mtu yeyote asiejua sheria yetu ya msingi anaweza kushtakiwa kwa uhaini wa juu kwa kukiuka katiba kwa maksudi."
Bunge la Taifa lililochaguliwa siku moja na uchaguzi wa rais Desemba 30 2018, lina mamlaka ya kusalia ofisini hadi 2023. Kulivunja kunaweza kuwa athari kubwa mithili ya "bomu la atomiki", alionya Richard Moncrief kutoka kundi la kushughulikia migogoro ICG.
Kuondoa ada za shule kwampa umaarufu miongoni mwa baadhi
"Tshisekedi ametoa vitisho, lakini mpangom wake wa kwanza ni kuendelea na muungano na Kabila." Miongoni mwa Wacongo, hatua za Tshisekedi kukomesha malipo ya ada katika shule za msingi kumepatia umaarufu kwa baadhi, lakini wengine wameeleeza kuvunjwa moyo na mazungumzo yasiyoisha kuhusu maisha bora.
Katika taifa hilo kubwa lenye utajiri wa madini ya kila aina, theluthi mbili ya watu milioni 80 wanaishi katika hali ya umaskini wa kutupwa. "Kwa rais huyo, kila mara unaskikia maneno, ujumbe, ahadi, hotuba kwa taifa, lakini ahadi zake hazijazaa matunda," alisema mkaazi wa Kinshasa, Jena-Yves, akitoa tu jina lake la kwanza.
Akikabiliwa na ukatishwaji tamaa na siasa za ndani, Tshisekedi ameelekeza nguvu zake zaidi katika kupunguza utengwaji wa Congo nje ya nchi, akifanya ziara nchini Marekani, Ufaransa na mkoloni wa zamani Ubelgiji.
Amefanikiwa kuboresha uhusiano na nchi jirani za Rwanda na Uganda akitumai kuleta amani katika upande wa mashariki uliogubikwa na machafuko, ambako makundi ya waasi yanayoanzia enzi za vita vya Congo katika miaka ya 1990 wanadhibiti maeneo makubwa.
Moncrieff amemsifu Tshisekedi kwa kukubali umuhimu wa mataifa ya kanda katika matatizo ya mashariki mwa DRC. Lakini ametahadharisha dhidi ya kuvialika vikosi vya kigeni nchini humo kusaidia kupambana dhidi ya wanamgambo.
"Amepuuza ukubwa wa uhasama wa watu wanaoishi mashariki kuelekea mataifa jiran," alisema. Mamia ya watu wameuawa katika mikoa ya mashariki ya Beni na waasi wa kundi la Allied Democratic Forces (ADF), kundi la kikatili la wanamgambo lenye asili yake nchini Uganda, na kuangazia zaidi ahadi ya Tshisekedi ya kuyasambaratisha makundi ya waasi nchini humo.
Chanzo: afpe