1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

DRC: Guterres akutana na Tshisekedi

Angela Mdungu
2 Septemba 2019

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, amesema baada ya kukutana na Rais Felix Tshisekedi, kwamba upepo mpya wa matumaini na hali bora unavuma nchini Kongo.

UN-Generalsekretär Guterres
Picha: picture-alliance/dpa/Bildfunk/Keystone/C. Zingaro

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, amesema baada ya kukutana na rais Felix Tshisekedi, kwamba upepo mpya wa matumaini na hali bora unavuma nchini Kongo. Usalama mashariki mwa Kongo, mapambano dhidi ya Ebola na marekebisho ya muhula wa Monusco ni baadhi ya maswala yaliojadiliwa na viongozi hao. Guterres ambae anakamilisha ziara yake leo nchini Kongo hii leo, atakutana na viongozi wa upinzani na wale wa mashirika ya kiraia.

Kufuatia ziara yake ya siku tatu nchini Kongo ambayo ilianzia huko Kivu ya kasakazini, katibu mkuu wa umoja wa mataifa Antonio Guterres ametowa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuunga mkono juhudi za Kongo katika kukuza demokrasia.

Aitaka Jumuiya ya kimataifa kuwaunga mkono viongozi wa Kongo

Guterres amesema kwa siku mbili alizotembelea Kivu ya kaskazini, ameshuhudia kwamba kuna upepo mpya wa matumaini na ya hali nzuri kwa ajili ya Kongo na kuitaka jumuiya ya kimataifa kuunga mkono viongozi wa nchi hiyo ili upepo huo uwe wa usalama na suluhisho la matatizo ya kiutu.

Guterres alikuwa na mazungumzo ya takriban saa moja na rais Felix Tshisekedi, kwenye ikulu ya Palais de la Nation. Mazungumzo yao yalihusu hasa usalama, ugonjwa wa Ebola na muhula wa kikosi cha MONUSCO.

Katibu mkuu wa umoja wa mataifa ambaye ametembelea kwa mara ya kwanza Kongo toka ashike wadhifa huo ameomba makundi yote ya wapiganaji huko Kivu kuweka chini silaha. Antonio Guterres ameahidi mageuzi katika kikosi cha MONUSCO na muhula wake huku akisema kwamba baraza la usalama ndilo linatarajiwa kupitisha azimio jipya kuhusu kikosi hicho.

Guterres amesema Umoja wa Mataifa hautawasahau raia wa Kongo. Katibu mkuu huyo wa umoja wa Mataifa amekutana pia na spika wa bunge Bi Jeannine Mabunda na viongozi wa upinzani, na kuwahimiza raia wa Kongo kukuza misingi ya demokrasia na haki za binadamu.

Mwandishi: Saleh Mwanamilongo, DW Kinshasa.

 

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi