DRC kabla ya uchaguzi yatakiwa kuwa na utulivu
19 Desemba 2018Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo itafanya uchaguzi wake uliocheleweshwa kwa muda mrefu ambao utashuhudia ubadilishanaji wa madaraka kwa njia ya amani kwa mara ya kwanza tangu nchi hiyo kupata uhuru kutoka Ubelgiji.
Kiasi watu sita wameuwawa katika ghasia zilizojitokeza katika utawala wa miaka 17 wa Rais Joseph Kabila. Serikali ya nchi hiyo inakana kuhusishwa kwa njia yoyote na mauaji hayo pamoja na kampeni. Baraza la Usalama limezitaka pande zote kuendelea kupinga ghasia za aina yoyote, na kujizuwia kwa kiwango cha juu kabisa katika hatua wanazozichukua na kujitenga na kuchochea ghasia na hotuba za uchochezi na kutakiwa kutoa maelezo ya tofauti zao kwa njia za amani, imesema taarifa ya baraza hilo.
Wajumbe wa baraza la Usalama pia wamesisitiza umuhimu wa kuhakikisha usalama na ulinzi kwa wagombea na wapiga kura wakati wa kipindi cha kampeni.
Wakati huo huo, wamerejea wito wao kwa vyama vyote kufanyakazi kwa amani na kwa njia nzuri katika mchakato wa uchaguzi, kuhakikisha uwazi, matokeo ya amani na yenye kuaminika.
Hatua zimepigwa katika kuelekea uchaguzi
"Wakati wanakaribisha hatua zilizopigwa katika matayarisho ya kiufundi kwa ajili ya uchaguzi huo, wajumbe wa baraza la Usalama la Umoja wa mataifa wana wasi wasi juu ya kile walichokieleza kuwa ni matukio ya ghasia yanayochafua siku za mwisho za kampeni za uchaguzi, taarifa yao ilisema. Kwa hiyo baraza hilo linatoa wito kwa serikali ya DRC kufanya uchunguzi wa haraka kuhusiana na matukio hayo, taarifa hiyo imesema.
Katika kuelekea katika uchaguzi huo siku ya Jumapili tarehe 23, kuanzia mataifa yenye mpaka pamoja na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, baadhi yake yakiwa yamechochea mizozo ya nchi hiyo, mataifa makubwa ya kimataifa kujaribu kufanya juhudi za kuleta amani , athari za uchaguzi ujao, mitikisiko katika nchi hiyo inaonekana kufika mbali zaidi.
Mataifa jirani ya taifa hilo yamepigana vita katika ardhi ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, lakini bado taifa hilo linalinda maslahi yake katika taifa hilo lenye matatizo.
Utawala wa sasa katika DRC ni matokeo ya moja kwa moja ya uingiliaji kati wa mataifa jirani katika mizozo miwili kati ya mwaka 1996 na 2003 ambayo imesababisha kuingizwa nchini humo majeshi kutoka karibu mataifa saba ya Afrika na kusababisha mamilioni ya watu kuuwawa.
Moto wa eneo hilo uliwashwa na mauaji ya kimbari nchini Rwanda mwaka 1994, wakati kiasi ya wakimbizi wengi wao wakiwa ni wahutu karibu milioni mbili pamoja na wale ambao waliongoza mauaji hayo , walipokimbilia ndani ya Congo. Waasi walitumia kambi zao kama vituo vipya vya kufanya mashambulio yao dhidi ya Rwanda , na kusababisha Rwanda kuivamia Congo.
Rwanda kwa msaada wa Uganda , iliunga mkono uasi ambao ulisababisha kuangushwa kwa Rais Mobutu Sese Seko na kushuhudia Laurent Desire kabila kuwa rais mwaka 1997. Haikuchukua hata mwaka mzozo mwingine ukaibuka.
Mwandishi: Sekione Kitojo/afpe
Mhariri: Mohammed Khelef