1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

DRC kuendeleza juhudi za kuyalinda mazingira

1 Desemba 2021

Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo imesema haiwezi kuzungumzia juu ya kuvunjika moyo kuhusiana na suala la mazingira baada ya kumalizika mkutano wa hivi karibuni huko Glasgow,Scotland

DR Kongo Umweltministerin Eve Bazaiba
Picha: Dirke Köpp/DW

Waziri wa mazingira wa nchi hiyo Eve Bazaiba alizungumza na DW katika mahojiano maalum na kutoa msimamo wa nchi yake kuhusu suala hilo.

Waziri wa mazingira wa nchi hiyo Eve Bazaiba amesema anafikiri kitu muhimu kwa nchi yake sio suala la  kuvunjika moyo bali wanaamini katika kila mchakato kuna mafanikio na mapungufu ambayo yanapaswa kushughulikiwa.Na kuhusiana na nchi yake kuna mafanikio mengi ambayo yako wazi kabisa.Amesema haiwezi kupingwa kwamba Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo ni nchi ambayo ina mchango  katika kutafutia suluhisho mgogoro wa  mazingira. 

Amesema walichofanikiwa Glosgow ni kuzipaaza sauti zao na zikasikika. Aidha amaweka wazi kwamba wao kama nchi za eneo la bonde la mto Kongo sio wazalishaji wa gesi inayochafua mazingira na wala sio miongoni mwa nchi zinazoharibu mazingira na kwa hivyo kanuni ya kuwataka wachafuzi wa mazingira wabebe dhamana inapaswa kutumika katika suala hili. Waziri  Eve Bazaiba ameongeza kusema.

''Kila mmoja anafahamu kwa upande mmoja kwamba kuna nchi zilizohusika kuchafua mazingira na kwa upande mwingine misitu yetu inachangia kunyonya hewa inayochafua mazingira''

Pamoja na hilo amesema wanahitaji fedha zitakazowasaidia kwenye harakati hizo za kulinda mazingira ili kufanikisha hatua ya  kupunguza kiwango cha joto duniani.

Hifadhi ya wanyama ya Virunga nchini CongoPicha: WWF/Brent Stirton

Ama kuhusiana na suala la kuilinda misitu mwito wake mkubwa alioutowa ni kwamba kama nchi wameshadhamiria kutowa mchango chini ya makubaliano ya Paris na kwamba kipaumbele chao kikubwa kama taifa katika kupunguza uzalishaji wa gesi chafu kitalenga hasa sekta ya nishati,kilimo,na uchimbaji madini kwasababu sekta zote hizi zina mchango wake katika athari za mazingira.

Ingawa pia ameweka wazi kwamba pale wanapoomba fedha kutoka nchi zilizoendelea kiviwanda,fedha hizo hazihusu msaada wa maendeleo bali nchi hizo zinapaswa kuutazama mchango wao katika mapambano dhidi ya ongezeko la joto duniani.Na sababu kubwa ni kwamba athari hiyo inatokana na uchafuzi wa mazingira unaosababishwa maendeleo ya kiviwanda.

Japokuwa pia amesisitiza kwamba hawawezi kuzilaumu nchi tajiri kiviwanda kwasababu hata nchi zao zimefaidika kutokana na maendeleo ya nchi za kiviwanda. Kwa mtazamo wa waziri huyo wa mazingira wa Kongo mkakati bora wa kulinda msitu wa nchi yake ni kufanikisha familia nyingi na biashara kuwa na uwezo wa kupata umeme kwasababu ukweli ni kwamba familia nyingi hazitumii tu misitu kwa ajili ya kuni za kupikia na matumizi mingine ya nyumbani.

Lakini ikiwa watahitaji kutumia rasilimali zao wenyewe kwa mfano kutengeneza magari yanayotumia umeme bila shaka nishati itahitajika.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW