DRC kufanya mazungumzo na nchi jirani kukabili Ebola
18 Julai 2019Akizungumza mbele ya vyombo vya habari mjini Goma, waziri anayehusika na wizara ya Afya katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Dkt. Oly Ilinga, amesema nchi yake itafanya mazungumzo ya pamoja na nchi jirani kuhusu mbinu na mikakati ya kupambana na mlipuko wa ebola katika eneo hilo. Kufikia sasa mlipuko wa Ebola umewaua takriban watu 1,700 katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Hata hivyo Dkt. Ilinga amelaani kile alichokiita kuwa usambazaji wa taarifa zisizosahihi kupitia mitandao ya kijamii, kuhusu mlipuko wa ugonjwa huo.
Katika mkutano na vyombo vya habari mjini Goma Dkt. Ilunga ameelezea kuridhishwa na hatua ya shirika la afya duniani WHO, kuutangaza mripuko wa sasa wa Ebola kuwa dharura ya kimataifa, baada ya mkutano uliofanyika mjini nchini Uswisi.
Waziri huyo wa afya amelaani tabia iliyoshika kasi miongoni mwa wananchi, ya kutumia mitandao ya kijamii kusambaza habari za uongo kuhusu mlipuko huo bila kuzingatia onyo toka uongozi wa kikosi kinachopambana na Ebola.
Wakaazi wa mji wa Goma wamejawa na wasiwasi tangu homa hiyo ilipotangazwa kuingia katika mji huo wenye wakaazi zaidi ya milioni moja.
Wakati huo huo, shirika la WHO limesema mvuvi wa Kikongo aliefariki kutokana na homa ya Ebola, huenda alibeba virusi hivyo kutoka Congo hadi ndani ya Rwanda na pia Uganda, mnamo wakati maafisa wa afya wakipambana kuwafuatilia watu ambao anaweza kuwa aliwaambukiza.
Watu watatu walifariki nchini Uganda mwezi uliopita, lakini hawakusamba Ebola zaidi nchini humo, na Rwanda haijawahi kurekodi kisa chochote cha Ebola.
Wizara ya afya ya Congo inashuku kuwa wakati akiwa ameambukizwa, mwanamke huyo pia alikuja mjini Goma na mji wa Gisenyi nchini Rwanda.