1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

DRC kujadili utekelezaji wa makubaliano

Sylvia Mwehozi
3 Januari 2017

Wapatanishi wanaojaribu kutatua mgogoro ulioiathiri Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wamesema pande zinazozozana katika mgogoro huo watakutana wiki hii kwa mazungumzo yao ya kwanza juu ya utekelezaji wa makubaliano.

DR Kongo Präsident Kabila einigt sich mit Opposition
Picha: Getty Images/AFP/J. D. Kannah

Mmoja wa wapatanishi Padre Donatien Nshole ambaye ni msemaji wa baraza la kitaifa la maaskofu katoliki nchini Congo CENCO ameliambia shirika la habari AFP kuwa "mkutano wa awali wa kuamua juu ya makubaliano hayo umepangwa kufanyika leo Jumanne".

Makubaliano hayo ya vuta nikuvute yaliyofikiwa mkesha wa mwaka mpya yanalenga kuzuia mgogoro juu ya mustakabali wa Rais Joseph Kabila.

Kwa mujibu wa katiba ya Congo, kiongozi huyo ilikuwa aondoke madarakani Desemba 20 mwaka jana baada ya kumalizika kwa muhula wake wa pili lakini hakuonyesha dalili ya kufanya hivyo. Chini ya makubaliano yaliyofikiwa rais Kabila atasalia madarakani hadi pale uchaguzi mkuu utakapofanyika "mwishoni mwa 2017".

Felix Tshisekedi kutoka chama cha upinzani UDPS akisaini makubaliano mapyaPicha: Reuters/K. Katombe

Katika kipindi cha miezi 12 baraza la mpito la taifa litaanzishwa na litaongozwa na kiongozi wa upinzani Etienne Tshisekedi.

Yaliyokubaliwa

Baadhi ya yaliyokubaliwa yameelezewa na rais wa baraza la kitaifa la maaskofu nchini Congo CENCO Askofu Marcel Utembi kuwa ni pamoja na " kwanza, mamlaka na muhula wa pili na wa mwisho wa rais wa Jamhuri ambayo yalimalizika Desemba 2016 hayatarudiwa upya. Mkuu wa nchi hatokuwa na muhula wa tatu. Suala la pili hata hivyo rais ataendelea kufanya majukumu yake hadi atakapochaguliwa rais mpya. Tatu; rais, bunge na uchaguzi wa kitaifa utafanyika kabla ya Desemba 2017. La nne, hakutakuwa na jaribio la kurekebisha katiba wakati wa kipindi cha kabla ya uchaguzi wala wakati wa kipindi cha uchaguzi"

Wachambuzi wa siasa za Congo wanasema pande zote zimeelewa umuhimu wa kutia saini makubaliano hayo na yeyote atakayekuwa wa kwanza kukiuka atabebeshwa lawama za kuanzisha machafuko.

Christopher Lutundula, ambaye alitia saini makubaliano hayo kwa upande wa upinzani, amesema mazungumzo yaliopangwa yatahusu "mipango maalumu" juu ya uanzishwaji wa baraza la mpito ambalo limepewa jina la Baraza la Taifa la Kusimamia Mkataba na Mchakato wa Uchaguzi CNSAP.

Upande wa Serikali

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Joseph Kabila Picha: picture alliance/AP Images/J. Bompengo

Kwa upande wa serikali, waziri wa mawasiliano Lambert Mende amesema mazungumzo hayo yanapaswa kutafutia ufumbuzi tatizo la "ushirikishwaji" akimaanisha wajumbe 10 wanaounga mkono serikali ambao hawakutia saini makubaliano hayo.

Mende amesema serikali imeridhishwa na makubaliano hayo lakini sehemu ya upinzani ambao walisaini makubaliano ya Oktoba 18 hawakuwepo na kwamba kulikuwa na ukosoaji wa makubaliano ya awali kwa sababu kadhaa ambazo zimejitokeza tena katika makubaliano ya sasa, lakini akasisitiza kuwa "ninayo matumaini kwamba sababu hizohizo hazitaleta athari ileile na nimeridhika kwa ajili ya nchi yangu."

Wakati mpango huo wa maelewano ukifanikiwa hadi sasa kuzuia kutokea kwa vurugu, maswali mengi yanayosalia vichwani mwa watu ni kwamba ni kwa namna gani? na ikiwa yatatekelezwa. Jumuiya za kimataifa zimepongeza hatua hiyo na kuzitaka pande zote kuheshimu makubaliano.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/AFP

Mhariri: Iddi Ssessanga

 

 

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi
Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW