1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

DRC: Mahakama kuanza kusikiliza kesi kuhusu uchaguzi mkuu

Jean Noël Ba-Mweze
8 Januari 2024

Mahakama ya katiba nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo itaanza leo kusikiliza kesi kuhusu uchaguzi mkuu uliomrudisha tena madarakani rais Felix Tshisekedi.

Rais Felix Tshisekedi (katikati) akizungumza na wafuasi wake baada ya tume ya uchaguzi kumtangaza mshindi
Rais Felix Tshisekedi (katikati) akizungumza na wafuasi wake baada ya tume ya uchaguzi kumtangaza mshindiPicha: Arsene Mpiana/AFP/Getty Images

Kesi hiyo inaanza huku viongozi wa upinzani wakiendelea kusisitiza matakwa yao ya kufutwa kwa ujumla uchaguzi huo uliofanyika Disemba 20, wakitowa hoja kwamba,ulifanyika udanganyifu.

Hayo yamejiri baada ya tume huru ya uchaguzi CENI, kufuta matokeo ya wagombea 82 katika uchaguzi wa ubunge wa kitaifa na ule wa mikoa kwa tuhuma za udanganyifu, ufisadi na umiliki haramu wa vifaa vya kupigia kura.

Ni Wakongo wawili ndiwo waliwahi kufikisha malalamiko yao mbele ya mahakama ya katiba ambao ni Théodore Ngoy ambaye ni miongoni mwa waliogombea kiti cha urais pamoja na mwananchi mwengine moja wa kawaida.

Soma pia: Umoja wa Mataifa waonya kukithiri kwa matamshi ya chuki DRC 

Baadhi ya wagombea wengine wa urais wakiwemo Moïse Katumbi, Martin Fayulu na Denis Mukwege nao wametaka matokeo ya uchaguzi yabatilishwe japokuwa  walikataa kufikisha malalamiko yao mbele ya mahakama ambayo wanaamini ni ya kikabila na inatumiwa na jamii ya raïs Félix Tshisekedi.

Wagombea wanane wanaamini kuwa kasoro zote zilifanyika katika ushirikiano na utawala wa Tshisekedi, kama alivyoeleza Martin Fayulu, mmoja wa wagombea hao, "Tumetambua kwamba walionufaika na vifaa vya kupigia kura wote ni kutoka familia moja ya kisiasa, yaani ile ya Tshisekedi. Sasa CENI itaonyesha vipi kuwa katika uchaguzi wa pamoja, ni  uchaguzi wa wabunge tu ndiwo uliibiwa ila sio ule wa rais."

Wagombea 82 wafutiwa matokeo

Mmoja wa wapinzani Prince Epenge wakati wa maandamano ya kushinikiza kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi wa Disemba 20 mjini KinshasaPicha: Paul Lorgerie/DW

Miongoni mwa wagombea waliofutiwa matokeo yao ya uchaguzi ni pamoja na  mawaziri wanne, magavana wa mikoa mitano  wakiwemo Gentiny Ngobila wa hapa kinshasa. Pia maseneta sita pamoja na wabunge watatu. Tume  ya kupambana na ufisadi hapa nchini, Licoco, imewataka wote kufikishwa mbele ya mahakama.

Ernest Mpararo ambaye ni mratibu wa licoco ameeleza, "Tunaomba Ofisi ya Mwendesha Mashtaka Mkuu wa korti kuu kuwafungulia mashtaka ili wapewe adhabu kufuatana na sheria. Tutawasiliana na ofisi ya mwendesha mashtaka Jumatatu hii ili wagombea hao wote kuadhibiwa ipasavyo."

Soma pia:  Maaskofu waomba mwanga kuhusu kasoro za uchaguzi Kongo

Tangu kuanzishwa mchakato wa uchaguzi nchini Kongo, muungano wa  wataalam wa mashirika ya kiraia ulikuwa umeonya mara kwa mara kuhusu hatari ya udanganyifu. Wataalam hao sasa wametowa mwito matokeo ya chaguzi zote kufutwa na kuanza upya mchakato huo. Dieudonné Mushagalusa ni mratibu wa muungano huo.

"Tunaendelea kusema chaguzi zote hizi zifutwe ili kuziandaa upya katika utaratibu. Hivi CENI tayari imekiri kila kitu tulichokuwa tumekionya. Tunatarajia sasa mahakama ya katiba kuahirisha uthibitisho wa matokeo ya mwisho ya mgombea yeyote."

Takriban vyama 30 vimeathirika na kadhia hiyo. Wahusika walio wengi ni kutoka Union Sacrée, muungano wake rais Tshisekedi.

Upande mwengine, CENI iliamua pia kufuta matokeo ya uchaguzi wa bunge wa kitaifa na wa mikoa katika maeneo ya Masimanimba mkoani Kwilu na Yakoma katika mkoa wa Ubangi kaskazini.