1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

DRC: Mauaji yaendelea licha ya uwepo wa vikosi vya usalama

22 Machi 2023

Licha ya mataifa ya mashariki na kusini mwa Afrika kutuma wanajeshi wake mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, bado mauaji dhidi ya raia yanaendelea na wimbi jipya la wakimbizi linashuhudiwa.

DR Kongo Flüchtlinge aus Flüchtlingslager Kanyaruchikya
Picha: Benjamin Kassembe/DW

Kuufahamu ukubwa wa mzozo wa Kongo, tupia jicho lako nchi jirani ya Tanzania, ambako tangu mwanzoni mwa mwezi huu wa Machi pekee, kila siku wakimbizi baina ya 300 na 600 wanavuuka mpaka kutoka Kongo na kusajiliwa na Ofisi ya Wakimbizi katika Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi hiyo.

Watu hawa wanapelekwa kwenye kambi ya wakimbizi ya Nyarugusu, anasema Sudi Mwakibasi, afisa mwenye dhamana, "Hiki kinachofanyika hapa ni utekelezaji wa jukumu letu la msingi katika hifadhi ya wakimbizi duniani."

Watu wanaopokelewa hapa wanakimbia ukatili unaofanywa na makundi mbalimbali yenye silaha katika mkoa wa Kivu Kaskazini, kama vile M23.

Ujumbe maalum wa EAC ukiongozwa na rais mstaafu wa Kenya Uhuru Kenyatta wawasili mjini GomaPicha: Benjamin Kasembe/DW

Anasema Selemani Malembe, ambaye amefanikiwa kufika mjini Kigoma baada ya kutumia mtumbwi kuvuuka Ziwa Tanganyika, akiwa peke yake bila mkewe wala wanawe, "Tunakimbia vita yenye inatusumbua sana, yaani tushasumbuka sana. Tunaomba serikali itusaidie sana. Yaani mafamilia wengi wanauawa. Kama mimi hivi sijui kama mke wangu iko wapi na watoto. Yaani hivi ni mateso kwa kweli."

Makundi ya waasi DRC yafanya mauaji Ituri na Kivu Kaskazini

Kundi la waasi la M23 lililoanzishwa mwaka 2012 kwa jina la Vuguvuguh la Machi 23, limefanikiwa hadi sasa kuendesha kampeni kubwa ya kijeshi katika mkoa huo wa Kivu Kaskazini, ambako limetwaa vijiji na miji kadhaa.

Lakini M23 hawako peke yao mashariki mwa Kongo. Kundi la waasi la ADF linalojinasibisha na kundi la kigaidi lijiitalo Dola la Kiislamu limefanya mauaji kadhaa ya maangamizi ama likitumia bunduki au mapanga.

Picha: Benjamin Kasembe/DW

Hayo ni hata baada ya kuanzishwa kwa kile kiitwacho "Operesheni Shujaa" baina ya jeshi la Uganda na Kongo mwaka 2021. Kikubwa kinachoweza kunasibishwa na mafanikio ya operesheni hiyo ni kuuawa kwa kiongozi wa kundi hilo mwishoni mwa mwezi Februari.

Adolphe Agenonga Chober wa Chuo Kikuu cha Kisangani anasema katika eneo ambalo kila mmoja anabeba silaha, ni shida amani kuletwa na vikosi hivi vya pamoja, "Tangu mwanzoni mwa Operesheni Shujaa, kazi imekuwa ikiachwa kwa kikosi hiki cha pamoja tu, ingawa hakidhibiti eneo lote ambako ADF wanaendesha mashambulizi yao."

"Pia ifahamike kumekuwa na mkanganyiko tangu makundi ya kujihami ya raia yatambuliwe kuwa ni wasaidizi wa jeshi. Wakati mwengine ni shida kujuwa ikiwa wapiganaji wenye silaha ni ADF au kundi la kujihami la Maimai."

EAC yaunda kikosi cha pamoja kukabiliana na waasi

Hali hii ya kuchanganyikiwa inaongezeka hadi kwenye mji mkuu, Kinshasa - kwa mara nyengine. Awali majaribio yalifanyika kuunda kikosi cha pamoja cha Jumuiya ya Afrika Mashariki ili kukabiliana na ukosefu wa salama na kitisho cha mashambulizi, hasa kutoka kundi la M23.

Akina mama na watoto ndio wahanga wakubwa wa vita nchini DRCPicha: GUERCHOM NDEBO AFP via Getty Images

Lakini hilo nalo halijafanya kazi. Maeneo ya kutenganisha wanajeshi na wasi yaliyowekwa na vikosi vya EAC ili kusimamia usitishaji mapigano hayakubaliki na Kinshasa inayosema kuwa yanaviweka kando vikosi vyake huku vya M23 vikipata nguvu ya kusonga mbele.

Badala yake, jicho sasa liko kwa jirani wa kusini, Angola. Siku ya Ijumaa, bunge lilipitisha kwa kauli moja uamuzi wa kutuma wanajeshi 500 huko. Kwa hakika, Rais Joao Lourenco wa Angola amesimama kama mpatanishi wa mzozo huo na kuwezesha makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyotakiwa kuanza tarehe 7 Machi.

Hadi sasa, hakuna uhakika ikiwa kweli makubaliano hayo yangalipo ama yameshazikwa.