1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

DRC: Raia wataka ghasia kusitishwa Kivu Kaskazini na Ituri

24 Januari 2022

Ili kupinga hali ya dharura mkoani Kivu Kaskazini na Ituri muungano wa makundi ya mavuguvugu ya vijana ukiwemo Lucha, umewasihi wakaazi wa Beni kubaki nyumbani kwani hamna mabadiliko tangu kutangazwa kwa hali ya dharura

DR Kongo | Nord Ost Ituri | Menschenrechtsverletzungen
Picha: Tom Peyre-Costa/NRC

Tangu alfajiri leo jumatatu,askari polisi wamekuwa wakifyetua risasi angani, kuwatawanya waandamanaji, katika kata za Kanzuli pamoja na Ngongolio. Akiwaomba wakaazi wa Beni kuendelea na shughuli zao za kawaida mjini Beni,baada ya kuwapeleka askari wake kwenye maeneo kadhaa ya Beni, kamanda wa Polisi mjini, kamisa Sébastien Kauma, aliwaonya pia waandamanaji kwa matamshi haya

"Yeyote atakayeondoka nyumbani kwake kwenda barabarani kuchafua usalama,anatakiwa kutizama picha ya mke wake, ya ndugu zake,dada zake na watoto wake. Na anapotoka nyumbani akiwa anadhani kwamba yuko juu ya sheria, ole wake kwani hatowaona tena ndugu na dada zake kwani nafasi yake imetayarishwa mahali fulani na hawatokuwa tena katika jamaa zao," alisema Sébastien Kauma.

Muungano wa mavuguvugu ya vijana katika mji wa Beni, waliitisha mgomo wa siku tano, kama awamu ya kwanza ya mfululizo wa maandamano yatakayofanywa.

soma zaidi: Mapigano yazuka upya Ituri wakati rais Tshisekedi akiwa Goma

Akizungumza na DW, mmoja wa vijana wa Vuguvugu kwa ajili ya mabadiliko Lucha mjini Beni,Fabrice Mulwahali amesema, kuwa muda umewadia wa kuwarudisha madarakani viongozi raia, ambao nafasi yao imeshachukuliwa na maofisa wa polisi pamoja na jeshi kwani, viongozi wa polisi na jeshi kwenye wilaya,miji na mikoa,hawawaheshimu raia hata kidogo.

Mgomo wa siku tano mfululizo, haujaridhiwa hata hivyo na mashirika ya kiraia katika mji wa Beni.

Mwanasheria Pepin Kavota, mwenyekiti wa mashirika hayo amesema, kuwa ni muhimu kwa vijana pamoja na viongozi wa serikali kukaa kwenye meza ya mazungumzo na kutatua tofauti zao.

Tangu alfajiri, ni watu thelathini waliokamatwa na polisi, kufuatia maandamano ya leo na pikipiki mbili kuchomwa moto na waandamanaji.

Hadi tunatuma ripoti hii,milio ya risasi imekuwa ikisikika na shughuli nyingi zimefungwa,mukiwemo shule katika mkoa mdogo wa Mulekera.

Mwandishi: John Kanyunyu DW Beni

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW