1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Athari ya vita katika mfumo wa elimu mjini Goma DRC

8 Machi 2024

Wakimbizi wa Vita vya M23 wanaharibu mfumo wa elimu katika mji wa Goma. Baadhi ya shule haziwezi kuendesha shughuli za masomo kwa sababu wakimbizi hao kutoka MASISI wanahifadhiwa kwenye madarasa ya shule hizo.

DR Congo | Maandamano ya wanafunzi mjini Goma
Wanafunzi wanaoandamana mjini Goma huku mzozo unaoendelea kati ya vikosi vya DR Kongo na waasi wa M23 ukiuzuia shughuli za masomo katika eneo hilo,13.02.2023 Picha: Benjamin Kasembe/DW

Wamiliki wa shule ya Msingi ya Lac Vert iliyo magharibi mwa mji wa Goma, wamewapa wakimbizi hao muda wa mwisho hadi jumatatu ijayo kuondoka ili kuruhusu watoto kuanza masomo.

Wakimbizi hao walioingia katika mji wa Goma, wengi wao wamejazana kwenye madarasa ya shule za eneo la Mugunga. Hali hiyo imeathiri shughuli za shule katika sehemu hio ya mji wa Goma kwa wiki kadhaa sasa. Mmiliki wa Shule ya Msingi ya Lac Vert Hangi Bahati, amezungumzia hali hiyo, akibainisha kuwa tangu wakati huo, watoto wamekuwa mitaani. "Kupitia vita watoto kwa leo hawako tena ndani ya masomo. Masomo imebaki ni ma camps ya ma jeshi. Na watoto kwa leo wana zunguka mitaani sababu ya vita, hawana walimu."

Amri ya wakimbizi kuondoka katika eneo wanalojihifadhi

Watu waliokimbia makazi yao wanaonekana katika kambi ya wakimbizi nje kidogo ya Goma, jimbo la Kivu Kaskazini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Februari 8, 2024.Picha: Zanem Nety Zaidi/Xinhua/IMAGO

Wakimbizi hao wamepewa siku chache waondoke shuleni hapo ili kuruhusu watoto kurejea shuleni kuanzia Jumatatu, Machi 11, 2024. Wazazi wa wanafunzi bado wana wasiwasi juu ya hali hio, ambayo inawalazimisha watoto kubaki mitaani badala ya kwenda shule kusoma ili kuhakikisha mustakabali wao mzuri. Bora Batende, ni mzazi wa mwanafunzi mmoja na ambae anasema kabla ya vita walikuwa wanasoma na kutokana na hali hiyo watotohawana nafasi tena ya kusoma jambo ambalo sio zuri kwa sasa.

Watu waliokimbia vita ambao wapo katika shule hio wangependa kuondoka mahali hapa. Lakini wanasema, hawana pa kwenda, wala hawana vifaa vya kujenga mahema ya muda katika kambi walizopelekwa. Mkimbizi Bibiche Ndoole anasema "Tulikimbia vita ya M23, tuliona mashambulizi yanakuwa mengi, ndugu zetu wengi wameuwawa, ndio sababu tukakimbia na kuja kujihifadhi hapa shuleni. Kwa sasa tunashindwa kujua mahala pa kwenda, tunafahamu wanafunzi wa hapa Mugunga hawawezi kusoma kwa sababu yetu."

Athari za vita kwa elimu ya msingi katika eneo la Kivu ya Kaskazini

Mamlaka ya elimu ya msingi katika mkoa wa Kivu Kaskazini inasema kuwa hali hio inaathiri elimu nchini. Luc Baweza Kabango, Afisa Mkuu wa Elimu Kaskazini mwa Kivu, anaamini kuwa vita vinawaathiri vibaya watoto na pia inaathiri elimu yao ya msingi. "Tangu vita vilipoanza zaidi ya miaka miwili iliyopita, utaona kwamba mambo hayabadiliki; yaani, shule nyingi zimefungwa na kuna watoto ambao hawasomi. Itabidi tufanye kazi kubwa kwa sababu akili za watoto zinaathiriwa na migogoro ya silaha, kuna watoto wengine ambao pia watakuwa kama wanyama au waasi. Hii inaharibu vipengele vyote vya elimu.

Soma zaidi: Waasi wa M23 wauzingira mji wa Sake, DRC

Mji wa Goma unakumbwa na mgogoro wa elimu huku athari za vita vya M23 zikionekana. Wapiganaji wa M23 wanaendelea na mashambulizi kwenye maeneo kadhaa. Ijumaa, ya tarehe nane Machi, vijiji vya Katanda na Mayi ya Moto vilivyoko kilomita chache kutoka Vitshumbi vimedhibitiwa na waasi. Watu wanaendelea kuyakimbia maeneo ya Vitshumbi, Kanyabayonga, Butembo na katika wilaya ya Walikale.

DW, Goma.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW