DRC: Waasi wa ADF waua watu 10 huko Lubero
16 Januari 2025Waasi hao wa ADF walishambulia jana kijiji cha Makoko katika eneo la Lubero, Jimbo la Kivu Kaskazini. Wakati wa mashambulizi hayo, hakukuwa na askari wa Kongo katika kijiji hicho, ispokuwa wapiganaji wanaojulikana kama Wazalendo, ambao mara kadhaa wamekua wakishirikiana na vikosi vya Kongo.
Hayo yameelezwa na mbunge wa jimbo hilo David Sikuli, ambaye ameitolea wito serikali ya Kongo kuruhusu kutanuliwa kwa operesheni za pamoja Jeshi la Kongo na Uganda hadi kwenye maeneo yote wanakopatikana waasi hao wa ADF.
Eneo la Mashariki mwa Kongo linakabiliwa kwa miongo kadhaa na ghasia za makundi yenye silaha. Zaidi ya vikundi 120 vinapigania ushawishi, ardhi na rasilimali muhimu za madini, huku makundi mengine yakijaribu kutetea jamii zao. Ghasia hizo zimesababisha karibu watu milioni 7 kuyakimbia makazi yao.