DRC: Watu 25 wauawa na waasi mkesha wa Mwaka Mpya
1 Januari 2021Kiongozi wa wilaya ya Beni katika mkoa wa Kivu Kaskazini, Donat Kibuana ameliambia shirika la habari la AFP kuwa jeshi la serikali ya Kongo lilikuwa likiwafukuza waasi hao, lilipoiona miili ya wahanga hao ambao ''walivamiwa kwa kushtukizwa'' walipokuwa katika mashamba yao.
Soma zaidi: Wafungwa 900 watoroka katika uvunjaji gereza Congo Mashariki
Mauaji hayo yametokea katika kijiji cha Tingwe kilichoko umbali wa takribani kilomita nane kutoka mji wa Eringeti. Mkuu wa asasi za kiraia katika kijiji hicho Bravo Mohindo Vukulu amesema idadi ya waliouawa sio chini ya 30.
Jeshi liliarifiwa likashindwa kuchukua hatua
''Hatu hao walikuwa wamekwenda kwenye mashamba yao kujiandaa na mkesha wa sikukuu ya mwaka mpya, kisha, ADF ikawashambulia mmoja baada ya mwingine,'' amesema Vukulu, na kuongeza kuwa ''tulikuwa tumeliarifu jeshi la serikali kuwa waasi hao wamepita katika eneo hilo wakitokea mashariki na kuelekea kaskazini mashariki mwa mji wa Eringeti, lakini jeshi hilo halikuchukua hatua haraka.''
ADF ambayo ilianza kama kundi la waasi wa Kiislamu kutoka Uganda miaka ya 1990, ni mojawapo ya magenge makumi kadhaa ya wanamgambo wanaovuruga amani upande wa mashariki wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Soma zaidi: DRC: Wito watolewa FARDC na UPDF kuungana kukabili ADF-Nalu
Inashutumiwa kuwauwa raia wapatao 800 katika mkoa wa Kivu Kaskazini tangu kuanza kwa mwaka 2020, mkoa huo ukipakana na Uganda.
Mapato kwa njia za kihalifu
Kundi hilo hupata fedha kwa kufanya biashara haramu ya mbao, na maafisa wa Kongo hushuku kuwa baadhi ya wanajeshi wanahusika katika ghasia zinazofanywa na ADF. Kundi hilo lenyewe halijawahi kukiri kuhusika katika mauaji yoyote.
Hata hivyo, kuanzia Aprili 2019, kile kinachojulikana kama Dola la Kiislamu katika Ukanda wa Afrika ya Kati kimekuwa kikidai kuhusika na mashambulizi hayo ya mashariki mwa Kongo, bila hata hivyo kutoa ushahidi wowote.
Mwezi Julai Umoja wa Mataifa ulisema mashambulizi hayo yanaweza kuchukuliwa kama uhalifu dhidi ya ubinadamu na uhalifu wa kivita.
Tshisekedi apiga hatua nyingine kumuengua Kabila
Huko hayo yakijiri, rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Felix Tshisekedi amemteuwa seneta, ambaye atakuwa na jukumu la kuchunguza ikiwa rais huyo anaweza kujenga muungano wa kibunge ambao utamuwezesha kulivunja baraza la mawaziri la sasa ambalo linadhibitiwa na watu watiifu kwa rais mstaafu Joseph Kabila.
Soma zaidi: Rais Tshisekedi kuuvunja ushirikiano na upande wa Kabila
Seneta huyo, Modeste Bahati amepewa muda wa siku 30 kubainisha ikiwa ''Muungano Mtakatifu'' anaotaka kuunda Tshisekedi unaweza kuungwa mkono na wabunge wengi.
Tangazo la Ikulu ya rais mjini Kinshasa lililotolewa jana Alhamisi, lilisema muda huo unaweza kurefushwa mara moja.
Mwezi uliopita, Rais Tshisekedi alichukua uamuzi wa kuvunja ushirika wa kisiasa wenye utata wa kugawana madaraka baina yake na mtangulizi wake Joseph Kabila, akisema migawanyiko katika ushirika huo inakwamisha utekelezwaji wa mageuzi katika sekta za usalama na mahakama, ambayo yanaungwa mkono na Shirika la Fedha Ulimwenguni (IMF) na Benki ya Dunia.
Vyanzo: Reuters, AFP