DRC yaaga mashindano ya AFCON huko Morocco
7 Januari 2026
Katika mechi hiyo ya Jumanne mjini Rabat, timu ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo iliondolewa na Algeria iliyopata ushindi mwembamba wa bao 1-0, baada ya mchezaji wa Algeria Adil Boulbina kupachika bao maridadi kabisa nyakati za lala salama za mwishoni mwa muda wa ziada na kuzima kabisa matumaini ya timu ya Léopard ya DRC.
Algeria na DRC zilipambana vilivyo na mechi hiyo ilikuwa ikielekea kwenye mikwaju ya penalti na ndipo Boulbina alipopenya upande wa kushoto mnamo dakika ya 119 na kuingia eneo la hatari na kupiga shuti kali lililotikisa nyavu na kupelekea idadi kubwa ya mashabiki zaidi ya 18,800 wa Algeria kushangilia kwa kishindo.
Boulbina alikuwa shujaa asiyetarajiwa, baada ya kushiriki mechi yake ya pili tu katika mashindano hayo ya AFCON na alijumuishwa katika kikosi hicho baada ya kuichezea Algeria katika michuano ya Kombe la mataifa ya Kiarabu huko Qatar hivi karibuni.
Kauli ya Kocha na mashabiki wa DRC
Sébastien Desabre, ni Kocha wa timu ya DRC amesema ni wazi wamehuzunishwa na matokeo ya mechi hiyo na kusisitiza kuwa ulikuwa mchezo wa kiwango cha juu mno kati ya timu mbili bora.
" Bila shaka, tulipofungwa bao hilo muhimu, tulikatishwa tamaa. Wachezaji waliwajibika ipasavyo uwanjani, tulipambana hadi mwisho lakini kwa bahati mbaya, hilo halikutosha, " aliongeza Kocha huyo wa DRC.
Mwandishi wa DW aliyekuwa uwanjani huko Rabat, alizungumza na mashabiki wa DRC baada ya mechi hiyo kumalizika. Baadhi wameipongeza timu yao huku wengine wakikosoa maamuzi ya refa kuwa alikuwa akifumbia macho baadhi ya makosa ya wachezaji wa Algeria.
Timu ya Kongo inaweza angalau kujifariji kutokana na ukweli kwamba itacheza mechi ya mchujo mwezi Machi, ambapo ushindi dhidi ya New Caledonia au Jamaica utawawezesha kufuzu kushiriki michuano ya Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1974.
Katika mechi nyingine iliyochezwa Jumanne huko Marrakech, timu ya Cote d´Ivoire ilijipatia ushindi mnono wa mabao 3-0 dhidi Burkina Faso. Amad Diallo alipachika bao la kwanza mnamo dakika ya 20 na kufuatiwa na bao la Yan Diomande dakika 12 baadaye. Bazoumana Toure alifunga dimba kwa kupachika bao la tatu mnamo dakika ya 87.
Kalenda ya mechi za robo fainali kwenye AFCON hii huko Morocco tayari imefahamika. Siku ya Ijumaa ya Januari 9: Mali wataingia uwanjani dhidi ya Senegal na baadaye Cameroon watamenyana na wenyeji Morocco. Jumamosi, Nigeria itapambana na Algeria huku Misri ikishikana mashati na Cote d´Ivoire.