1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

DRC yaandaa maombolezo ya kitaifa kwa waliouawa na mafuriko

Mitima Delachance8 Mei 2023

Serikali ya Jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo inafanya maombolezo ya kitaifa kuwakumbuka zaidi ya watu 400 waliofariki mwishoni mwa juma kufuatia mafuriko.

Demokratische Republik Kongo Überschwemmungen
Picha: GLODY MURHABAZI/AFP

Mafuriko hayo yalisababishwa na mvua kubwa katika baadhi ya vijiji vya wilaya ya Kalehe jimboni Kivu Kusini.

Kulingana na maafisa wa serikali wa Kalehe miili ipatayo 400 imepatikana na tayari imezikwa.

Hadi sasa hali iliyotanda ni ya majonzi na machozi yanayoonekana kwenye nyuso za waathirika wa mafuriko hayo yaliyotokea katika vijiji vilivyoko pembezoni mwa Mto Chibira vya Chabondo hadi Nyamukubi katika kijiji cha Bushushu usiku wa kuamkia Ijumaa iliyopita.

Katika vijiji hivyo, miili ya waliokufa imefungwa katika magunia na kuzikwa ndani ya kaburi la pamoja.

Zaidi ya watu 400 wamethibitishwa kuuawa kutokana na mafuriko hayo.Picha: GLODY MURHABAZI/AFP

Shirika la kiraia linakadiria kuwa kuna watu wapatao elfu nne na mia tano ambao bado hawajaonekana, huku likihisi kwamba kadri muda unavyosonga zaidi, yamebakia matumaini kidogo sana ya kuwapata ndugu zao wakiwa hai.

Gavana wa jimbo la Kivu Kusini, Théo Ngwabidje anasema maafa haya yamesababisha uharibifu mkubwa na hali ya operesheni ya kibinaadamu kuwa ngumu zaidi.

''Kipaumbele cha kwanza kilikuwa kuizika katika hali nzuri miili ya waliopoteza maisha ili kuepuka magonjwa. Pia, ilitubidi kuwaangalia waliojeruhiwa. Waliojeruhiwa kidogo wanatibiwa kwenye vituo vya afya vya Kalehe, lakini pia tumeamua kuwapeleka wenye majeraha makubwa zaidi Bukavu. Sasa kipaumbele kingine ni kupata namna ya kuwahamisha waathirika ili kuwaweka mbali na maeneo yenye maafa. Hatua zote zinachukuliwa ili kushughulikia kwanza dharura, lakini pia kufanyia kazi suluhu zinazofaa kwa siku zijazo. Ni janga lililojitokeza, hatukujipanga. Lakini ni wajibu wetu kufanya maamuzi muhimu,'' Ngwabidje amesema.

Mvua kubwa iliyonyesha eneo la Kalehe Kivu kusini, ilisababisha maporomoko ya ardhi na mito kuvunja kingo zao, huku maafa makubwa yakitokea.Picha: GLODY MURHABAZI/AFP

Idadi ya watu waliokufa kutokana na mafuriko na maporomoko ya ardhi nchini Kongo yavuka watu 200

Ujumbe wa serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo kutoka mjini Kinshasa wakiwemo mawaziri wawili na naibu spika wa bunge unatarajiwa kufika katika vijiji vya Bushushu na Nyamukubi huko, Kalehe mchana huu ili kuomboleza na waathirika.

Mitima Delachance, DW, Bukavu.