1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

DRC yahesabu siku kabla ya uchaguzi mkuu wa Jumatano

17 Desemba 2023

Wagombea takriban Laki moja wajiandaa kuwania nafasi mbali mbali katika uchaguzi mkuu

Demokratische Republik Kongo | Binnenvertriebene im Flüchtlingslager Kanyaruchinya
Picha: Cunningham/Getty Images

Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo inajiandaa kuingia kwenye  uchaguzi mkuu Jumatano ijayo huku kiasi watu milioni 44 wakiwa wamejiandikisha kupiga kura katika nchi hiyo yenye kiasi wakaazi milioni 100. Wapiga kura watachagua rais,wabunge,magavana na viongozi wa serikali za mitaa.

Kuna wagombea wasiopungua 100,000 watakaowania nafasi mbali mbali kwenye uchaguzi huo,huku rais wa sasa Felix Tshisekedi akiwania muhula wa pili baada ya kuingia madarakani kupitia uchaguzi uliozusha utata mnamo mwaka 2018.

Uchaguzi wa mara hii huenda ukawa chachu ya kuimarisha Demokrasia au kusababisha machafuko mapya katika wakati ambapo mivutano ya kisiasa inatokota katika taifa hilo. Kutokana na ukubwa wa nchi hiyo ambao ni takriban sawa na lilivyo eneo zima la Ulaya ya Magharibi kuandaa uchaguzi ni suala gumu na hasa kwa upande wa miundombinu ya usafiri.

Nchi hiyo pia ni mojawapo ya nchi masikini kabisa duniani na kuna miundo mbinu michache tu yenye viwango vizuri wakati pia  tume yake ya uchaguzi CENI ikionesha kupambana kusambaza vifaa vya uchaguzi kwa zaidi ya watu 170,000.Wafuasi wa Katumbi waridhishwa kuruhusiwa kuwania urais DRC

Mchambuzi wa masuala ya kisiasa Gaucher Kizito ameliambia shirika la habari la AFP kwamba uchaguzi unapaswa kufanyika bila matatizo katika maeneo yenye wakaazi wengi ingawa itakuwa shida katika maeneo ya vijijini uchaguzi huo kwenda vizuri kutokana na ukosefu wa usalama na barabara mbovu.

Ijumaa iliyopita baraza la usalama la Umoja wa Mataifa liliidhinisha ombi lililotolewa na serikali ya Kongo la kutaka kikosi cha kuweka amani cha Umoja huo kinachoondoka nchini humo kutoa msaada wa kusimamia shughuli za usafirishaji vifaa vya uchaguzi katika maeneo matatu yanayokabiliwa na machafuko ya mashariki mwa nchi hiyo.

Wafuasi wa mgombea Martin Fayulu katika kampeini mjini GomaPicha: Benjamin Kasembe/DW

Wasiwasi

Kwa mujibu wa mwanadiplomasia mmoja aliyezungumza na shirika la habari la AFP sio vituo vyote vya kupiga kura vitafunguliwa Desemba 20 kutokana na ukosefu wa vifaa.Mwanadiplomasia huyo amesema baadhi ya vituo huenda vikafunguliwa siku moja au mbili baadae au hata pengine baada ya hapo.Mnamo siku ya Jumamosi shirika la kutetea haki za binadamu,Human Rights Watch lilitoa tahadhari kwamba machafuko yanaweza kutishia kutofanyika uchaguzi.

Mashambulizi ya mitandaoni kwa wagombea urais KongoShirika hilo  limeorodhesha machafuko yaliyofanyika kati ya wafuasi wa vyama vinavyokinzana nchini humo tangu mwanzoni mwa mwezi oktoba,ambayo yamesababisha kushuhudiwa matukio ya watu kushambuliwa,unyanyasaji wa kingono na kuripotiwa kwa kifo cha mtu mmoja.Na kutokana na historia ya misukosuko ya kisiasa nchini Kongo,uchaguzi uliopita wa mwaka 2018 ulioibua mvutano mkubwa ulifanyika kwa utulivu na kuonekana kwa mara ya kwanza kwa hatua ya  kukabidhiana kwa amani madaraka.

Japokuwa mara hii wachambuzi wa kisiasa wanasema kutovumiliana kumejitokeza wazi kwenye mijadala huku mwanadiplomasia aliyezungumza na AFP akisema hotuba za chuki zimeonesha kutawala zaidi kuliko sera na mipango ya wagombea.Juu ya hilo suala linalotiwa wasiwasi mkubwa ni kuhusu uwezekano wa kutokea udanganyifu huku wagombea wote wa vyama vikuu vya upinzani wakitowa mwito wa kuwepo uangalizi makini.

Rais Felix Tshisekedi anayewania muhula wa pili madarakaniPicha: Pool Vlad Vanderkelen/Belga/picture alliance

Malalamiko ya Upinzani

Upinzani kwa muda mrefu wamekuwa wakiituhumu serikali kwamba imeweka watu wake kwenye tume ya uchaguzi na mahakama ya katiba ambayo ndio chombo cha kutowa maamuzi ya mwisho katika migogoro ya uchaguzi.

Kuna Jumla ya wagombe 19 wa kinyang'anyiro cha uchaguzi wa rais,ambapo miongoni mwa wagombea wakuu walioko katika kambi ya upinzani ni pamoja Moise Katumbi,mfanyabiashara tajiri na gavana wa zamani ambaye anaungwa mkono na wagombea wanne waliojitoa.

Mgombea urais wa upinzani Moise Katumbi Picha: Nicolas Maeterlinck/picture alliance

Mgombea mwingine ni Martin Fayulu  aliyewahi kugombea uchaguzi uliopita na kudai alikuwa mshindi halali wa uchaguzi huo. Yuko pia Denis Mukwege ambaye ni  Daktari wa wanawake na mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel.Uchaguzi utafanyika Desemba 20 na matokeo yakitarajiwa kutangazwa siku kadhaa baadae.