DRC yaishutumu Rwanda kwa shambulio la mizinga
11 Juni 2022Katika taarifa yake, jeshi la Congo limesema kwamba vikosi vya Rwanda viliyashambulia kwa mizinga maeneo mawili ya Rutshuru katika jimbo la Kivu Kaskazini mnamo siku ya Ijumaa mchana. Taarifa hiyo imeongeza kuwa watoto waliouawa walikuwa na umri wa miaka 6 na 7 na mwingine amejeruhiwa katika shambulio hilo. "Mbali na idadi ya watu, jeshi la Rwanda lililipua shule nzima kwa mabomu. Hili linachukuliwa kuwa uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu," ilisema taarifa hiyo. Soma pia DRC yadai askrai 500 wa Rwanda wameingia nchini mwake
Madai hayo yanafuatia kauli iliyotolewa na wizara ya ulinzi ya Rwanda mapema siku ya Ijumaa, ambayo ililituhumu jeshi la Congo kwa kurusha maroketi mawili ndani ya eneo lake. Kwenye taarifa yake, wizara ya ulinzi ya Rwanda ilisema kuwa "jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, FARDC, lilirusha roketi mbili hadi Rwanda kutoka eneo la Bunagana," magharibi mwa nchi hiyo majira ya saa sita mchana". Iliongeza kuwa hapakuwa na majeruhi lakini wakaazi wa eneo hilo wameingiwa na hofu.
Aidha taarifa hiyo ilisema mashambulizi ya aina hiyo ya makombora ya vikosi vya Congo yalifanyika Machi 19 na Mei 23 na kusababisha hasara na kuharibu mali.
Shutuma hizo zinatolewa wakati uhusiano wa mataifa hayo jirani ukizidi kuzorota kwa kasi, kutokana na kuzuka upya kwa wanamgambo wa M23 katika eneo la mashariki mwa Congo ambalo limekumbwa na machafuko.
Rwanda yasema iko tayari kulipiza kisasi iwapo Congo itashambulia tenaCongo-Kinshasa inaituhumu Rwanda kwa kuwaunga mkono wapiganaji wa M23 na Kigali imekanusha madai hayo. Siku ya Ijumaa pia jeshi la Congo liliyakana madai ya Rwanda ya kurusha kombora ikipendekeza kwamba Rwanda imepanga shambulio hilo kwenye ardhi yake katika jitihada za "kudanganya au kupotosha jumuiya ya kimataifa".
Umoja wa Afrika, Umoja wa Mataifa na wadau wengine wametoa wito wa kuwepo utulivu katikati mwa mvutano wa kikanda. Mfalme Philippe wa Ubelgiji, ambaye kwa sasa yuko nchini Congo kwa ziara ya kihistoria ya siku sita katika koloni la zamani la Ubelgiji, amepanga kuzuru mji wa mashariki wa Bukavu siku ya Jumapili.