DRC yatakiwa kuheshimu uhuru na haki za raia
20 Aprili 2015Wito huo umetolewa jana na Mkuu wa kikosi cha Umoja wa Mataifa cha kulinda amani nchini Kongo-MONUSCO, Martin Kobler,wakati akihojiwa na shirika la habari la Ufaransa, AFP.
Kobler amesema hali ya kisiasa lazima iwe ya uhakika, ikiwemo nafasi ya upinzani, nafasi ya vyama vya kiraia na kwa watetezi wa haki za binaadamu. Amesema ni muhimu kuwa wanawasiliana na serikali kuhusu masuala hayo na jukumu la MONUSCO ni pamoja na kutetea haki za binaadamu na kuwalinda raia.
Amefafanua kwa kufanya hivyo siyo kwamba wanaingilia masuala ya ndani ya Kongo. Kobler amesema wanasiliana na serikali ya Kongo kila siku wakijaribu kuangalia namna ya kuendeleza ushirikiano wa kijeshi kwa sababu hali inazidi kuwa mbaya kwenye eneo la mashariki.
Wakati jeshi la Kongo linasema operesheni yake ya kijeshi imewaua, kuwakamata au kuwalazimisha mamia ya wapiganaji wa waasi kujisalimisha, Kobler amesema hawezi kuthibitisha kuhusu madai hayo, kwa sababu MONUSCO kwa sasa haishirikiani na jeshi hilo.
Kongo yakumbwa na wasiwasi
Wasiwasi umeongezeka nchini Kongo tangu watu kadhaa walipokufa wakati wa maandamano ya kupinga kupitiwa upya sheria ya uchaguzi, yaliyofanyika mwezi Januari mwaka huu, ambayo wakosoaji wanasema huenda ikamruhusu Rais Joseph Kabila kuendelea kubakia madarakani, hata baada ya muda wake wa mwisho kukamilika.
Uchaguzi wa rais na wabunge umepangwa kufanyika Novemba mwaka ujao wa 2016, lakini upinzani umemshutumu Rais Kabila kwa kujaribu kutafuta juhudi za kuhakikisha anabakia madarakani, kuliko kuachia madaraka baada ya kumaliza kipindi cha mihula miwili kama ilivyo kwa mujibu wa katiba ya Kongo.
Kukamatwa kwa wanaharakati wa demokrasia mwezi Machi, huku baadhi yao wakiwa bado wanashikiliwa, pia kumesababisha makundi ya kimataifa ya kutetea haki za binaadamu kulaani kitendo hicho.
Tangu mwezi Januari, viongozi wa upinzani wamelaani kitendo cha kukatwa kwa mitambo ya mawasiliano katika baadhi ya vyombo vya habari pamoja na kukamatwa kwa waendesha kampeni wa haki na wakosoaji wa serikali. Kwa upande wake serikali imewashutumu wanaharakati kwa kujiona wako juu ya sheria.
Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo yenye utajiri mkubwa wa madini, ambayo ilikumbwa na vita mara mbili mfululizo kabla ya Rais Kabila alipoingia madarakani mwaka 2001, imekuwa ikipambana na makundi yenye silaha yanayoendelea kusababisha ghasia kwenye eneo la mashariki mwa Kongo.
Mwandishi. Grace Patricia Kabogo/AFPE
Mhariri: Yusuf Saumu