1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

DRC yatangaza baraza lake jipya la mawaziri la watu 54

29 Mei 2024

Nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, serikali iliyo na mawaziri 54 hatimaye imetangazwa miezi miwili baada ya Judith Suminwa kuteuliwa kama Waziri Mkuu.

DR Kongo |  Judith Tuluka Suminwa und Felix Tshisekedi
Picha: DRC Presidency/Handout/Xinhua/picture alliance

 

Miongoni mwa manaibu sita wa waziri mkuu, Jean-Pierre Bemba amepewa wizara ya uchukuzi na hivyo kuiacha wizara ya ulinzi itakayoongozwa sasa na Guy Kabombo Mwadiambita anayeingizwa serikalini kwa mara ya kwanza. Jean-Pierre Lihau anabaki na  wizara ya kazi za umma, huku watu wawili wapya maarufu wakiingia serikalini. Nao ni Guylain Nyembo aliyekuwa mkuu wa ofisi ya Rais Félix Tshisekedi ambaye sasa anakaimu Wizara ya Mipango na Jackmain Shabani, aliyekuwa mshauri maalum wa Rais ambaye anakuwa makamu Waziri Mkuu ahusikaye na Mambo ya Ndani. 

Mawaziri wengine ni kama Aimé Boji, Eve Bazaiba, Alexis Gisaro na Guy Loando ambao wanabaki kila mutu pa nafasi yake yaani bajeti ya taifa, mazingira, miundombinu na mipango ya maeneo, huku Muhindo Nzangi aliyekuwa Waziri wa Elimu ya Juu na Vyuo Vikuu akiwa sasa Waziri wa maendeleo Vijijini. Constant Mutamba aliyejulikana kuwa mpinzani, tayari ameteuliwa kuwa waziri wa sheria. 

Serikali mpya imetangazwa miezi minne baada ya Rais Tshisekedi kuapishwa

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Félix TshisekediPicha: DW

Baadhi ya mawaziri wengine ni Doudou Fwamba anayejiunga na serikali kwa mara ya kwanza akiwa waziri wa fedha na hivyo kuchukua nafasi ya Nicolas Kazadi ambaye anashukiwa kuhusika na ubadhirifu wa fedha za umma. Julien Paluku, waziri wa zamani wa viwanda sasa atashikilia wizara ya biashara ya nje. Molendo Sakombi anatoka wizara ya mikataba ya ardhi na kuchukuwa hidrokaboni, huku Kizito Pakabomba akisimamia wizara muhimu ya madini iliyokuwa ikiongozwa na Antoinette Samba.

Bunge la Kongo lamchagua Vital Kamerhe kuwa spika

Miongoni mwa mawaziri ambao hawakuguswa ni pamoja na Patrick Muyaya anayebaki kwenye wizara ya mawasiliano, Roger Kamba wa afya ya jamii pamoja na Gilbert Kabanda wa utafiti wa kisayansi bila kudahau Irene Esambo ahusikae na maswala ya walemavu. Masuala ya kimila sasa yatasimamiwa na mmoja wa viongozi wa asili. Naye ni Mwami Jean-Baptiste Ndeze, aliyeteuliwa kuwa makamu Waziri wa Mambo ya Kimila. 

Serikali hiyo mpya inayo wanawake 18 imetangazwa miezi minne baada ya Rais Tshisekedi kuapishwa na miezi miwili baada ya Judith Suminwa kuteuliwa kama waziri mkuu. Kwa mujibu wa ofisi ya mawasiliano ya rais Tshisekedi, kuchelewa huko kulifuatia pande tofauti za muungano tawala kuchukuwa muda kuelewana.

Mwandishi: Jean Noel 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW