1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waasi wa M23 wakabidhi kambi ya jeshi mashariki ya Kongo

7 Januari 2023

Waasi wa M23 wameirudisha kambi ya kijeshi mashariki mwa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo katika hatua ya kutimiza ahadi yake ya kuondoka kutoka kwenye maeneo waliyoyanyakua na kuyadhibiti kwa miezi kadhaa.

Kongo I Treffen zwischen EACRF und  M23-Rebellen
Picha: Guerchom Ndebo/AFP

Wakazi wa eneo hilo la mashariki ya Kongo siku ya Ijumaa walielezea furaha yao wakati waasi hao walipokabidhi vifaa na kambi ya kijeshi ya Rumangabo, kubwa zaidi katika eneo la mashariki mwa mkoa wa Kivu kaskazini. Hata hivyo wakazi hao pia wamesema bado wametawaliwa na wasiwasi. 

Kongo-Waasi wa M23 wakilinda wakati wa hafla ya makabidhiano ya kambi ya Rumangabo.Picha: Guerchom Ndebo/AFP

Hafla ya kukabidhi kambi hiyo ya Rumangabo kwa vikosi vya kulinda amani vya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EACRF) inaashiria mwanzo wa kuondoka kwa wapiganaji wa kundi la M23 kutoka kwenye mji wa kimkakati wa kijeshi wa Rumangabo, ulio kilomita 40 kaskazini mwa mji mkuu wa mkoa Goma, ambao waasi waliuteka mwishoni mwa mwezi Oktoba.

Kwa mujibu wa waandishi wa habari wa shirika la AFP walioruhusiwa kuripoti juu ya makabidhiano hayo, shughuli hiyo ilisimamiwa na vikosi vya Kenya vya kulinda amani vilivyopelekwa nchini Kongo na Jumuiya ya Afrika Mashariki, na kwamba shughuli hiyo ya jana inafuataia makabidhiano kama hayo ya mwezi uliopita ya kambi ya Kibumba, iliyo karibu kilomita 20 kusini mwa Kongo.

Maafisa wa Jeshi la Kanda ya Afrika Mashariki (EACRF) waliopo nchini DR KongoPicha: Guerchom Ndebo/AFP

Jenerali Emmanuel Kaputa Kasenga, naibu kamanda wa kikosi cha Afrika Mashariki amesema kudhibiti tena kambi ya Rumangabo kunaashiria hatua muhimu katika juhudi zinazoendelea za kuleta amani na utulivu katika eneo la mashariki nchini jamumuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Naibu kamanda huyo amesema vikosi vya Jumuiya ya Afrika Mashariki vitaendelea kusimamia utaratibu wa kurudishwa maeneo yaliyotekwa na waasi wa M23 na ameyataka makundi mengine kufuata utaratibu huo na kusalimisha silaha zao.

Kiongozi wa M23, Imani Nzenze alisema katika hafla hiyo ya Ijumaa. Kwamba wao wanataka amani na wataendelea kujumuika katika mchakato huo wa kutafuta amani na ndio sababu kundi lake la M23 limeamua kukabidhi rasmi kambi ya kijeshi ya Rumangabo kwa kikosi hicho cha Afrika mashariki.

Kiongozi wa M23, Kanali Imani NzenzePicha: Guerchom Ndebo/AFP

Viongozi wa kikanda walifanikisha kufikiwa makubaliano kati ya pande hasimu mnamo mwezi Novemba hatua inayolifanya kundi la M23 likiondoka na kukabidhi maeneo waliyoanyakua hatua itakayowawezesha watu waliogeuka wakimbizi wa ndani kurejea katika makazi yao waliyoyakimbia.

Vyanzo: AFP/RTRE