1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Drones za kamikaze zaushambulia mji wa Kiev-Ukraine

Sylvia Mwehozi
17 Oktoba 2022

Ukraine imesema hii leo kwamba Urusi imeushambulia mji wa Kiev kwa ndege zisizo na rubani aina ya kamikaze, katika kile ambacho ofisi ya rais wa Ukraine imekitaja kuwa ni kitendo cha kukata tamaa kwa Urusi.

USA | Rüstung | Switchblade Drohne
Picha: AeroVironment/abaca/picture alliance

Kwa mujibu wa mwandishi wa habari wa shirika la habari la AFP, ndege zisizo na rubani zilionekana zikishuka chini kwenye wilaya ya kati ya mji mkuu wa Kiev, huku maafisa wa polisi wakijaribu kuzilenga kwa kutumia silaha na moshi mkubwa ukionekana kutoka eneo la milipuko katika mji huo.Watu wanane wauawa baada ya Urusi kushambulia soko Ukraine

Shambulio hilo linatokea takribani wiki moja baada ya Urusi kuanzisha mashambulizi makubwa ya makombora ya siku mbili katika miji kadhaa nchini Ukraine ambayo yalitatiza usambazaji wa nishati na maji kote nchini. Ving'ora vya mashambulizi ya anga vilisikika mjini Kiev muda mfupi kabla ya mlipuko wa kwanza majira ya asubuhi vikifuatiwa baadae na ving'ora kote nchini.

Hali ilivyo mjini Kiev siku ya Jumatatu 17.10.2022Picha: Gleb Garanich/REUTERS

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amelaani mashambulizi hayo akiyataja kuwa ugaidi dhidi ya raia. Ameongeza kuwa adui anaweza kuishambulia miji lakini hatowavunja moyo.

Meya wa mji wa Kiev  Vitali Klitschko amedai kwamba jengo moja la makaazi ya raia katika wilaya moja mjini humo limeshambuliwa huku watu 18 wakiokolewa lakini wawili bado wamekwama ndani. Mkuu wa shirika la reli Alexander Kamyshin, naye alithibitisha mashambulizi karibu na kituo kikuu cha reli akisema kwamba panahitajika kwa haraka silaha za mifumo ya anga kuweza kukabiliana na mashambulizi. Inakadiriwa kwamba vikosi vya Urusi vimefyatua makombora mawili na takribani mashambulizi ya anga yapatayo 26 na kurusha zaidi ya maroketi 80.

Miji 40 ya Ukraine yashambuliwa kwa makombora ya Urusi

01:26

This browser does not support the video element.

Wakati huohuo kinu cha nyuklia cha Zaporizhzhia kimekatwa mawasiliano kutoka gridi ya taifa ya umeme hii leo kufuatia mashambulizi ya Urusi na kusababisha majenerata ya dizeli kuanza kutumika. Itakumbukwa kwamba vikosi vya Urusi vinakidhibiti kinu hicho kilichoko kusini mwa Ukraine, muda mfupi tangu kuanza uvamizi wake karibu miezi minane iliyopita lakini kinaendeshwa bado na wafanyakazi wa Ukraine.

Na mkuu mpya wa ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa Volker Turk ameelezea wasiwasi juu ya mzozo unaozidi kuongezeka nchini Ukraine wakati akianza kazi hii leo na kusisitiza kwamba raia ni lazima walindwe.

"Ni wazi kwamba ongezeko lolote la vita linatusumbua sana na linatokea nchini Ukraine, linatokea pia katika sehemu nyingine nyingi za dunia. Na tunahitaji kurejea kwenye ufahamu wa kina juu ya kwa nini ni muhimu kuheshimu sheria za kimataifa. Kwa sababu, inawahusu binadamu ambao hawahusiki katika vita na wanahitaji kulindwa, hivyo ndivyo sheria ya kimataifa inavyosema."

Kamishina huyo raia wa Austria ambaye amefanya kazi ndani ya mifumo ya Umoja wa Mataifa ametoa wito wa kupunguzwa kwa mvutano nchini Ukraine.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW