1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Droni za Urusi zafanya mashambulizi Kyiv

Angela Mdungu
28 Mei 2023

Mji mkuu wa Ukraine, Kyiv, ulikabiliwa na mashambulizi makubwa zaidi ya ndege zisizo na rubani za Urusi usiku wa kuamkia Jumapili. Mtu mmoja ameuwawa kutokana na mashambulizi hayo.

Ukraine | Krieg | russischer Drohnenangriff auf Kiew
Picha: Valentyn Ogirenko/REUTERS

Afisa wa ngazi ya juu wa jeshi mjini Kyiv Serhii Popko amesema kuwa mashambulizi hayo yaliyofanyika wakati mji huo ukisherehekea kumbukumbu ya kuanzishwa kwake yalidumu kwa  saa tano na yalifanywa kwa kutumia ndege zisizo na rubani aina ya Shahed zilizotengenezwa Iran. Ukraine ilifanikiwa kudungua zaidi ya droni 40.Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amevipongeza vikosi vya ulinzi wa anga kwa kudungua ndege hizo. Kulingana na meya wa mji wa Kyiv, Vitali Klitscho, aliyeuwawa kutokana na mkasa huo ni mwanamume mwenye miaka 41. Mwanamke mwenye miaka 35 amejeruhiwa na yuko hospitali kwa matibabu baada ya kupata majeraha yaliyosababishwa na kuangukiwa na mabaki ya droni yaliyoangukia kwenye ghorofa na kusababisha moto.

Jeshi la anga la Ukraine lilisema Jumamosi usiku kuwa kati ya ndege hizo zisizo na rubani 54 zilizorushwa katika maeneo mengi ya nchi hiyo, 52 zilidunguliwa na mfumo wa ulinzi wa anga. Naye Gavana Oleh Syniehubov wa jimbo la Kaskazini mashariki la Kharkiv amesema mwanamume mmoja wa miaka 60, na mwanamke mwenye miaka 61 wameuwawa katika mashambulizi mawili tofauti ya mabomu.

Kwa mujibu wa mamlaka za Kyiv Mashambulizi hayo ya droni yaliyofanywa na Urusi dhidi ya Ukraine ni ya 14 kwa mwezi huu na yanaelezwa kuwa yalifanyika kwa wakati mmoja yakielekezwa katika pande tofauti. 

Moto uliotokana na moja ya mashambulizi ya droni mjini KyivPicha: Alex Babenko/AP/dpa/picture alliance

Mji wa Kyiv umepatwa na mkasa huo wakati ukiadhimisha siku ya kuanzishwa kwake. Kwa kawaida siku hiyo huadhimishwa kwa matamasha, maonesho kwenye mitaa pamoja na na kurusha fataki.

Katika hatua nyingine, waziri wa mambo ya kigeni wa Urusi, Sergei Lavrov ameyatahadharisha mataifa ya magharibi dhidi ya makubaliano yao ya kuipatia Ukraine ndege za kivita chapa F 16. Amesema kwa kufanya hivyo ni sawa na ''kucheza na moto" na kuwa hatua hiyo inauchochea mzozo. Lavrov meyasema hayo katika mahojiano yake na televisheni ya Urusi na kushutumu vikali jaribio la Marekani na Uingereza kuidhoofisha Urusi.

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW