1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Droo ya Kombe la Dunia kufanyika Qatar

28 Machi 2022

Mipango ya kinyang'anyiro cha Kombe la Dunia 2022 itashika kasi wiki hii, ambapo droo ya mashindano hayo maarufu duniani itafanywa nchini Qatar Ijumaa hii Aprili mosi.

Schweiz Zürich | Auslosung Fußball-WM in Katar
Picha: ULMER Pressebildagentur/imago images

Timu zitafahamu hatima yao, ijapokuwa kutokana na mchakato mgumu wa kufuzu katika baadhi ya maeneo, na mzozo kati ya Urusi na Ukraine, ina maana washiriki wote 32 hawajajulikana. Mabingwa watetezi Ufaransa, pamoja na Brazil, Argentina, England, Ubelgiji, Ujerumani na Uhispania watakuwepo, ijapokuwa mabingwa wa Ulaya Italia watakosa.

Kombe la Dunia litafanyika Novemba na Desemba ili kuepusha joto kali la Juni na Julai katika eneo la Ghuba, na litasababisha mparanganyiko, hasa katika ligi za Ulaya. Pia limekumbwa na ukosoaji kuhusu haki za wafanyakazi, ijapokuwa serikali ya Qatar na FIFA zinasema hatua zimepigwa za kuboresha mazingira ya kazi. Msikilize Rais wa FIFA Gianni Infantino "Haki za binaadamu na ulinzi wa haki za binaadamu katika kiwango cha kimataifa ni suala la kipaumbele kwa FIFA. tumeliweka kwenye sheria zetu na nadhani sisi ndio wa kwanza kifanya hivyo katika mikataba yetu. Tuliliweka hilo kama sharti la mchakato wa kutuma maombi ya uwenyeji wa mashindano yetu yote na popote tunapokwenda uliwenguni bila shaka tunaangazia haja ya kulinda haki za binaadamu. linapokuja suala la Qatar haswa, nadhani tunapaswa kuwa wakweli pia na kukiri kuwa maendeleo mengi yamefanywa. Bila shaka mengi zaidi yanaweza kufanywa kila mahali, kila wakati."

Qatar imetumia mabilioni ya dola ili kuwa mwenyeji wa tamasha hilo la soka, kwa kujenga viwanja vya kisasa kabisa na vituo vya mazoezi, pamoja na kuboresha na kujenga miradi ya miundo mbinu.

Canada yavunja ukame wa miaka 36

Na hakika Subira huvuta heri, maana baada ya miaka 36 ya kusubiri, hatimaye Canada ni miongoni mwa timu zitakazojua hatima zao katika mashindano hayo ya Qatar. Canada wamefuzu katika mashindano hayo kwa mara yao ya pili baada ya kuwapiga jana Jamaica 4-0. Milan Borjan ni Kipa wa Canada

Nyota wa Canada Alphonso DavisPicha: John Raoux/AP Photo/picture alliance

"Nimekuwa katika mpango huu kwa miaka 12 sasa, 12, 13 sasa, na kumekuwa na matukuo mengi sana ya kukatisha tamaa katika miaka hiyo yote na sasa hii ni Canada mpya, undugu mpya, familia mpya, kila kitu kipya. nna furaha sana kuwa Mcanada. na nna furaha kuwa hapa. nna furaha kuwa mlinda mlango wa Canada na nna furaha kuleta kitu kizuri kwa Canada, baada ya Canada kunipa fursa hii, maisha mapya, kila kitu kipya. Kwa hiyo naipa Canada maisha mapya katika kandanda,

Timu nyingine inayotarajia kutimiza ndoto yake ni Macedonia Kaskazini ambayo kesho itashuka dimbani katika mechi ya mchujo dhidi ya Ureno yake Cristiano Ronaldo. Macedoniia kaskazini waliwaondoa mabingwa wa Ulaya Italia na sasa wana dakika 90 tu za kutimiza ndoto ya nchi nzima ya kutinga katika Kombe la Dunia kwa mara yao ya kwanza kabisa.

Nadhani mojawapo ya njia za kutumia ili kutimiza lengo hilo ni kama inayopangwa kutumiwa na Misri. Kocha wa timu ya taifa ya soka ya Misri Carlos Queiroz amesema timu hiyo itajilinda zaidi kwa "kucheza na wachezaji 16 nyuma" ili kutetea ushindi wao wa bao 1-0 dhidi ya Senegal watakapokutana kesho Jumanne katika mechi ya mchujo wa raundi ya pili ya kuwania kuingia kwenye michuano ya kombe la dunia.

Kocha huyo mzaliwa wa Msumbiji na aliyewahi pia kuwa meneja wa klabu ya Real Madrid na meneja msaidizi wa Machester United, amesema timu yake inastahili kushinda mchuano huo dhidi ya Senegal na kwa hivyo kila mchezaji anapaswa kuongeza juhudi mara mbili.

afp, dpa, ap

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW