"Dunia ilishindwa kuzuia mauaji Rwanda, Bosnia"
24 Mei 2013Ban Ki-moon amesema eneo la Maziwa Makuu limekumbwa na machafuko ambayo yamegharimu maisha ya watu wengi wasio na hatia wakati jamii ya kimataifa ikiendelea kuweka mikakati isiyozaa matunda kwa miongo kadhaa sasa.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kumaliza ziara yake nchini Rwanda akitokea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Katibu huyo mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema ikiwa hali ya mambo itaendelea kuwa ilivyo sasa, basi hakuna maendeleo bila amani na wala hakutakuwa na amani bila maendeleo.
"Mchakato wa amani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na utekelezwaji wake ni ndiyo nafasi muhimu ya maendeleo endelevu ya kanda hii nzima daima. Ninawahimiza marais wote na kila mmoja kuwa kutekeleza mchakato huo na kuheshimu majukumu yao juu ya hilo."
Dunia ilishindwa Rwanda, Bosnia
Alihoji Ban Ki-moon, ambaye alikuwa wazi kwa kusema kwamba Umoja wa Mataifa na jamii ya kimataifa walishindwa wakati yakitokea mauaji ya kimbari nchini Rwanda mwaka 1994 na mwaka uliofuata wakashindwa tena kwenye mauaji ya Srebrenica kwenye vita vya Bosnia-Herzegovina ambapo watu 8,000 waliuawa.
Kutokana na uzoefu huo akasema jamii ya kimataifa haiwezi kukaa kando wakati mambo yakiendelea kuharibika mashariki mwa DRC. Ban Ki Moon amesema kwamba ili kutekeleza maazimio ya kuleta amani mashariki mwa DRC ndiyo maana Umoja wa Mataifa ukatuma kikosi zaidi cha kulinda amani mashariki mwa nchi hiyo.Amekiri wazi kwamba mikataba kadhaa ya awali kuhusu DRC haikutekelezwa lakini kwamba kwa sasa wamepania.
"Mikataba kadhaa hapo awali ilisainiwa lakini haikuheshimiwa lakini wakati huu tutahakikisha tunatekeleza mikakati hii ili watu wa eneo hili waweze kuishi kwa amani na usalama bila woga."
Jana Katibu Mkuu huyo alifanya mazungumzo yaa faragha na Rais Paul Kagame na baadaye wakakutana na mawaziri mbalimbalikwenye mjadala wa pamoja.
Kwa upande mwingine Rais wa Benki ya Dunia, Jim Yong Kim, ambaye anafuatana na Ban Ki-moon, amesema Benki yake inaunga mkono michakato na juhudi kuleta amani ya kudumu kwenye eneo hilo kwa kusaidia miradi mbalimbali ya maendeleo kama vile miundombinu ya barabara, umeme, afya na elimu.
Tayari Benki ya Dunia imekwishatangaza kutoa dola bilioni 1 za Kimarekani kusaidia miradi hiyo.
Mwandishi: Sylvanus Karemera/DW Kigali
Mhariri: Mohammed Khelef