1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Dunia inahitaji hatua thabiti za kulinda mazingira

26 Januari 2021

Mjumbe wa Marekani anayeshughulikia maswala ya tabia nchi John Kerry amesema dunia inahitaji hatua thabiti kupambana na athari zinazotokana na mabadiliko ya hali ya hewa la sivyo mafanikio ya uchumi yatarudi  nyuma

Deutschland | John Kerry | Münchner Sicherheitskonferenz
Picha: picture-alliance/dpa/F. Hörhager

Bwana John Kerry aliyewahi kuwa waziri wa mambo ya nje ya Marekani ametoa mwito huo kwenye mkutano wa dunia unaojadili masuala ya tabia nchi chini ya udhamini wa serikali ya Uholanzi. Kerry amesema njia thabiti ni kuyazingatia mabadiliko ya tabia nchi kama hali ya dharura na kuimarisha juhudi za ulimwengu kwa lengo la kupunguza utoaji hewa chafu zinazoharibu mazingira ili kudumisha kiwango cha nyuzi joto 1.5 kwa mujibu wa mkataba wa Paris.

John Kerry ametanabahisha kwamba ongezeko la joto linaelekea kufikia nyuzi joto kati ya 3.7 na 4.5 kipimo cha celsius. Mjumbe huyo wa Marekani amesema majanga ya dhoruba pia yanasababisha hasara ya mabilioni ya dola nchini Marekani kila mwaka.

Bwana Kerry amesema ni bora kuzuia madhara na kuyadhibti kuliko kuacha yatokee na kuyashughulikia baadae. Viongozi wapatao 20 wa dunia wamezungumza kwenye mkutano huo kwa njia ya video sambamba na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres. Wakuu wa taasisi za fedha pia wameshiriki kwenye mkutano huo wa siku mbili.

Maandamano ya vijana kuhusu mazingira nchini UholanziPicha: Ana Fernandez/ZUMAPRESS.com/picture alliance

Viongozi kadhaa wa nchi wameahidi kutenga fedha zaidi kwa ajili ya kutimiza  malengo hayo. Kansela wa Ujerumani Angela Merkel ameahidi kwamba serikali yake itaonzega fedha kwa ajili ya bima ya kufidia madhara yanayosababishwa na majanga asili kwenye nchi zinazoendelea.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesisitiza umuhimu wa kuwekeza katika juhudi za kupambana na athari zinazosababishwa na mabadiliko ya tabia nchi na hasa kwenye nchi masikini.

Amesema kuunga mkono hatua za kujenga mazingira ni muhimu sana kimaadili, kiuchumi na kijamii na kwamba hatua hizo ni pamoja na kuweka mazingira yatakayozuia mafuriko, kutoa tahadhari za mapema, kuwapa wakulima ushauri bora juu ya hali ya hewa na kilimo bora. Guterres ametoa mwito wa kutenga asilimia 50 ya bajeti ya hali ya hewa kwa ajili ya kutimiza malengo hayo.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW