1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Dunia inakabiliwa na uharibifu wa ardhi ya kilimo

16 Desemba 2024

Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la UNCCD Ibrahim Thiaw katika mazungumzo ya COP16 yanayoshughulikia maswala Bio Anuai amesema dunia inakabiliwa na uharibifu wa ardhi ya kilimo hadi kufikia asilimia 40.

Viazi | Kilimo
Kilimo cha viaziPicha: Florence Lo/REUTERS

Rais wa COP16, Abderrahman Al-Fadhli, ambaye pia ni Waziri wa Mazingira, Maji na Kilimo wa Saudi Arabia, amesema ukame na uharibifu wa ardhi unachochea sio tu uhamiaji wa watu kutoka vijijini kwenda mijini na uhamiaji wa kuvuka mipaka bali pia ukame unachochea migogoro.

"Sehemu kubwa ya migogoro inayohusiana na rasilimali au kukosekana kwa utulivu wa kisiasa inahusishwa na uharibifu wa ardhi na kupoteza rasilimali, mambo ambayo husababisha harakati za watu kuyahama maeneo yao. Uhamiaji huu hutokea kutoka vijijini kwenda mijini au hata watu kuvuka mipaka."

Mkuu wa UNCCD, Ibrahim Thiaw, katika ufunguzi wa mkutano wa COP16 pia alisema kwamba ardhi si njia ya kujipatia riziki tu bali ni mustakabli wa watu, imebeba hadithi, ndoto na matumaini yao kwa hivyo udongo uliokuwa na rutuba na ambao watu waliutegemeza sasa unageuka kuwa mfano wa tasa kwa maana kwamba hauzalishi chochote, hauwezi kuhimili mazao au kuwa na maji ya kukata kiu ya mifugo.

Soma pia: Nigeria yakopa mamilioni ili kusaidia kilimo wakati njaa ikinyemelea 

Kulingana na wataalamu hasara hii sio tu janga la mazingira lakini pia inawalazimisha mamilioni ya watu kutafuta hifadhi mahala pengine.

Katika eneo la kaskazini mwa Kenya, familia zinaacha vijiji vyao, nyumba zao zilizochakaa na mashamba yaliyogeuka kuwa viwanja vilivyokauka na kwenda kwenye kambi za muda au kwenye miji iliyojaa watu wengi.

Ukweli huu unadhihirika katika kaunti ya Marsabit nchini Kenya, ambako mwanasosholojia na mwanauchumi Julia Fuelscher ambaye pia ni mtaalamu wa kukabiliana na hali ya ukame na anayewasaidia watu walio hatarini zaidi amasema watu wanaondoka Kwenda kwenye kambi hizo za muda au wanahamia mijini kutafuta ahueni.

"Kwanza ni dhahiri kwamba watu wanahama hama kwa wingi, kwa mfano, kutoka Marsabit na Turkana (nchini Kenya) wanahama kwenda Nairobi. Wengine hata huondoka nchini na kwenda kwa mfano Riyadh, Saudi Arabia. Wakenya wengi kutoka mikoa hii wanakwenda Riyadh hasa kwa sababu wengi wao ni Waislamu kwa hivyo wanauona mji huo ni bora kwao lakini pia wanahamia katika nchi nyingine."

Wito wa kurejesha rutuba kwenye ardhi

Mkulima nchini NigerPicha: DW

Kuenea kwa jangwa kunatokana na aina ya uharibifu wa ardhi ambapo ardhi yenye rutuba inapoteza tija kubwa ya kibaolojia na kiuchumi, na ni mojawapo ya changamoto kuu ambazo zinalikabili eneo la kaskazini mwa Nigeria hasa katika majimbo ya Borno na Yobe, pamoja na maeneo yaliyoko kwenye mipaka kati ya Nigeria na Chad na Cameroon.

Mwanaharakati wa nchini Chad, Hindou Oumarou Ibrahim, amesema kupotea kwa maisha ya watu katika Bonde la Ziwa Chad kunasababishwa na matokeo mengi.

Soma pia: WFP imetangaza mpango wa kutumia teknolojia katika kilimo 

Katika baadhi ya matukio hayo ni mapambano ya kugombea rasilimali ambayo yanageuka na kuwa ghasia za kijamii, zinazotumiwa na makundi ya watu wenye silaha kuwasajili watu waliokata tamaa na kuwa wanachama wapya kwenye makundi yao.

Mkuu wa UNCCD Ibrahim Thiaw ametoa wito wa kuchukuliwa hatua mara moja na kuongezwa kwa uhamasishaji wa upatikanaji wa fedha kwa ajili ya kurejesha rutuba kwenye ardhi, uzalishaji wa kilimo, usalama wa chakula, na kupunguza harakati za uhamiaji na migogoro.

Amesema juhudi zinazolenga kurutubisha mamilioni ya hekta za ardhi iliyoharibiwa barani Afrika, zinaonyesha kuwa inawezekana kubadili miendendo ya kuharibu mazingira na hivyo kuwawezesha watu kubakia katika maeneo yao. Hata hivyo, miradi hii inahitaji ufadhili zaidi ambao upatikanaji wake bado unasuasua amesema mkuu huyo wa UNCCD.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW