1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Dunia yaadhimisha siku ya kwanza ya baiskeli

3 Juni 2018

Tarehe tatu Juni imeazimiwa na baraza kuu la Umoja wa Mataifa kuwa ni siku ya baisikeli duniani. Azimio husika lilipitishwa mnamo mwezi wa Aprili na nchi wanachama 193 za umoja huo

Dänemark Kopenhagen Stadteil Noerrebro
Picha: picture alliance/ecomedia/Robert B. Fishman

Baisikeli ni chombo cha usafiri ambacho ni rahisi kukitumia, ni chombo kinachouzwa kwa bei ambayo takriban kila mtu anaweza kumudu, ni kifaa cha uhakika na pamoja na yote hayo chombo cha usafiri unaozingatia ulinzi wa mazingira.

Baiskeli pia inatoa mchango katika juhudi za kuyafikia malengo ya milenia ya maendeleo endelevu. Matumizi ya baisikeli yanaimarisha elimu, yanajenga afya na pia ni kinga ya maradhi. Pamoja na sifa hizo, chombo hicho cha usafiri kinahimiza hali ya kuvumiliana, uelewano, heshima na pia kinachangia katika kuleta utangamano wa kijamii na mahusiano ya amani.

Juu ya manufaa ya baisikeli, kiongozi wa shirika la misaada la kimataifa, World  Bicycle Relief Dave Neiswander ameeleza kwamba usafiri ni msingi muhimu katika kuleta maendeleo, amesema watu kwenye sehemu za mashambani mara nyingi wanatembea kwa miguu ili kufika wanakokusudia.

Bwana Neiswander ameongeza kusema kwamba njia rahisi ya kutumia baisikeli inaleta faida nyingi. Watoto  wanawahi masomo shuleni kutokana na kutumia baiskeli na hata wakulima wanawezeshwa kuwa na njia bora ya kupeleka mazao yao kwenye masoko ili kuyauza.

Baiskeli ni chombo muhimu cha usafiriPicha: picture-alliance

Chombo cha usafiri kisichotiliwa maanani

Hata hivyo licha ya faida zote hizo watu mara nyingi hawaitilii maanani baiskeli kuwa kifaa cha kuleta maendeleo. Baada ya kupitisha siku ya baisikeli duniani, Umoja wa Mataifa unawataka wanachama waipe basikeli kipaumbele katika mikakati yao ya maendeleo sambamba na kuijumuisha katika maamuzi ya kisiasa na mipango ya kitaifa na kimataifa.

Mkurugenzi wa shirika la misaada la Bicycle Relief kanda ya Ulaya Kristina Jasiunaite amesema baisikeli inatoa mchango mkubwa katika juhudi za kuleta maendeleo. Bi Jasiunaite amesema baisikeli kwa kweli ni chombo cha kufanikisha malengo endelevu duniani. Lakini aghalabu huwekwa pembeni ya mipango ya miradi ya maendeleo.

Mkurugenzi huyo amesema siku ya baiskeli duniani itasaidia kuhamasisha mwamko wa kutambua umuhimu wa baisikeli kijamii na kiuchumi. Ameeleza kuwa siku ya baisikeli duniani pia itachangia katika kuonyesha umuhimu wa usafiri wa baiskeli kwa kuhakikisha kwamba hakuna anaeachwa nyuma au anaeshindwa  kwenda shule, hospitali au sokoni, ati  kwa sababu tu sehemu hizo ziko mbali kutoka kwake.

Shirika la misaada ya baiskeli la Bicycle Relief linautekeleza mpago wake wa shule kwa kugawa baiskeli kwa watoto wa shule hasa wale wanaoishi mbali na shule zao. Kutokana na mradi huo mahudhurio shuleni yameongezeka kwa asilimia 28 kwenye sehemu za mashambani katika nchi za kusini mwa jangwa la Sahara . Na ufanisi miongoni mwa watoto wa shule umeongezeka kwa asilimia 59.

Shirika hilo la misaada ya baiskeli pia linashirikiana na wakulima wadogo wadogo na wahudumu wa afya ili kuzitatua changamoto za usafiri kwenye sehemu za mashambani. Mpaka sasa shirika hilo la misaada limeshagawa baiskeli 400,000 na pia limeshatoa mafunzo ya uhandisi wa baiskeli kwa vijana 1900 barani Afrika. 

Mwandishi: Zainab Aziz/Pressemitteilung zum ersten Weltfahrradtag am 3. Juni.

Mhariri: Iddi Ssessanga