1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Dunia yailaumu Algeria kwa mzozo wa mateka

21 Januari 2013

Operesheni ya jeshi la Algeria dhidi ya wanamgambo wa Kiislamu waliowateka wafanyakazi wa mtambo wa gesi imemalizika, huku mateka kadhaa wakiripotiwa kufa na nchi za Magharibi zikikasirishwa na Algeria.

Mtambo ya gesi wa Amenas, kusini wa Algeria.
Mtambo ya gesi wa Amenas, kusini wa Algeria.Picha: picture alliance / dpa

Chanzo kimoja cha habari kutoka vyombo vya uslama vya Algeria kimeliambia shirika la habari la Reuters, kwamba miongoni mwa mateka hao 30 waliouawa katika operesheni hiyo, wawili ni raia wa Japan, wawili raia wa Uingereza, na mfaransa mmoja.

Mateka wanane raia wa Algeria pia walipoteza maisha yao. Uraia wa mateka wengine ulikuwa bado haujafahamika vizuri. Mhandisi kutoka Ireland ambaye amebahatika kunusurika, amesema alishuhudia jeshi la Algeria likiiunguza moto gari moja iliyopakia mateka.

Kamanda wa jeshi la Algeria alisema vikosi vyao vilifanya uvamizi saa 30 baada ya wanamgambo wa kiislamu kuwateka wafanyakazi na kuudhibiti mtambo wa gesi wa In Amenas, kwa sababu wanamgambo hao walikuwa wameomba muda huo kuwapeleka mateka hao nje ya nchi.

Nchi za magharibi ambazo raia wao walikuwa miongoni mwa mateka hazikuficha jinsi zilivyohangaishwa na usiri ilioufanya Algeria katika kuandaa operesheni hii, na pia matokeo yake mabaya. Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron ambaye aliahirisha hotuba muhimu kuhusu sera ya Umoja wa Ulaya ili kuushughulikia mgogoro huu, alisema operesheni hiyo ilifanya hali kuwa ya hatari kubwa.

''Vikosi vya Algeria sasa vimefanya uvamizi mahali wanaposhikiliwa mateka, na hali ni ya hatari kubwa na iliyojaa sintofahamu, na ninadhani tunapaswa kujiweka tayari kupokea habari zisizo njema'', alisema Cameron.

Japan yamuita balozi wa Algeria

Raia 14 wa Japan ni miongoni mwa watu ambao hadi leo Ijumaa walikuwa hawajulikani waliko, na Waziri Mkuu  Shinzo Abe ameahirisha safari yake katika nchi za kusini mashariki mwa Asia, hiyo ikiwa safari yake ya kwanza tangu kuchaguliwa kuchukua wadhifa huo, na alitegemewa kurudi nyumbani mapema ili kuushughulikia kwa karibu mgogoro huo. Serikali mjini Tokyo imemwita kwa mashauriano, balozi wa Algeria nchini humo.

Wanajeshi wa Mali kaskazini mwa nchi hiyo ambako kunapakana na Algeria.Picha: ISSOUF SANOGO/AFP/Getty Images

Marekani imesema haikuwa na taarifa zozote kuhusu raia wake waliochukuliwa mateka, ingawa ndege ya nchi hiyo isiyokuwa na rubani ilipita juu ya mahali pa tukio. Kama washirika wake wa Ulaya, Marekani pia imeunga mkono operesheni ya Ufaransa dhidi ya wanamgambo wa Kiislamu nchini Mali.

Ingawa kuingilia kijeshi kwa Ufaransa nchini Mali kunaonekana kama suluhu la tatizo la wanamgambo wa Kiislamu nchini Mali, ambao ni washirika wa kundi la al-Qaida, mkasa huu umeacha maswali mengi yasio na majibu, juu ya uwezo wa Algeria kuhakikisha usalama wa miundombinu muhimu ya nishati, na pia kuhusu uhusiano wake na nchi za magharibi.

Waziri wa Habari wa Algeria Mohammed Said alisema awali kwamba serikali ya nchi yake inakataa katakata kufanya mazungumzo na magaidi waliowachukua watu mateka.

Kundi la kiislamu linalojiita kikosi cha damu lilidai kuhusika na utekaji huo, kikiitaka Ufaransa kusitisha operesheni zake za kijeshi nchini Mali.

Mwandishi: Daniel Gakuba/RTRE
Mhariri: Yusuf Saumu

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi
Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW