1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Dunia yakumbuka mauaji dhidi ya Mayahudi

Mohammed Khelef16 Aprili 2015

Leo dunia inakumbuka miaka 70 tangu kukombolewa kwa Mayahudi kutoka kambi za mauaji ya maangamizi dhidi ya jamii ya Kiyahudi barani Ulaya, yaliyopewa jina la Holocaust.

Israel Holocaust Gedenktag
Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, akiweka shada la maua kwenye mnara wa Makumbusho ya Yad Vashem kwa ajili ya wahanga wa mauaji dhidi ya Mayahudi miaka 70 iliyopita.Picha: picture-alliance/dpa/A.B. Gershom

Ni mauaji haya yaliyopelekea baadaye kuundwa kwa taifa la Israel na hivyo kuigeuza kabisa historia ya ulimwengu kwa ujumla na hasa hasa ile ya Mashariki ya Kati.

Nchini Israel kwenyewe, watu walisimama kimya kwa muda wa dakika mbili, huku ving'ora vikilizwa nchi nzima kuwakumbuka wahanga wa mauaji hayo ya kikatili kabisa kuwahi kushuhudiwa duniani. Vituo vya redio na televisheni kote Israel vipindi na muziki wa maombolezo hayo.

Kumbukumbu hizi zilianza usiku wa Jumatano ambapo Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu aliitumia hotuba yake mbele ya maelfu ya watu waliokusanyika kwenye uwanja wa Makumbusho ya Yad Vashem mjini Jerusalem, kuyatupia lawama mataifa ya Magharibi, kwa kudharau khofu iliyonayo Israel dhidi ya uwezekano wa Iran kumiliki silaha za kinyuklia

"Makubaliano mabaya yanayoundwa pamoja na Iran yanaonesha kwamba dunia haikujifunza na tukio hili la kihistoria. Mataifa ya Magharibi yamepinda magoti mbele ya vitendo vya uchokozi vya Iran."

Mataifa sita makubwa duniani - Marekani, Ujerumani, Ufaransa, Uingereza, Urusi, na China - yalifikia makubaliano na Iran juu ya programu hiyo mwezi uliopita. Baadhi ya mataifa hayo yalishuhudia mauaji makubwa ya Mayahudi wakati wa utawala wa Kinazi miaka 70 iliyopita.

Netanyahu hana imani na makubaliano

Huku dunia nzima ikionekana kuungana kwenye kuunga mkono juhudi za kufikiwa suluhisho na Iran, Israel inajikuta ikiwa peke yake. Mapema mwezi huu, Rais Barack Obama wa Marekani alionesha mara kadhaa kwenye hotuba yake kwamba Marekani inasimama bega kwa bega na Isarel juu ya suala la usalama na kwamba hatoruhusu chochote kuuyumbisha usalama huo.

Wanajeshi wa Israel wakisimama kwa heshima mbele ya Kumbukumbu ya Yad Mordechay kuadhimisha vita kati ya nchi yao na Misri, wakati huu wa kumbukumbu ya mauaji ya Holocaust.Picha: AFP/Getty Images/J. Guez

Hata hivyo, Netanyahu anaonekana kutoridhika na hakikisho hilo na ametumia pia hotuba yake ya leo kuifananisha Iran na utawala wa wa Kinazi katika kile kinachoonekana kuendeleza shinikizo lake dhidi ya makubaliano hayo ya nyuklia.

"Kama ambavyo Manazi walijaribu kuuharibu ustaarabu na kuwa na utawala wa "Kabila Kuu" huku wakiwafyeka Mayahudi, ndivyo Iran inavyojaribu kulitawala eneo hili na kutoka hapo kuendelea mbele zaidi kutekeleza lengo ililolitangaza la kulimwagia hewa ya sumu taifa la Mayahudi," alisema Waziri Mkuu huyo wa Israel.

Wakati ambapo dunia inakumbuka miaka hiyo 70 ya mauaji ya Mayahudi wapatao milioni sita, utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha Tel Aviv nchini Israel unaonesha kuwa mashambulizi yanayohusishwa na chuki dhidi ya jamii hiyo yaliongezeka kwa asilimia 38 duniani mwaka 2014, ukiwa ni wa pili kuwa na mashambulizi kama hayo tangu mwaka 2009.

Kwa mujibu wa utafiti huo, mashambulizi au vitish vingi dhidi ya watu au taasisi za Kiyahudi yalitokea nchini Ufaransa ambako mwaka 2014 kulikuwa na matukio 164. Ufaransa ndio nchi ya Ulaya yenye idadi kubwa ya Mayahudi, ambao wanakisiwa kufikia 600,000.

Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters/AFP
Mhariri: Saumu Yussuf