Dunia yalaani kuawa kwa jenerali wa jeshi Lebanon
12 Desemba 2007CAIRO.Nchi kadhaa zimelaani shambulizi la Bomu hii leo huko Lebanon lililomua afisa wa juu katika jeshi la nchi hiyo Brigadier General Francois el Hajj.
Umoja wa nchi za kiarabu umelaani vikali shambulizi hilo na kuelezea matumani yake kuwa halitazikwaza zaidi juhudi za kumchagua rais mpya.
Katibu Mkuu wa jumuiya hiyo Amri Mussa amesema kuwa pamoja na shambulizi hilo lakini umoja huo una matumaini kuwa uchaguzi utafanyika haraka.
Brigadier Francois el Hajj ambaye alikuwa ni mkuu wa kitengo cha harakati katika jeshi, ni miongoni mwa watu waliyokuwa wakitegemewa kumrithi Generali Michel Suleiman nafasi ya ukuu wa majeshi iwapo Generali Suleiman atachaguliwa kuwa rais.
Mjini Brussels, Umoja wa Ulaya umesema kuwa utaendelea kuiunga mkono serikali ya Lebanon pamoja na kutokea kwa shambulizi hilo.
Mkuu wa siasa za nje wa Umoja huo, Javier Solana amesema kuwa inasikitisha kuona kuwa shambulio hilo limekuja mnamo wakati ambapo vyama vinaayopingana viko katika mjadala kufikia muafaka.
Shambilizi hilo limetokea baada ya hapo jana bunge kuahirisha kwa mara ya nane kupiga kura ya kumchagua rais hali inayoashiria mvutano mkali miongoni mwa wanasiasa.
Naye Waziri wa Nje wa Ufaransa Bernard Kouchner amesema kuwa shambulizi hilo lilikuwa na nia ya kuzidisha hali tete nchini humo, na kusema kuwa njia pekee ya kulipiza ni kumchagua rais haraka iwezekanavyo.
Nchini Syria nchi hiyo, imelilaani shambulizi hilo na kusema Israel na mawakala wake wa ndani ya Lebanon wanahusika.
Hato hivyo mpaka sasa hakuna kikundi chochote kilichodai kuhusika na shambulizi hilo.