Dunia yalaani shambulizi la Israel dhidi ya Wapalestina Gaza
1 Machi 2024Rais huyo wa Ufaransa alisema kile kilichomsikitisha ni kuona namna raia walivyolengwa na wanajeshi wa Israel.
Macron alilaani tukio hilo akitoa wito wa kuwepo ukweli, haki na kuheshimiwa sheria ya kimataifa, huku akisema ni muhimu kwa makubaliano ya kusitisha mapigano kufikiwa haraka.
Akizungumza katika redio moja ya Ufaransa, Waziri wa Mambo ya Nje wa taifa hilo, Stephane Sejourné, alisema nchi yake iko tayari kuunga mkono wito wa Umoja wa Mataifa wa kufanya uchunguzi huru wa tukio hilo la siku ya Alhamis (Februari 29).
Kulingana na wizara ya afya inayoendeshwa na Hamas mjini Gaza, wanajeshi wa Israel waliwafyatulia risasi Wapalestina waliokuwa wakipokea msaada wa chakula na kusababisha vifo vya watu 112 na wengine zaidi ya 750 kujeruhiwa.
Watu 104 wauwawa katika operesheni ya kutoa msaada Gaza
Rais Joe Biden wa Marekani alisema tukio hilo lingelitatiza hatua za kufikiwa makubaliano ya kusitisha mapigano katika mzozo huo wa takribani miezi mitano.
Msemaji wa serikali yake, Mathew Miller, alisema bado Marekani ilikuwa inachunguza kujua ni kipi hasa kilichotokea.
Uturuki yasema Israel imefanya uhalifu mwengine dhidi ya ubinaadamu
Uturuki nayo iliishutumu Israel kwa kufanya uhalifu mwingine dhidi ya ubinaadamu kwa kuwalenga kwa makusudi Wapalestina wasio kuwa na hatia kwa lengo la kuwaangamiza.
Kupitia kwa msemaji wake, Stephan Dujarric, Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres pia aliyalaani mauaji hayo akisisitiza kuwa watu wa Gaza wanahitaji msaada wa haraka, wakiwemo wale walio upande uliozingirwa wa kaskazini, ambako Umoja huo bado haujafanikiwa kupeleka misaada ya kibinaadamu.
Umoja wa Ulaya, China, Qatar, Saudi Arabia, Austaralia na mataifa mengine yalilaani tukio hilo na kusema ni uonevu kwa watu wa Palestina, huku wakitoa mwito wa makubaliano ya kusitisha mapigano kufikiwa haraka ili kuwalinda watu wa Gaza wanaoendelea kuteseka.
Haniyeh: Tuko tayari kwa mazungumzo, lakini pia kuendeleza mapigano
Kolombia yatangaza kusitisha kununua silaha Israel
Rais Gustavo Petro wa Kolombia aliishutumu Israel kufanya mauaji ya halaiki mjini Gaza na kutangaza kusimamisha kwa muda ununuzi wa silaha za Israel.
Israel ni moja ya mataifa yanayouza silaha zake kwa taifa hilo la Amerika ya Kusini, ambazo hutumika katika mapambano yake ya muda mrefu na wanamgambo pamoja na magenge ya wahalifu wanaoendesha biashara ya madawa ya kulevya.
Rais Petro alisema ni lazima dunia ikomeshe matendo ya Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, dhidi ya Wapalestina.
Israel yakanusha kuhusika na mauaji
Lakini Israel ilikanusha kuhusika na kutoa lawama ya moja kwa moja kwa umati wa watu uliokuwa unapokea msaada huo.
Badala yake, Israel ilisema waathiriwa waliuawa katika mkanyagano na msukumano, wakati walipoyazingira malori 38 ya msaada.
Jeshi la nchi hiyo lilikwenda mbali zaidi kwa kusema huenda madereva wa malori hayo waliwakanyaga Wapalestina waliokuwa wanasubiri msaada huo.
Licha ya tamko hilo, mmoja ya maafisa wa Israel baadaye alikiri kuwa wanajeshi wao waliwamiminia risasi Wapalestina kwa sababu walidhani ni kitisho kwa usalama wao.
Wapalestina zaidi ya 30,000 wameshauwawa tangu vita hivyo vianze mnamo Oktoba 7, wengi wao wakiwa wanawake na watoto.
AP/AFP/Reuters