1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Dunia yaomboleza kifo cha Rais wa Poland

Kabogo Grace Patricia10 Aprili 2010

Rais Kaczynski amefikwa na mauti baada ya ndege yake kuanguka karibu na uwanja wa ndege wa Smolensk, Urusi.

Rais Lech Kaczynski wa Poland aliyefikwa na mauti leo kwa ajali ya ndege.Picha: AP

Viongozi mbalimbali duniani wameelezea kushtushwa na kifo cha Rais wa Poland, Lech Kaczynski, kilichotokea leo katika ajali ya ndege. Viongozi hao ni pamoja na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, Rais Barack Obama wa Marekani na Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel.

Viongozi wengine ni Malkia Elizabeth wa Pili wa Uingereza na Waziri Mkuu, Gordon Brown. Salamu za rambi rambi zinaendelea kutolewa kutokana na kifo hicho. Miongoni mwa salamu hizo ni zile kutoka kwa viongozi wa Umoja wa Ulaya, Waziri Mkuu wa Urusi, Vladmir Putin, na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu.

Rais Lech Kaczynski wa Poland akiwa na mkewe, Maria Kaczynski, ambaye pia amekufa katika ajali hiyo.Picha: AP

Rais huyo wa Poland alifikwa na mauti baada ya ndege yake kuanguka karibu na uwanja wa ndege wa Smolensk, Urusi. Abiria wengine waliokufa katika ajali hiyo ni mke wa rais huyo, Maria, Naibu Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje, Andrzej Kremer, Mkuu wa majeshi ya Poland, Franciszek Gagor, Gavana wa Benki Kuu ya nchi hiyo, Slawomir Skrzypek, wabunge na wanahistoria kadhaa.

Rais huyo wa Poland pamoja na ujumbe wake walikuwa wakielekea katika mji wa Katyn karibu na Smolensk kuhudhuria kumbukumbu ya mauaji ya wafungwa wa vita wa Urusi na Poland waliouawa wakati wa utawala wa kisovieti. Kufuatia kifo hicho, Spika wa bunge la Poland, Bronislaw Komorowski, anachukua madaraka ya nchi hiyo.

Mwandishi:Grace Patricia Kabogo(AFPE/RTRE/BBC/DPAE)

Mhariri:Othman Miraji