1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Dunia yazungumzia ushindi wa Merkel

25 Septemba 2017

Rais Emannuel Macron wa Ufaransa ameungana na viongozi wengine duniani kumpongeza Kansela Angela Merkel wa Ujerumani kwa ushindi, lakini nako kuingia bungeni kwa chama cha siasa kali cha AfD kukisifiwa kwa kiasi kikubwa.

USA Präsident Macron vor der UN-Vollversammlung
Picha: Reuters/E. Munoz

Viongozi wa dunia, akiwamo Rais Macron wameupongeza ushindi wa Kansela Merkel katika uchaguzi wa jana Jumapili (Septemba 24), huku wakitoa ahadi ya kuimarisha mahusiano ya msingi yaliyopo.

Jana usiku, Macron aliongoza kwa kutuma salamu za pongezi kwa ushindi wa Kansela Merkel baada ya kushinda awamu ya nne ya ukansela. "Nilimpigia simu Angela Merkel kumpongeza. Tutaendeleza mashirikiano yetu kwa kuangazia zaidi mafanikio ya umoja huo na nchi zetu", Macron aliandika kwenye ukurasa wa Twitter.

Waziri Mkuu wa Uhispania, Mariano Rajoy, alisema kuchaguliwa tena kwa Merkel kutawezesha kuimarishwa zaidi kwa Umoja wa Ulaya.

Katika ujumbe wake, Rajoy alimpongeza Merkel kwa matokeo hayo mazuri baada ya chama chake cha Christian Democratic Union (CDU) na chama ndugu chenye makao yake jimboni Bavaria, cha Christian Social Union (CSU) kwa ushindi wa asilimia 33 ya kura.

Aidha, Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, naye alituma ujumbe kama huo, akimuelezea Merkel kama "rafiki wa kweli wa Israel"

Waziri mkuu wa Hispania, Mariano Rajoy, asema ushindi huo ni alam njema kwa uimara wa umoja wa Ulaya Picha: Getty Images/AFP/J. Soriano

AfD yapongezwa

Mjini Brussel, makao makuu ya Umoja wa Ulaya, mwanadiplomasia wa kwanza kutoa maoni yake kuhusu ushindi wa Merkel alikuwa ni Pierre Moscovici, ambaye ni kamishna wa uchumi na mahusiano ya kifedha, aliyengazia zaidi kuanza vyema kwa chama cha Mbadala kwa Ujerumani (AfD) kinachofuata siasa kali za  mrengo wa kulia. Chama hicho kimepata asilimia 13 ya kura, na kwa mara ya kwanza kitaingia bungeni kikiwa na viti 94.

"Kuingia kwa AfD kwenye bunge la Ujerumani ni jambo la kushtukiza na linazua wasiwasi ndani ya jamii", aliandika Moscovici kwenye ukurasa wake wa Twitter. Lakini aliongeza kuwa "Ujerumani ya baada ya vita ya pili bado ni imara".

Viongozi wa Ulaya kutoka vyama vya sera kali za mrengo wa kulia walikuwa mstari wa mbele kukipongeza chama hicho mshirika cha Ujerumani. "Hongera kwa mshirika wetu AfD kwa ushindi huu wa kihistoria. Ni alama mpya ya mwamko wa jamii ya watu wa Ulaya" aliandika kiongozi wa chama cha French National Front, Marine Le Pen.

Kiongozi wa chama cha French National Front cha Ufaransa, Marine Le Pen, akipongeza chama cha AfD Picha: Getty Images/AFP/F. Lo Presti

Waangalizi wa sera za nje nchini Marekani, wanasema ingawa matokeo haya ya kihistoria kwa chama cha AfD, ambacho ni cha kwanza cha sera kali za mrengo wa kulia kuchaguliwa kwenye bunge la Ujerumani kwa zaidi ya nusu karne, ni jambo linalotakiwa kuchukuliwa kwa uzito mkubwa, kwa kuwa pia linaakisi kwa mapana masuala ya kimataifa.

"Ingawa hatujui ugumu wa kuundwa kwa serikali ya muungano itakayofuata, sitarajii kama kutakuwa na mabadiliko makubwa kwenye sera za nje za Ujerumani," amesema Charles Kupchan, aliyehudumu kama mshauri mkuu wa Barack Obama kuhusu Ulaya na sasa akiwa ni mjumbe mwandamizi wa masuala ya mahusiano ya nje kwenye Halmashauri ya Umoja ya Ulaya. 

Aliyekuwa mshauri wa masuala ya mahusiano ya nje wakati wa kampeni za Rais wa Marekani, Donald Trump, James Cafarano, amesema haoni kama hatua hii inaweza kuwa na athari yoyote kwenye mashirikiano kati ya Ujerumani na Marekani.

Bila ya kukipongeza moja kwa moja chama cha AfD, kiongozi wa chama cha sera kali za mrengo wa kulia nchini Uholanzi, Geert Wilders, aliangazia umaarufu wa kila chama kikuu barani Ulaya kinachopinga wahamiaji, mara tu baada ya kutoka kwa matokeo ya uchaguzi. 

Akizungumzia namna AfD kilivyotarajiwa kuwa chama cha tatu kwa ukubwa nchini Ujerumani pamoja na chama chake cha Dutch Party of Freedom, ambacho kiliwekwa cha pili katika uchaguzi wa Uholanzi mwezi Aprili, aliandika kwenye ukurasa wake wa Twitter "ujumbe uko wazi. Sisi sio mataifa ya Kiislamu".

Mwandishi: Lilian Mtono/DW English
Mhariri: Yusuf Saumu

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW