Duru mpya ya mazungumzo ya Libya yaanza Tunisia
27 Septemba 2017Duru mpya ya mazungumzo yanayodhaminiwa na Umoja wa Mataifa yaliyonuiwa kuunganisha pande mbili zinazohasimiana nchini Libya yameanza nchini Tunisia. Mkutano huo ulifunguliwa na mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kwa Libya Ghassan Salame
Viongozi wa pande mbili hasimu hivi karibuni walikubaliana kushirikiana pamoja kuinasua Libya kutoka katika machafuko yanayotishia usalama wa kanda nzima na Ulaya kwa Ujumla. Lengo la mwisho ni kubwa: Mazungumzo ya kitaifa na vyama vyote vya kisiasa nchini Libya, kupatikana kwa katiba mpya na kufanyika uchaguzi wa urais.
Marekebisho ya makubaliano yaliyofanywa Morocco
Lakini kitu cha kwanza kabisa kinacholengwa katika mazungumzo hayo ni kuwepo marekebisho katika makubaliano ya amani yaliyofikiwa mjini Skhirat Morocco mwaka 2015. Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Libya Ghassan Salame, amesema hapana shaka uhalali wa makubaliano hayo ya amani utaimarishwa na kuungwa mkono miongoni mwa walibya.
Salame ameongeza kuwa uchaguzi wa bunge na ule wa rais unapaswa kufanyika ndani ya mwaka mmoja huku akiongeza kuwa anatumai yatafanyika na kumalizika katika wiki chache zijazo ili kutoa nafasi ya mazungumzo ya kitaifa miezi kadhaa ijayo yatakayowaleta pamoja pande mbili hasimu.
Salame amesema kanuni ya uchaguzi itaandaliwa katika kipindi cha machipuko huku uchaguzi ukitarajiwa kufuatia ndani ya mwaka mmoja. "Sheria ya uchaguzi ni muhimu kwa sababu Libya haijawahi kuandaa uchaguzi unaojumuisha makundi mengi” aliongeza Salame akiwa mjini Tunis ambako mkutano wa kwanza kati ya wawakilishi wa bunge lililo Mashariki mwa Libya na wawakilishi wa serikali iliyoko mjini Tripoli unapofanyika.
Kuondoa ushindani na kuimarisha taasisi
Mazungumzo hayo ya amani yaliyoanza hapo jana siku ya Jumanne, yamefungua njia ya hatua ya kwanza ya mazungumzo yanayoongozwa na Ghassan Salame ambaye alisema kwa sasa wanazungumzia juu ya masuala muhimu na sio majina kwa maana ya kwamba wanakusudia kuondoa ushindani na kuleta taasisi thabiti.
Aidha viongozi hasimu nchini humo tukianzia na upande wa Serikali ya Tripoli Fayez Serraj na Khalifa Haftar wa upande wa bunge lililoko upande wa mashariki walikutana mjini Paris mwezi Julai na kukubaliana kuandaa uchaguzi wa bunge haraka iwezekanavyo lakini hawakutoa taarifa zaidi juu ya tarehe ya uchaguzi huo. Siku ya Jumanne Haftar alikaribishwa mjini Roma ambako alikutana na Waziri wa Ulinzi wa Italia Roberta Pinotti na jenerali Claudio Graziano, hii ilionekana kuwa hatua nzuri ya kidiplomasia kwa Italia ambayo Libya ilikuwa ni himaya yake wakati wa kipindi cha ukoloni.
Libya iliingia katika machafuko kufuatia maandamano ya kutaka mageuzi mwaka 2011 yaliyosababisha mauaji ya kiongozi wake Moammar Gadhafi.
Mwandishi:Amina Abubakar/AP/dpa
Mhariri: Josephat Charo