1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUrusi

Duru nchini Urusi zasema kiongozi wa Wagner amekufa

24 Agosti 2023

Duru nchini Urusi zinasema kiongozi wa Kundi la Mamluki wa Kirusi la Wagner, Yevgeny Prigozhin, amefariki dunia baada ya ndege inayoaminika alikuwemo kuanguka na kuteketea kwa moto hapo jana jioni.

Russland | Jewgeni Prigoschin | mutmaßliches Flugzeugunglück in der Region Twer
Mabaki ya ndege inayoaminika Mkuu wa Kundi la Wagner, Yevgeny Prigozhin alikuwemo Picha: Investigative Committee of Russia/Handout/REUTERS

Ukurasa wa mtandao wa Telegram wenye jina la Grey Zone, ambao una mafungamano na Kundi la Mamluki la Wagner, umeripoti kuwa Prigozhin amekufa.

Ujumbe kwenye ukurasa huo umemtaja kuwa shujaa na mzalendo ambaye amepoteza maisha chini ya kile mtandao huo umesema kuwa mikono ya watu wasiojulikana iliyowatambulisha kuwa "wasaliti wa Urusi".

Mbali ya ripoti za ukurasa huo, mamlaka za Urusi zilichapisha orodha ya watu waliopoteza maisha katika ajali ya ndege iliyotokea jana jioni likiwemo jina la Yevgeny Prigozhin.

Orodha hiyo ilitolewa na Wakala wa Usafiri wa Anga nchini Urusi, Rosaviatsia, ikijumuisha majina ya watu 10 ambayo mbali ya Prigozhin limo pia jina la Dmitry Utkin --mtu wa karibu sana na kiongozi huyo wa Wagner-- aliyemsaidia kuliunda na hata kulipatia jina.

Chombo hicho, kilichokuwa kinasafiri kutoka mji mkuu wa Urusi, Moscow, kwenda mji mwingine mkubwa nchini humo wa St-Petersburg, kilianguka karibu na kijiji cha Kuzhenkino kilichopo kwenye mkoa wa Tver. Hayo yameelezwa na Wizara ya Huduma za Dharura nchini Urusi.

Wapelelezi nchini Urusi wamesema wamefungua uchunguzi wa jinai kubaini sababu ya kuanguka kwa ndege hiyo binafsi inayoaminika ilimbeba Prigozhin.

Baadhi ya vyanzo ambavyo havikutajwa majina vimeviambia vyombo vya habari vya Urusi kuwa vinaamini ndege hiyo iliangushwa na kombora la mifumo ya ulinzi.

Ikulu ya Kremlin ipo kimya kuhusu taarifa za kifo cha Prigozhin

Hakuna taarifa yoyote iliyotolewa na ikulu ya Urusi, Kremlin, wala Wizara ya Ulinzi ya nchi hiyo kuhusiana na kifo cha Prigozhin.

Uasi wa kundi la Wagner wa Juni, 23 na 24, 2023 ulizusha hamkani nchini Urusi Picha: Erik Romanenko/TASS/dpa/picture alliance

Kiongozi wa kundi la Wagner alijitangaza kuwa adui wa watawala wa jeshi la Urusi kutokana na yeye mwenyewe kuwatuhumu kwa  uwezo mdogo wa kuendesha vita vya Urusi nchini Ukraine.

Kufuatia kutokuwepo za uhakika kuhusu kifo cha kiongozi huyo wa Wagner, wafuasi wake wameinyooshea kidole serikali ya Urusi na wengine wameitupia lawama Ukraine, ambayo leo inaadhimisha siku yake ya uhuru.

Katika jengo la ofisi za kundi la Wagner mjini St Petersburg, taa ziliwshwa katika umbo lenye kuonesha alama ya msalaba ambayo imetafsiriwa na wengi kuwa ishara ya kuomboleza na kutoa heshima kwa Prigozhin.

Prigozhin mwenye umri wa miaka 62 aligonga vichwa vya habari duniani baada ya kuongoza uasi uliodumu kwa muda mfupi dhidi ya mamlaka za Urusi mnamo Juni 23 hadi 24.

Wapiganaji wa Wagner walizidungua helkopta za mashambulizi za Urusi na kuwauwa marubani wasio na idadi huku wakisonga mbele kuelekea mji mkuu Moscow.

Jeshi la Urusi lilighadhibishwa na kitendo hicho ambacho rais Vladimir Putin alikitaha kuwa "usaliti" uliotishia kuitumbukuza Urusi kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Prihozhin alifanya uasi huo baada ya miezi kadhaa ya kulikosoa waziwazi Jeshi la Urusi kwa jinsi linavyoendesha vita nchini Ukraine na alijaribu mara kadhaa kushinikiza Waziri wa Ulinzi wa nchi hiyo Sergei Shoigu na Mkuu wa Majeshi waondolewa mamlakani.

Uasi huo wa Wagner ulisitishwa kufuatia makubaliano yaliyoshuhudia Prigozhin akiridhia kuihama Urusi na kwenye taifa jirani la Belarus. Hata hivyo tangu wakati huo alikuwa na ruhusa ya kufanya safari bila kizuizi ndani ya Urusi.

Biden asema hajashangazwa na taarifa zinazoashiria kifo cha Prigozhin

Yevgeny PrigozhinPicha: PMC Wagner/Telegram/REUTERS

Tangu kusambaa taarifa za ajali hiyo na uwezekano wa kuwa Prigozhin ni miongoni mwa waliopoteza maisha, maoni yanamiminika kutoka kila pembe ya dunia kuhusu kile kilichotokea.

Rais Joe Biden wa Marekani alipoulizwa na waandishi habari kuhusu mkasa huo, alijibu hana taarifa za kutosha lakini hakuna kilichomshangaza akisema karibu kila kinachotokea nchini Urusi bila ya kuwa na mkono wa rais Vladimir Putin.

Abbas Gallyamov, mwandishi wa zamani wa hotuba za rais Putin ambaye sasa ni mkosoaji wa utawala wake, amesema kiongozi huyo wa Urusi anahusika na ajali hiyo ya ndege na kilichotokea kimeimarisha nafasi yake ya mamlaka kuelekea uchaguzi wa mwaka ujao ambao Putin anatarajiwa atawania muhula mwingine.

Mkosoaji mwingine wa ikulu ya Kremlin na mfanyabiashara mwenye miaka chungunzima ya uzoefu wa siasa za Urusi, Bill Browder, anakubaliana na mtizamo wa kuwa Putin anayo dhima kwenye ajali inayoaminika imemuua kiongozu wa kundi la Wagner.

Amesema "Putin kamwe huwa hasamehi wala kusahau na kitendo cha uasi kilichofanywa na mkuu wa kundi la Wagner kilimfedhehesha na isingekuwa rahisi akubali kumwacha Prigozhin akitamba duniani bila kuchukuliwa hatua"

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW