Duru ya kwanza ya uchaguzi wa bunge la Ufaransa
11 Juni 2012Francois Hollande,msoshialisti mpenda mageuzi aliyechaguliwa kuwa rais May sita iliyopita,anapewa nafasi nzuri ya kujipatia wingi mkubwa na madhubuti wa viti katika bunge la nchi hiyo,kama alivyoshauri kama uchaguzi huo kuitishwa.
Mkuu wa chama cha kisoshialisti-PS,Martine Aubry anasema:
"Nafikiri jana wafaransa wametaka kudhihirisha imani yao kwa Francois Hollande ili aendelee na mageuzi aliyoahidi.Wametaka kumpa uwezo wa kutekeleza aliyoahidi."
Amesema mwenyekiti wa chama cha kisoshiliasti na kuwasihi wapiga kura wa mrengo wa shoto wasichoke mpaka watakapokamilisha ndoto yao,na kupata wingi mkubwa wa viti,duru ya pili ya uchaguzi itakapoitishwa jumapili ijayo.
Wasoshialisti wanawatia kishindo wa hafidhina pia ambao katika baadhi ya maeneo,wanaweza kuamua kushirikiana na wafuasi wa siasa kali ya mrengo wa kulia katika duru ya pili ya uchaguzi.
Kwa mujibu wa makadirio ya watafiti wa maoni ya umma,wasoshialisti wanaweza kujipatia kati ya viti 283 na 329 jumapili ijayo toka jumla ya viti 577 vya bunge.Kwa namna hiyo,wanaweza peke yao kudhibiti wingi mkubwa wa viti bila ya hata kuwategemea washirika wao serikalini,walinzi wa mazingira (wanaotazamiwa kujikingia viti kuanzia 10 hadi 15),seuze wafuasi wa siasa kali za mrengo wa shoto.
Wahafidhina kwa upande wao,ingawa hawakupoteza sana,lakini ushindani wa chama cha siasa kali ya mrengo wa kulia-FN unawapokonya fursa ya kuweza kujikusanyia viti zaidi duru ya pili ya uchaguzi itakapoitishwa.
Chama cha kihafidhina cha UMP na washirika wake wamejipatia asili mia 34 ya kura dhidi ya asili mia 35 walizopata wasoshialisti na asili mia 5 za walinzi wa mazingira.UMP wanaweza kujikingia viti kati ya210 na 263 katika bunge lijalo.
UMP wanakabiliana na ushindani mkali kutoka chama cha siasa kali ya mrengo wa kulia cha FN kilichojipatia asili mia 13.6 ya kura na huenda kikatuma wagombea 61 katika duru ya pili -kushindana ama na mgombea wa kisoshialisti au wa kihafidhina .
"Hatutoshirikiana na FN,lakini tushikirikiane na nani-mgombea wa mrengo wa shoto-hakuna uhakika?amesema kwa upande wake mkuu wa chama cha kihafidhina cha UMP,Jean Francois Copé.
Wasoshialisti wameamua kumtoa mgombea wao katika mkoa wa kusini wa Vaucluse, ambako wanakamata nafasi ya tatu ili kurahisisha ushindi wa chama cha kihafidhina dhidi ya Marion-Maréchal Le Pen,mjukuu wa muasisi wa chama cha asiasa kali ya mrengo wa kulia nchini Ufaransa Jean Marie Le Pen.
Mwenyekiti wa chama hicho,binti yake,Mari´ne Le Pen amezusha maajabu kwa kuongoza matokeo ya duru ya kwanza katika eneo lake-atashindana na msoshiliasti katika duru ya pili ya uchaguzi jumapili ijayo.
FN wanaweza kuwakilishwa katika bunge la Ufaransa,kwa mara ya kwanza safari hii baada ya kupita miaka 24.
Wadadisi wanakubaliana Francois Hollande atajipatia nafasi ya kutekeleza atakavyo mageuzi aliyokusudia katika wakati ambapo Ufaransa sawa na kanda ya Euro zinakodolewa macho na masoko ya hisa na baadhi ya mapendekezo yake kuhusu umri wa kustaafu au namna ya kuinua uchumi, yanaangaliwa kwa jicho la wasi wasi na washirika wake barani Ulaya.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP
Mhariri Yusuf Saumu