DW Idhaa ya uhakika
1 Februari 2013 Watangazaji mahiri, na uongozi makini
Hapa nitawakariri, kwa majina na ubini
Ute Schaeffer ni ngangari, ni kiranja namba wani
Ni mhariri mkuu, bora asiye mithili
Wa pili katika chati, mzoefu mwenye shani
Ni Andrea Schmidti, mchezo hana kazini
Kavishinda vizingiti, kwa elimu ya kichwani
Mkuu wa matangazo, hayupo yake mithili
Sekioni wa Kitojo, kumsikiza sichoki
Huwa hapendi porojo, habari huzihakiki
Mambo hayendi 'rijojo, aishikapo maiki
Huyu ni mtangazaji, bingwa asiye mfano
Mkongwe Umulkheri, napenda yake machejo
Anasoma tahariri, kwa dhati wala si fujo
Amejawa tafakuri, katika kila utajo
Huyu ni mtangazaji, bingwa asiye mfano
Abdul Mtulia, mtangazaji wa shoka
Tangu zama katulia, Deutsche Welle hajatoka
Uandishi aujua, kazini hana dhihaka
Huyu ni mtangazaji, bingwaasiye mfano
Amina Abubakari, kweli hana mpinzani
Kila mtu anakiri, anayo nyingi thamani
Amejaa kwelikweli, mezani Ujerumani
Huyu ni mtangazaji, bingwaasiye mfano
Mohammed Dahmani, ni mtu wa sawasawa
Alitangaza zamani, hata mimi sijazawa
Wengi wanaotamani, kama yeye kuja kuwa
Huyu ni mtangazaji, bingwa asiye mfano
Stumai binti Joji, fani ameanza juzi
Sana ananifariji, anavyoimudu kazi
Wale wasomtaraji, 'mebaki midomo wazi
Huyu ni mtangazaji, bingwa asiye mfano
Sudi mwana wa Mnete, mtangazaji mahiri
Chanda chema yake pete, tena iuzwayo ghali
Anatamba siku zote, kwa kutupasha habari
Huyu ni mtangazaji, bingwa asiye mfano
Caro mwana wa Tsuma, sitaacha kumtaja
Japo si sana husema, achapa kazi ya haja
Sababu ya kujituma, idhaa ipate tija
Dada huyu ni mtaji, bingwa asiye mfano
Othmani wa Miraji, mambo yake taratibu
Napenda anavyohoji, na mambo kuyaratibu
Kwa maswali kama jaji, kwa nyingi zake lakabu
Japo tunakuhitaji, umetuaga jamani!
Iddi mwana wa Sesanga, habarizo zina radha
Watupa vingi visanga, habari kadha wa kadha
Mtima unatukonga, tuna raha si bughudha
Huyu ni mtangazaji, bingwa asiye mfano
Salma binti Saidi, sauti yake murua
Atangaza kwa ustadi, Unguja wanamjua
Lafudhi yake ya jadi, na sauti ya kutua
Huyu ni mtangazaji, bingwa asiye mfano
Khatibu bin Mjaja, redioni unavuma
Kwa shangwe ninakutaja, songa usirudi nyuma
Nyingi watupa faraja, habari unavyosoma
Huyu ni mtangazaji, bingwa asiye mfano
Syilivia Muehozi, watangaza toka Bonni
Kukusahau siwezi, hakika wewe ni mboni
Unao mwingi ujuzi, katika hii midani
Huyu ni mtangazaji, nguri asiye mfano
Mohammed Khelefu, watangaza kwa hisia
Wengi unawasadifu, twapenda kukusikia
Habarizo hazikifu, vizuri wasimulia
Huyu ni mtangazaji, bingwa asiye mfano
Abubakari Liongo, aripoti Tanzania
Hakika hana kinyongo, habari kutupashia
Katika huu uringo, hana wa kumfikia
Mkongwe mtangazaji, nguri asiye mfano
Saumu biti Mwasimba, redioni anatamba
Sauti yake nyembamba, utadhani anaimba
Hizi kamwe sio kamba, habari anazipamba
Huyu ni mtangazaji, bingwa asiye mfano
Erick mwana Mponda, anaripoti ya Kenya
Kitu ninachompenda, kila kona anapenya
Eldoret huenda, na Mombasa hukusanya
Huyu ni mtangazaji, bingwa asiye mfano
Leila mwana wa Ndinda, vyema anawakilisha
Kampala ni Uganda, habari anatupasha
Kizungumza 'tapenda, abadan kutuchosha
Huyu ni muwakilishi, bingwa asiye mfano
Swalehe Mwanamilongo, mtu asiye makuu
Aripoti toka Kongo, hata maziwa makuu
Ni mpenzi wa bolingo, hata hufanya nukuu
Huyu ni mtangazaji, bingwa asiye mfano
Silivanu Karemera, sauti yake ni kali
Kulokuwa ukabila, sasa kuna serikali
Sasa watu wanakula, anaripoti Kigali
Huyu ni mtangazaji, bingwa asiye mfano
Daniel wa Gakuba, na Samia Othumani
Hamwezi sahaulika, Pendo Ndovie makini
Nina Makigraf cheka, sikusahau kundini
Nyie ni wachapa kazi, mabingwa muso mfano
Nakaditama tamati, kalamu chini naweka
Nasema hili kwa dhati, moyoni mwangu latoka
Muda 'ngepata laiti, wote ningewakumbuka
Redio ya Deutsche Welle, inavuma kwa kishindo!
Tanbihi: Shairi hili limeandikwa na Haji B. Mtulia wa Arusha -Tanzania kwa ajili ya maadhimisho ya miaka 50 ya DW.
Mhariri: Mohammed Khelef