DW miaka 50 na bado kijana
23 Januari 2013Miaka 50 kwa mwanaadamu huwa ni umri wa kujukuu. Kwa DW umekuwa umri wa kutukuu. Mwaka 1963 ilianza na watangazaji wawili. Siku ya Ijumaa asubuhi, Sheikh Omar Juma alikuwa akianza matangazo kwa mawaidha ya Kiislamu. Jumapili asubuhi mwenzake alikuwa akitoa mahubiri ya Kikristo. Matangazo ya mchana yalikuwa yakianza saa 8:15 mchana na kumalizika saa 8:50. Mashallah, hivi sasa DW inatangaza kwa masaa matatu kwa siku na ikiwa na watangazaji zaidi ya 12 mbali ya wale walioko nje ya Ujerumani.
Katika miaka ya 1960, mwamko wa harakati za kudai uhuru barani Afrika ulikuwa umepamba moto. Baba yangu alikuwa mwanaharakati na alifanya bidii sana hadi akafanikiwa kununua redio kwani kama zilivyokuwa adimu idhaa za Kiswahili, kadhalika redio zilikuwa haba.
Alikuwa amesoma Kiarabu pekee, na redio aliyonunua ilikuwa na maandishi ya herufi za Kizungu na stesheni zote zilikuwa zimesharekebishwa na akaandikiwa kwenye karatasi. Pale redio ilipobadilika stesheni zake kwa bahati mbaya, mimi nikawa napata bahati ya kukaribishwa kuzitafuta upya taratibu, maana tayari nilikuwa tayari nasoma shule. Ilikuwa ni fursa ya dhahabu.
Nililazimika kuwa makini na mwangalifu sana. Ingawa redio yetu ilikuwa kubwa kama kasha, haikunibabaisha hata kidogo, maana redio ni vitu viwili pekee: mitabendi na bendi ambayo mita hiyo ipo. Bahati iliyoje! Redio tulikuwa tunayo na maarifa ya kuifungua si haba. Hivyo pale mwaka 1963 Idhaa ya Kiswahili ya DW ilipozaliwa, wasikilizaji wa kuipokea tulikuwa tuko tayari.
Na tangu hapo, sisi wengine hatujaacha kuisilikiza, maana tunaridhishwa na ukweli kwamba DW imekuwa ikitimiza madhumuni ya Idhaa ya redio.
Madhumuni ya idhaa huwa ni kupasha habari kama zinavyojiri katika dunia yetu leo, kuelimisha na kuburudisha. Ndani ya kipindi hiki cha miaka 50, DW imetimiza madhumuni ya kuundwa kwake kwa ufanisi mkubwa.
Katika kupasha habari, DW huvifafanua vifungu vya habari zote muhimu kwa upana zaidi. Mara nyingi, habari muhimu ya wiki hupata nafasi pia ya kuchambuliwa kwenye kipindi maalum cha Maoni, ambacho hualika wataalamu kutoka nchi mbali mbali chini ya uwenyekiti wa mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili, kulijadiliana ama kutafuta ufumbuzi, nasaha na ushauri.
DW pia inatuelimisha kuhusu afya zetu. Kwa akinamama, mada zinazozungumziwa kwenye afya ni tangu zile za ujauzito, kujifunguwa hadi malezi ya mtoto. Jamii bora ni yenye afya nzuri ya nguvukazi yake.
Bali DW hutuelimisha pia kwenye masuala ya mazingira namna yanavyohusiana na kilimo na ufugaji wetu. Tunaelimishwa kuhusu Ulaya kwa ujumla na Ujerumani yenyewe pia. Na kwa kutambua umuhimu wa tabaka la vijana, DW haikuwaacha nyuma, maana wao ndio hasa wanaohitaji zaidi kuelimishwa dhidi ya kujitumbukiza katika bahari ya maisha yenye kina kirefu na mawimbi makali yenye papa wanaomeza watu wazima wazima.
Ulimwenguni leo tumefikia upeo wa ustaarabu na maendeleo. Katiba za nchi, mahakama na mashirika ya kutetea haki za binadamu: zote hizo zinatetea maslahi ya wananchi, lakini la kusikitisha ni kwamba haki hizo huvunjwa. Ndipo DW ikawa na kipindi maalum cha Mbiu ya Mnyonge kinachomulika udhalilishaji na unyanyasaji dhidi ya binaadamu. Dhamira ni kuifanya sauti ya asiye sauti isikike ulimwenguni na kwa kufanya hivyo, asidhulumiwe na aliyedhulumiwa arejeshewe haki yake, kwani ulimwengu umeshafahamu juu ya dhuluma hiyo.
Idhaa ya Kiswahili ya DW pia inatimiza vyema jukumu la kutoa burudani kwa wasikilizaji wake kwa uchaguzi mzuri wa nyimbo, mashairi ama hadithi na makala za michezo, hasa kandanda. Wengi wetu Afrika Mashariki na Kati ni mashabiki wa timu za Ulaya. Binafsi nilikuwa shabiki mkubwa wa Baryen Munich, kabla ya kustaafu.
Lakini, kuliko yote hayo, burudani yangu kuu kutoka DW ni mtiririko wa ufasaha, madaha na mbwembwe za watangazaji wakati wanapotangaza mvumo wa kishindo cha DW, ambao hakika humtingisa na kumdhibiti kila msikilizaji.
Kwa DW, msikilizaji ni sehemu ya matangazo. Sio tu kushirikishwa katika ujumbe mfupi wa simu ya mkononi au ukurasa wa Facebook, bali pia kupandishwa jukwaani kwa njia za barua na mazungumzo ya moja kwa moja ya simu ambapo humwaga dukuduku na kero zake shibe yake.
Basi DW tunakuombea kheri, mafanikio na umri mrefu. Ingawa kweli umefikisha nusu karne, kwetu ndio mwanzo unaanza tata. Pongezi na hongera zikumiminikie mfano wa mvua.
Indhari: Barua hii imeandikwa na msikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW, Ahmed Mohamed Basty, kutokea Kapenguria, Kitale nchini Kenya kwa ajili ya maadhimisho ya miaka 50 ya Idhaa hii.
Mhariri: Mohammed Khelef