1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

DW yamtunukia Anabel Hernández tuzo ya Uhuru wa Habari

28 Mei 2019

Tuzo ya mwaka huu ya Uhuru wa Habari inayotolewa na Deutsche Welle ametunukiwa mwandishi wa habari wa Mexico, Anabel Hernández, ambaye ametumia muda mwingi kuandika kuhusu biashara haramu ya madawa ya kulevya.

Freedom of Speech Award 2019
Picha: DW/F. Görner

"Ninashukuru kwa kupewa tuzo hii ya Uhuru wa Habari kwa sababu nadhani ni alama kuwa jamii ya kimataifa inatambua kuwa janga la makundi ya biashara ya madawa ya kulevya lililoko Mexico si jukumu la Wamexico pekee, bali la dunia nzima," alisema Anabel Hernández baada ya kupokea tuzo hiyo ya juu kabisa kimataifa kutolewa na Deutsche Welle, ambayo kawaida huwa wanatunukiwa wanahabari na watetezi wa haki za binaadamu waliotoa mchango mkubwa kwenye uhuru wa habari duniani kila mwaka. 

Kwa miongo kadhaa sasa, mwandishi huyu wa kike amekuwa akiandika bila kuchoka ripoti zinazoibua kashfa za ufisadi, biashara ya madawa ya kulevya, unyanyasaji kingono na hali ya wahalifu kulindwa wasiadhibiwe kisheria kwa makosa yao.

Mkurugenzi Mkuu wa DW, Peter Limbourg, alisema mwanahabari huyo mwenye umri wa miaka 47, ana ujasiri mkubwa sana wa kiuandishi. "Anabel daima amekuwa karibu na ripoti kwa utafiti wake, kufuatilia ufisadi kwa miaka mingi na kukusanya ushahidi wa kisheria na mapambano yake dhidi ya kuficha makosa na kuwalinda wakosaji. Hakika yeye ni mfano wa uandishi wa uchunguzi na wa kishujaa." Alisema Limbourg.

Kulazimika kukimbia nchi

Anabel Hernández akiwa na Tuzo yake ya Uhuru wa Habari iliyotolewa na Deutsche Welle Picha: DW/F. Görner

Mbali na uandishi wa habari, Anabel Hernández ni mwandishi wa vitabu na ni kitabu chake cha mwaka 2010 alichokiita "Taifa la Madawa ya Kulevya: Wababe wa Madawa wa Mexico na Baba Zao" ambacho kilimlazimisha kuikimbia nchi yake na kukimbilia kwanza Marekani na kisha Ulaya. Kwenye kitabu hicho, aliwataja majina makubwa yanayoshiriki kwenye biashara hiyo haramu.

"Niliyaweka bayana majina yote na muundo wote wa kundi la Sinaloa, wakiwemo watu ndani ya serikali ya Mexico ambao wakishirikiana na kundi hilo huku wakijifanya wanapigana vita vya uongo dhidi ya madawa ya kulevya. Nilitaja jina la rais mmoja wa zamani na rais wa wakati huo, waziri wa ulinzi, viongozi wa juu wa jeshi la polisi na mfanyabiashara mmoja mkubwa, ambao wote kwa pamoja walishirikiana kuunda kundi la Sinaloa," aliliambia kongamano la kimataifa la vyombo vya habari mjini Bonn.

Mwaka 2016 kitabu chake kingine kiitwacho "Mauaji ya Maangamizi Mexico: Ukweli Kuhusu Wanafunzi 43 Waliopotea" kilichapishwa. Ndani ya kitabu hicho, Anabel Hernández anachunguza undani wa mauaji wa wanafunzi 43 kwenye jimbo la Guerrero yam waka 2014 ili kuwapa wahanga na familia zao sauti.

Kongamano la kila mwaka la vyombo vya habari lililotayarishwa na DW lilitarajiwa kumalizika siku ya Jumanne (28 Mei).
 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW