1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Uhuru wa vyombo vya habariUjerumani

DW yatimiza miaka 70 - mizozo ya dunia yaiongezea umuhimu

11 Mei 2023

Kilichoanza kama kituo cha redio kikitangaza lugha ya Kijerumani kupitia mfumo wa masafa mafupi hivi sasa ni shirika la habari la kimataifa linaloajiri maelfu ya waandishi wanaofanya kazi katika lugha 32.

Berlin Festakt 70 Jahre Deutsche Welle
Picha: Ronka Oberhammer/DW

"Wapendwa wasikilizaji katika mataifa ya mbali..." Maneno hayo yaliotamkwa na rais wa shirikisho la Ujerumani wakati huo, Theodor Heuss, ndiyo yalikuwa ya kwanza kusikika hewani kupitia Deutsche Welle.

Ilikuwa Mei 3 mwaka 1953, na matamshi hayo yalikuwa sehemu ya hotuba ya kuikaribisha Deutsche Welle. Katika kipindi hicho cha kwanza, ilikuwa dhahiri kwamba lengo mahususi lilikuwa ni kuwapa fursa wasikilizaji wa mataifa mengine kufahamu picha halisi ya kisiasa, kiuchumi na kitamaduni wa Ujerumani.

DW ilianza kurusha matangazo yake kupitia masafa mafupi kutokea mjini Cologne na kufikia hadhira katika sehemu nyingi za dunia, lakini ikitumia lugha ya kijerumani tu. Lugha za kwanza za kigeni zilianza kuongezwa mwanzoni mwa mwaka 1954.

Na mwaka 1992, ilianzisha kituo chake cha runinga, na muda mfupi baadae, ikaanzisha makujwaa ya mitandao ya kijamii. Lakini enzi ya masafa mafupi imekwishapitwa na wakati, anasema mkurugenzi mkuu Peter Limbourg ambaye ametaja pia mafanikio ya shirika hilo.

"Tumekuwa shirika la habari la kimataifa linalowaweka mbele watumiaji. Nimeridhishwa sana na waliofanikisha wenzetu, na bila shaka kuona kwamba jukumu letu limekuwa muhimu zaidi katika miaka ya karibuni."

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz akiwahutubia wafanyakazi wa DW kwa njia ya video, aktika maadhimisho ya miaka 70 ya shirika hilo la kimataifa la utangazaji, Mei 10, 2023.Picha: Ronka Oberhammer/DW

"Tunashuhudia makabiliano makubwa katika vita barani Ulaya. Tunaona yote haya na shinikizo juu ya uhuru wa habari ni kubwa, sababu kwa nini jukumu letu bado lina umuhimu mkubwa," alisema mkurugenzi huyo wa DW.

Soma pia: Mwandishi wa El-Salvador atunukiwa Tuzo ya DW 2023

Nyuma ya neno "kituo cha utangazaji" kuna vipidi na huduma mbalimbali zinazotolewa na DW. Vipindi vya televisheni, vipindi vya redio pamoja na habari ziazotolewa kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii kwa lugha 32. Umuhimu wa simu za mkononi kama kifaa cha kufikisha huduma za DW, unazidi kuongezeka. Wasikilizaji wa zamani, kwa sasa ni wafuatiliaji ambao wengi ni vijana.

'Shinikizo ni kubwa mno'

Katika maadhimisho ya miaka hii 70 ya DW, baadhi ya mambo yanayotokea duniani yanafanana na hali ngumu kisiasa ya enzi ya kuasisiwa kwa DW. Kwa mara nyingine ulimwengu unashuhudia mazungumzo juu ya Vita Baridi, uhuru wa kujieleza na uhuru wa vyombo vya habari ambao uko hatarini kote duniani.

Miaka 70 ya shirika la utangazaji la DW

04:38

This browser does not support the video element.

Limbourg amesema "uandishi wa habari wa kimataifa unakabiliwa na changamoto kubwa inayozuia upatikanaji wa habari kwa kuwa tawala za kiimla zinajaribu kutuzuia waandishi wa habari na mara nyingine kuzichuja taarifa zetu na ninadhani hicho ni kitu kinachotishia uandishi wa habari kimataifa."

Hapa, sisi wote tunaoamini katika maadili ya kidemokrasia na tunaopaswa kutetea watu wengi duniani, hatuna budi kushirikiana ili tuendelee kupatikana kwa watumiaji wetu... watu wanaotuhitaji.” Hiyo ndiyo "changamoto kuu tunayopaswa kukabiliana nayo. "

Soma pia: Dunia yaadhimisha Siku ya Uhuru wa Habari

Ripoti kuhusiana na masuala ya Israel na chuki dhidi ya Wayahudi nazo ziliuingiza mashakani mfumo wa uhariri wa DW.

Hii ni baada ya mwishoni mwa mwaka 2021, DW kukabiliwa na madai yaliyotokana na taarifa iliyohusiana na chuki dhidi ya Wayahudi, iliyochapishwa kwenye akaunti za mitandao ya kijamii ya timu ya wahariri wa idhaa ya Kiarabu pamoja na vituo vyake washirika. Tangu hapo kumekuwepo na mijadala juu ya uhariri wa ripoti za Israeli.

Kulingana na Limbourg, "DW iliyashughulikia mara moja na kwa uthabiti mkubwa madai hayo, ikiwa ni pamoja na kujitenga na watu kadhaa." Akaongeza "Hii ni kwa sababu hakuna nafasi ya mawazo kama hayo hapa DW."

Waziri wa utamaduni wa Ujerumani Claudia Roth na mkurugenzi mkuu wa DW Peter Limbourg wakiwa katika sherehe za kuadhimisha miaka 70 ya DW, Mei 10, 2023.Picha: Jörg Carstensen/dpa/picture alliance

Hata hivyo, uchunguzi huru pia ulithibitisha kuwa machapisho ya wahariri wa DW katika suala hili hayana kasoro. Limbourg alisema, DW inataka kutuma ishara wazi kwamba inapinga ubaguzi wa rangi, chuki dhidi ya Wayahudi na ubaguzi.

Soma pia:Uhuru wa vyombo vya habari uko wapi? 

Tangu Urusi ilipoivamia Ukraine, waandishi wengi wamekuwa Ukraine wakiripoti na hasa mashariki mwa nchi hiyo. Na Yuri Rescheto, aliyekuweko studio za DW za Moscow tangu Machi 2022, kwa sasa ndio mkuu wa studio hizo, zilizojengwa katika mji mkubwa wa Latvia, Riga, mwishoni mwa mwaka 2022.

"Tupo hapa, hatujafa na hatujakaa kimya na hatujafutwa". Huku Riga timu inafanya kazi kwa uhuru na hapo tunaweza kusema chochote. Mnatusikia, mnatuona na kutusoma, anasema Rescheto.

Mwandishi: Strack, Christoph

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW