1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

EAC yakumbwa na ukata, wanachama wakwepa kulipa michango

Veronica Natalis
10 Machi 2026

Jumuiya ya Afrika Mashariki inakabiliwa na upungufu mkubwa wa fedha. Ni nchi mbili tu kati ya nane katika jumuiya hiyo ndio zinaelezwa kulipa kikamilifu michango yao ya mwaka.

Tansania Arusha | Mkutano wa kilele wa EAC
Viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki katika mkutano wa kilele wa EAC mjini ArushaPicha: Philbert Rweyemamu/EAC

Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) inakabiliwa na changamoto kubwa ya kifedha inayotishia uendeshaji wa baadhi ya taasisi zake muhimu, huku ucheleweshaji wa michango kutoka kwa nchi wanachama ukitajwa kuwa chanzo kikuu cha tatizo hilo.

Tovuti rasmi ya Mahakama ya Afrika Mashariki (EACJ), moja ya taasisi muhimu za utoaji haki katika jumuiya hiyo kongwe barani Afrika, ilichapisha taarifa mwaka 2024 ikieleza kuwa mahakama hiyo imeshindwa kuendesha baadhi ya shughuli zake kutokana na ukosefu wa fedha.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kuchelewa kwa michango kutoka nchi wanachama kulilazimisha kusitishwa kwa baadhi ya vikao vya kusikiliza kesi. Hali hiyo ilisababisha kuongezeka kwa mlundikano wa zaidi ya kesi 200 ambazo hazijapatiwa usikilizwaji kwa wakati.

Viongozi wakiri changamoto ya michango

Kwa miaka kadhaa sasa, viongozi wa juu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wamekuwa wakikiri kuwepo kwa tatizo la ucheleweshaji au kutolipwa kabisa kwa michango ya nchi wanachama. Hata hivyo, kumekuwa na kusita kuzitaja wazi nchi ambazo zimekuwa zikichelewesha au kutotoa michango hiyo.

Katika mkutano wa wakuu wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika mwezi Machi jijini Arusha, Tanzania, mwenyekiti wa jumuiya hiyo aliyemaliza muda wake, Rais wa Kenya William Ruto, alitangaza hatua kadhaa zinazolenga kunusuru jumuiya hiyo dhidi ya uhaba wa fedha.

Rais wa Kenya William Ruto akiwasili Arusha kuhudhuria mmoja ya vikao vya wakuu wa jumuiya ya Afrika Mashariki.Picha: Philbert Rweyemamu/EAC

"Kuanzia sasa na kuendelea ili kuwa na uchangiaji wa usawa, nchi zinazonufaika zaidi na Jumuiya, na zenye uchumi mkubwa zaidi, zitachangia zaidi kuliko nchi ambazo hazinufaiki sana na Jumuiya na zenye uchumi wa chini.

Na vilevile mishahara ya wabunge wa Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki ambayo huchukua karibu asilimia 30 ya bajeti ya Jumuiya sasa italipwa na nchi zao,” alisema Ruto.

Makubaliano ya kupunguza madeni

Katika mkutano huo, marais wa nchi nane wanachama pia walifikia makubaliano ya kupunguza mzigo wa madeni ya michango kwa nchi zinazodaiwa.

Kwa mujibu wa makubaliano hayo, nchi ambazo zina madeni ya michango zimesamehewa asilimia 50 ya madeni yao, huku asilimia 50 iliyobaki ikitakiwa kulipwa ndani ya kipindi cha miaka miwili.

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki aliyemaliza muda wake, Veronica Nduva, alisema changamoto za kifedha zilikuwa miongoni mwa matatizo makubwa aliyokutana nayo alipokuwa akiiongoza taasisi hiyo.

Kongo mwanachama mpya wa jumuiya ya EAC

03:04

This browser does not support the video element.

"Nilipoingia madarakani, Jumuiya ya Afrika Mashariki ilikuwa inakabiliwa na changamoto za kiuchumi, uaminifu wa taasisi na upungufu wa rasilimali watu. Niliweka vipaumbele vyangu katika kuimarisha uthabiti wa taasisi na kuiweka upya Jumuiya inayowafikisha watu katika kitovu cha maendeleo,” alisema Nduva.

Vyanzo vya mapato vya jumuiya

Jumuiya ya Afrika Mashariki huendeshwa kwa kiasi kikubwa kupitia michango ya nchi wanachama. Vyanzo vingine vya mapato ni pamoja na ada za usajili wa biashara, huduma za kisheria pamoja na fedha kutoka miradi ya pamoja ya kikanda.

Hata hivyo, wachambuzi wa masuala ya kikanda wanaonya kuwa bila mfumo thabiti wa kuhakikisha nchi wanachama zinatimiza wajibu wao wa kifedha, taasisi muhimu za Jumuiya kama Mahakama ya Afrika Mashariki na Bunge la Afrika Mashariki zinaweza kuendelea kukabiliwa na hatari ya kushindwa kutekeleza majukumu yao kikamilifu.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW