EALA yapitisha sheria dhidi ya ukeketaji
30 Januari 2017Bunge la jumuiya ya Afrika mashariki maarufu kama EALA lilipanga kujadili na kupitisha miswada kadhaa kwenye vikao vyake vilivyofululiza kwa wiki mbili katika majengo ya bunge la Uganda. Miongoni mwa miswaada hiyo ulikuwa ule wa kupiga marufuku ukeketaji katika mataifa wananchama.
Kulingana na spika wa bunge hilo Daniel Kidega, sheria hiyo ni muhimu kulinda haki za wanawake na wasichana wanaoathirika kutokana na tamaduni za jamii mbalimbali katika mataifa wanachama wa jumuiya hiyo.
"Mswaada ambao unaharamisha vitendo vinavyokiuka haki za binadamu za wasichana wetu pale wanapodhurika kimwili kwa madai ya kutii utamaduni ulipitishwa na kuwa sharia, hayo ni mafanikio mazuri sana," alisema spika Kidega katika mkutano na waandishi habari mjini Kampala.
Watetezi wa haki za wanawake wanadai baada ya sheria kama hiyo ya kuharamisha ukeketaji kupitishwa nchini Uganda, baadhi ya watu wa jamii za Uganda zinazozingatia desturi hiyo wamekuwa wakiwavusha wasichana mipaka na kuwafanyia ukeketaji katika mataifa jirani.
Jamii zinazohamia Afrika Mashariki kutoka Somalia na Ethiopia nazo zimetajwa kushiriki katika maovu hayo na kuwepo kwa sheria hiyo itakuwa hatua muhimu kuwadhibiti.
Ulinzi kwa walemavu wa ngozi
Mswaada binafsi wa kuwalinda watu walio na ulemavu wa ngozi uliowasilishwa na mbunge mwakilishi kutoka Tanzania Shyrose Bhanji utajadiliwa zaidi katika vikao vijavyo.
Mswaada mwingine ulipitishwa na kuwa sheria ni ule wa mahakama huru ya haki ya afrika mashariki. Sheria hiyo inalenga kuipa uwezo mahakama kuendesha shughuli zake ikitambuliwa kuwa miongoni mwa miundo ya kulinda haki za raia wa jumuiya.
Spika wa bunge la EALA Daniel Kidega kutoka Uganda aliorodhesha miswaada mingine ambayo itajadiliwa katika vikao vijavyo. "Mjadala kuhusu mswaada juu ya masuala ya usawa wa kijinsia haukukamilika. Lakini umefika hatua ya pili. Kutokana na ukosefu wa muda tutaushughulikia kwenye vikao vitakavyofuata."
Kwenye mojawapo ya vikao vya bunge hilo, matumizi ya lugha ya Kiswahili katika shughuli za bunge lijalo yalipendekezwa. Hata hivyo, wabunge kutoka Uganda walionekana kusita kuunga mkono hoja hiyo, baadhi yao wakielezea kuwa suala hilo linahitaji muda kuzingatiwa.
Kwa sasa wagombea mbalimbali wamejitokeza kuwania nafasi katika bunge la nne linalotarajiwa kuchukua mahala pa lile la sasa baada ya mwezi Julai mwaka huu.
Mwandishi: Lubega Emmanuel DW Kampala
Mhariri: Saumu Yusuf