Ebola barani Afrika: Kwa nini bado ni tishio la kudumu
22 Agosti 2026
Shirika la Afya Duniani (WHO) lilitangaza hali ya dharura ya afya ya umma ya kimataifa Mei 17, 2026, baada ya taarifa za mlipuko wa Ebola unaosababishwa na virusi vya Bundibugyo katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Uganda.
Hata hivyo, WHO ilisema mlipuko huo "haujakidhi vigezo vya kutangazwa kuwa janga la dunia.”
Hatua hiyo inakuja muda mfupi baada ya mlipuko wa virusi vya hanta kwenye meli ya MV Hondius — na wakati WHO ikifanya Mkutano Mkuu wake wa 79 kuanzia Mei 18 hadi 23, 2026.
Unachopaswa kujua kuhusu Ebola:
• Ebola huharibu mishipa ya damu na kusababisha kutokwa damu ndani ya mwili
• Husambaa kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu na kati ya watu kupitia kugusana na damu, viungo vya mwili, majimaji na ute wa mwili
• Baadhi ya aina za Ebola zinaweza kuzuiwa kwa chanjo na kutibiwa kwa dawa
• Ebola iligunduliwa kwa mara ya kwanza mwaka 1976, na mlipuko mkubwa zaidi kati ya 2014–2016 uliua zaidi ya watu 10,000 Afrika ya Kati.
Ebola inasalia kuwa changamoto inayoendelea kwa wananchi na mamlaka katika maeneo yaliyoathirika. Maendeleo ya chanjo yanaweza kusaidia kupunguza madhara ya ugonjwa huo.
Mlipuko mingi ya Ebola imesababishwa na aina ya virusi vya Zaire Ebola (Zaire ebolavirus) na Sudan Ebola (Sudan ebolavirus).
Katika milipuko ya hivi karibuni, iliyokuwa na idadi kubwa ya maambukizi, watafiti wametumia mazingira hayo halisi kujaribu chanjo zinazotengenezwa.
Milipuko mikubwa zaidi ya Ebola ilikuwa ipi?
Mlipuko mkubwa zaidi wa Ebola ulitokea karibu miaka 40 baada ya ugonjwa huo kugunduliwa kwa mara ya kwanza.
Kati ya mwaka 2014 na 2016, Ebola ilisambaa kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) katika Afrika ya Kati hadi Liberia, Guinea na Sierra Leone magharibi mwa Afrika. Kulikuwa na zaidi ya maambukizi 28,600 na vifo 10,000.
Kuanzia 2018 hadi 2020, Ebola ilisambaa tena kutoka DRC hadi Uganda. Pia kumekuwa na milipuko mingine nchini Gabon, Afrika Kusini, Ivory Coast, Nigeria, Mali na Senegal, iliyosababisha vifo vya angalau watu 2,000.
Ebola iligunduliwa karibu na Mto Ebola wakati wa milipuko miwili ya wakati mmoja mwaka 1976 — nchini Zaire, ambayo sasa ni DRC, na Sudan Kusini.
Ugonjwa wa Ebola (EVD), uliopewa jina la mto huo, ndio aina hatari zaidi ya virusi hivyo. Kiwango cha manusura ni takriban asilimia 10 pekee ya wagonjwa.
Ugonjwa wa Vorusi vya Sudan (SVD) husababisha vifo katika karibu asilimia 50 ya maambukizi.
Aina ya tatu inayopatikana zaidi Afrika ni virusi vya Bundibugyo, vilivyogunduliwa mwaka 2007.
Dalili zake zinafanana: homa, kichefuchefu, udhaifu, kupoteza hamu ya kula na kutokwa damu kusikoelezeka. Maumivu ya kifua yanaweza kutokea zaidi kwa wagonjwa wa SVD kuliko EVD.
Ebola hutibiwaje?
Ikiwahi kugunduliwa mapema, matibabu hospitalini kwa kutumia maji ya kunywa, maji ya mishipa na dawa yanaweza kusaidia kupunguza hatari ya kifo.
Moja ya dawa hizo ni Ebanga, dawa inayotumia kingamwili kuzuia virusi kuingia kwenye seli na hivyo kupunguza kasi ya kusambaa mwilini.
Dawa nyingine ni Inmazeb, ambayo ni mchanganyiko wa kingamwili tatu.
Katika matibabu yote mawili, wagonjwa wanashauriwa kuepuka kutumia chanjo zenye virusi hai kwa wakati mmoja.
Shirika la Afya Duniani (WHO) halishauri wagonjwa kutibiwa nyumbani, hasa bila msaada wa wataalamu wa afya. Virusi vya Ebola huambukiza kwa urahisi sana na watu wengine wa nyumbani wanaweza kuambukizwa.
Matibabu mengine ni pamoja na kuongezewa damu, dawa za kupunguza maumivu, kichefuchefu, kutapika na kuharisha, pamoja na kutibu magonjwa mengine yanayoambatana nayo kama malaria.
Kuna chanjo dhidi ya Ebola?
Chanjo ya Ervebo imeidhinishwa kutumika Marekani na Umoja wa Ulaya.
Chanjo hiyo inaweza kutumika kuwalinda watu wazima na watoto dhidi ya ugonjwa wa Ebola (EVD). Hata hivyo, masharti hutofautiana — Ulaya imeidhinisha matumizi yake kwa watoto kuanzia mwaka mmoja, wakati Marekani imeidhinisha kwa watu wenye umri wa miaka 18 na zaidi pekee.
Idhini ya dawa na chanjo kutoka taasisi kuu za Marekani na Ulaya, yaani FDA na EMA, hutambuliwa kama viwango vya kimataifa, hivyo Ervebo inaweza pia kutumika Afrika.
Pia, watu wanaosafiri kwenda maeneo yaliyoathiriwa na Ebola wanashauriwa kupata chanjo kabla ya safari.
Ervebo ni nini?
Ervebo ni chanjo yenye virusi vilivyodhoofishwa.
Hii ina maana kuwa chanjo hiyo ina protini dhaifu ya virusi vya Ebola (EVD), ambayo haina nguvu ya kusababisha maambukizi kamili lakini inatosha kuuchochea mwili kujenga kinga.
Kisha, mtu aliyepata chanjo akikutana na virusi halisi baadaye, mwili wake huwa tayari kujikinga dhidi ya maambukizi hayo.
Mwezi Februari 2025, International AIDS Vaccine Initiative, Wizara ya Afya ya Uganda, Chuo Kikuu cha Makerere mjini Kampala na WHO walizindua majaribio ya chanjo dhidi ya virusi vya Sudan (SVD).
Hilo lilikuwa jaribio la kwanza kufanyika wakati wa mlipuko halisi wa ugonjwa huo — mlipuko wa sita wa Uganda wa aina ya Sudan ya Ebola.
Chanjo ya Sudan imeundwa kwa mfumo unaofanana na Ervebo. Inaelezwa kuwa moja ya chanjo zenye matumaini makubwa dhidi ya Ebola na virusi vingine vya familia ya filoviruses, ikiwemo Marburg.