Ebola iliotokea 2007 ni aina mpya-Wanasayansi
21 Novemba 2008Virusi hivyo vya Ebola vimepewa jina la Bundibugyo kutokana na kuwa ndiko ulipotokea mwaka jana na kuwauwa watu 37.
Wanasayansi wamesema kuwa aina ya virusi vya homa ya Ebola iliotokea Bundibugyo nchini Uganda inatofautiana kabisa kwa hali na umbo na vile vya Ebola za aina tatu za mwanzo zilizotokea katika eneo la Afrika Mashariki na Kati.
Aina zingine ni Ebola ya Zaire,inayosemekana ni kali mno kwani husababisha vifo kati ya asili mia 80 hadi 90 ya wagonjwa wanaoambukiwazwa.Zingine ni Virusi vya Ebola vya Sudan inayoshika nafasi ya pili. nafasi ya tatu inachukuliwa na virusi vya Ebola vya Cote d'ivore vilivyogunduliwa mwaka wa 1994 ambavyo watalamu wanasema kuwa hivyo havina makali sana.
Virusi vingine vya Ebola vinaitwa virusi vya Ebola vya Reston ambavyo viligunduliwa katika kituo cha utafiti nchini Marekani mwaka wa 1989.Inadaiwa kuwa vilitokana na kima walioagizwa kutoka nje kwa ajili ya kutumiwa katika maabara. Watu wanne waliambikzwa na hakuna hata mmoja aliefariki.
Katika utafiti wa wanasayansi hao ambao umechapishwa katika jarida la Kisayansi la Marekani la Pathogens kupitia mtandao wa Public Library of Science-PLoS kwa kifupi, unasema kuwa zaidi ya mtu mmoja katika kila idadi ya watatu walioambukizwa na virusi hivyo, katika wilaya ya Bundibugyo alifariki.
Virusi vya Ebola pamoja na Marburg ndio virusi muhimu vya aina mbili vinavyosababisha homa inayojulikana katika herufi za kitalamu kama VHF. Homa hiyo inasemekana ni mbaya sana.
Dalili za mwanzo za homa hiyo ya VHF ni mwili kuwa na joto kali,mchoko, kupatwa kizunguzungu, maumivu ya misuli pamoja na kuharisha. Dalili hizo kawaida zinakosewa na kudhaniwa ni za homa nyingine kama vile mafua pamoja na homa ya njano.Hii ni kwa sababu homa ya VHF si kawaida kupatikana.
Virusi vya homa ya VHF humfanya mgonjwa kuanza kutokwa damu kupitia ngozi yake.Lakini hali ikiwa mbaya sana, mgonjwa huyo anaweza akatokwa damu mdomoni, kwenye masikio, na macho.
Mgonjwa wa aina hiyo anaweza kufariki katika kipindi cha siku kati ya tatu na saba bada ya kuonyesha dalili hizo kutokan na aidha kutokwa damu nyingi,ama kutetemeka.
Ebola ilijitokeza mara ya kwanza mwaka wa 1976 katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo ,wakati huo ikiitwa Zaire.Homa hiyo ikabatizwa jina hilo kutokana na jina la mto wa Ebola unaopatikana eneo homa hiyo ilipolipukia.
Shirika la afya duniani la WHO linasema kuwa tangu ugonjwa huo uzuke watu wanaokaribia 2,000 wameorodheshwa kuambukizwa na na ugonjwa huo,huku wengine 1,200 na ushei kuaga dunia.
Madaktari wa Uganda na Marekani walioandika ripoti hiyo ya uchunguzi wanasema kuwa aina mpya ya virusi vya Ebola ya VHF ilijulikana baada ya kuwaambukiza watu katika sehemu za Bundibugyo na Kikyo Novemba mwa wa 2007.Na uchunguzi wa sampuli 20 za damu ulionyesha kama hivyo ni virusi vya Ebola ambavyo ni tofauti.