1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ebola: Tiba ya majaribio yazinduliwa Mashariki mwa DR Kongo

5 Julai 2026

Raia nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wamepata matumaini mapya baada ya kuanza kwa majaribio ya dawa mbili zinazolenga kuudhibiti mlipuko wa ugonjwa wa Ebola.

DR Kongo Rwampara 2026 | Mhudumu wa afya katika kituo cha kudhibiti Ebola cha Rwampara
Mhudumu wa afya katika kituo cha kudhibiti Ebola cha Rwampara huko Ituri nchini KongoPicha: Jospin Mwisha/AFP

Uzinduzi wa tiba hiyo umefanyika katika kituo cha matibabu ya Ebola kilichopo kwenye hospitali moja huko Bunia, katika jimbo la Ituri mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Watalaamu wameanza majaribio hayo baada ya kufanyika utafiti wa matibabu ya aina mbili ya Ebola yanayolenga  kuudhibiti mlipuko wa ugonjwa huo unaoendelea kuongezeka. Wakaazi katika eneo hilo la mashariki mwa Kongo wanaweka matumaini yao kwenye majaribio hayo mapya ya matibabu ya Ebola.

Wahudumu wanafuata hatua zote za kujikinga baada ya kuushughulikia mwili wa mtu aliyekufa kutokana na ugonjwa wa Ebola huko BuniaPicha: Moses Sawasawa/AP Photo/picture alliance

Shirika la Afya duniani, WHO limesema mshiriki wa kwanza tayari amejiandikisha katika utafiti huo, ambao unatathmini kama dawa ya kufubaza virusi aina ya remdesivir inaweza kupambana na mlipuko huo mpya au ikichanganywa na dawa ya kuimarisha kingamwili aina ya MBP134, zinaweza kuboresha maisha ya wagonjwa walioambukizwa virusi vipya vya Ebola kwa jina Bundibugyo.

Kulingana na mshauri wa utafiti wa WHO Dkt. Vasee Moorthy wanaoshiriki kwenye majaribio hayo watafuatiliwa kwa siku 28 mfululizo mara baada ya kuanza matibabu.

Profesa Yap Boum, mkuu wa matibabu ya dharura katika Vituo vya Afrika vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa amesema walengwa ni wagonjwa waliothibitishwa kuwa wanaugua ugonjwa wa Ebola na wanaopokea matibabu kwenye vituo maalum vya matibabu. Amesema awamu ya pili ya majaribio itajumuisha wafanyakazi wa afya, watu walio karibu na wagonjwa pamoja na wale walio katika hatari kubwa ya kuambukizwa.

Naye Profesa Placide Mbala, mratibu wa shughuli za maabara kuhusiana na mlipuko wa sasa, amesema utafiti unaweza kuendelea kwa miezi mitatu mpaka sita, kulingana na jinsi mlipuko huo unavyobadilika haraka.

Majaribio haya yanatoa matumaini kwa wakazi wanaoishi katika eneo ambalo virusi vya Ebola vimeenea na kwa wakazi wengi wa Bunia, majaribio hayo ni chanzo adimu cha kutia moyo baada ya wiki kadhaa za hofu inayoongezeka kila kukicha.

WHO inaunga mkono maaribio hayo yanayofanywa kwa ushirikiano wa taasisi ya kitaifa ya utafiti wa matibabu ya kibiolojia ya Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (INRB), Chuo Kikuu cha Oxford cha Uingereza, Taasisi ya Tiba ya nchi za joto ya mjini Antwerp pamoja na mashirika mengine ya kimataifa afya.

Mkuu wa Shirika la Afya Duniani, Tedros Adhanom GhebreyesusPicha: Martial Trezzini/KEYSTONE/picture alliance

Mkuu wa Shirika la Afya Duniani, Tedros Adhanom Ghebreyesus, amesema virusi vya Bundibugyo vinavyosababisha mlipuko huu mpya, sio sawa na vingine vinavyosababisha ugonjwa wa Ebola na mpaka sasa hakuna matibabu au chanjo ya kupambana navyo. Zaidi ya watu 1,400 wamegunduliwa kuwa wameambukizwa virusi hivyo na watu wengine 438 wamekufa.

Majaribio ya dawa hizo mbili yamepangiwa kupelekwa kwenye maeneo mengine mara tu dawa hizo zitakapothibitishwa kuwa ni salama.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW