ECOWAS bado inatumai kuna fursa ya upatanishi Niger
8 Agosti 2023Hapo jana, waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken, alisema kuwa diplomasia ndio chaguo bora kwa jumuiya ya kimataifa kushughulikia mzozo huo wa mapinduzi nchini Niger. Blinken amekiambia kituo cha redio cha RFI kwamba chaguo hilo ndilo linalotumiwa kwasasa na Jumuiya ya Kiuchumi ya Afrika Magharibi, ECOWAS pamoja na Marekani. Hii leo, raia wa Niger leo waliamkia hali ya kutokuwa na uhakika kuhusu iwapo Jumuiya ya ECOWAS itazingatia tishio lake la kutumia nguvu ya kijeshi kujaribu kumrejesha madarakani rais Mohamed Bazoum ama iwapo diplomasia ya mwisho itatawala, takriban wiki mbili baada ya wanajeshi walioasi kuipindua serikali ya raia aliyechaguliwa kidemokrasia. Jumuiya ya ECOWAS, ilikuwa imewapa viongozi hao wa mapinduzi hadi Jumapili kumuachia huru na kumrejesha madarakani Bazoum ama kutishia kutumia nguvu.
Kaimu naibu waziri wa nje wa Marekani akutana na viongozi wa mapinduzi wa Niger
Hapo jana, kaimu naibu waziri wa mambo ya nje wa Marekani Victoria Nuland, alikutana na viongozi wa mapinduzi nchini Niger na kusema walikataa kumruhusu kukutana na Bazoum, ambaye alimtaja kuwa chini kifungo cha nyumbani. Alisema wanajeshi hao walioasi hawakukubali ombi lake la kuanza kwa mazungumzo na kudumisha uongozi wa kikatiba.
Hata hivyo, msemaji wa wizara ya ulinzi ya Marekani Matthew Miller amesema maafisa wa wizara ya usalama walizungumza na Bazoum na kwamba waziri alizungumza na waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa kuhusu jinsi ya kutatua kwa ufanisi hali ya kudumisha utaratibu wa kikatiba.
ECOWAS, Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika kukutana leo
Katika hatua nyingine, afisa mmoja wa nje aliyezungumza kwa sharti la kutotambulishwa, ameliambia shirika la habari la AP kwamba mataifa wanachama wa ECOWAS, Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika wanatarajiwa kushiriki katika mazungumzo leo katika mji mkuu wa Niger, Niamey. Mazungumzo yanatarajiwa kuendelea wiki nzima. Jumuiya ya ECOWAS pia inatarajiwa kukutana tena Alhamisi mjini Abuja, nchini Nigeria, kuzungumzia hali nchini Niger.
Viongozi wa mapinduzi nchini Niger wameapa kupinga shinikizo kutoka nje za kumrejesha madarakani Rais Bazoum, baada ya ECOWAS kuwekwa vikwazo na washirika wa Magharibi kusimamisha misaada kwa taifa hilo. Niger imekuwa mshirika muhimu kwa Marekani na mataifa mengine ya Ulaya ambayo zinaichukulia kuwa moja kati ya mataifa ya mwisho yanayozingatia demokrasia katika eneo la Sahel, Kusini mwa jangwa la Sahara ambayo inaweza kushirikiana nayo kupambana na ghasia zinazoongezeka za itikadi kali zinahusishwa na kundi la wanamgambo la al- Qaida na lile linalojiita dola la kiislamu IS.