1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaBurkina Faso

ECOWAS kudhoofika baada ya wanachama wake 3 kujiondoa?

1 Februari 2024

Mali, Niger na Burkina Faso zimejiondoa kwenye Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi, ECOWAS. Jee hatua hiyo inaamanisha nini kwa nchi hizo tatu zisizokuwa na bandari?

Abuja, Nigeria | Rais wa Guinea-Bissau Umaro Sissoco Embalo akiwa katika kikao cha ECOWAS.
Rais wa Guinea-Bissau Umaro Sissoco Embalo akiwa katika kikao cha 64 cha Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Afrika Magharibi (ECOWAS) mjini Abuja.Picha: Kola Sulaimon/AFP

Wachambuzi wanahaofia kuwa hatua ya nchi hizo tatu itaidhoofisha zaidi jumuiya ya ECOWAS na pia huenda  ikasababisha vurumai kubwa kwenye eneo la nchi za jumuiya hiyo.

Viongozi wa kijeshi wa Mali, Niger na Burkina Faso, walioingia madarakani hivi karibuni kwa njia ya mapinduzi wamesema  katika tamko lao la pamoja kwamba watajiondoa kwenye jumuiya ya ECOWAS bila ya kuchelewa.

Viongozi hao wameilaumu  jumuiya hiyo kwa kutowaunga mkono na pia kwa vikwazo ambavyo wameviita kuwa si vya kibinadamu.

Hata hivyo mchambuzi wa Burkina Faso, Lassane Zorome amesema Ecowas inahimiza maadili ya kidemokrasia. Na kwa hivyo, mchambuzi huyo ameeleza kuwa jambo la kwanza kwa viongozi wa kijeshi wa nchi hizo tatu ni kujiondoa ECOWAS, ili kukimbia mashinikizo.

Soma pia:Mzozo wa Sahel waendelea kufukuta

Lakini mchambuzi wa sera wa jopo la wataalamu nchini Nigeria Ovigwe Eguegu, amesema uamuzi wa nchi hizo tatu wa kuipa kisogo jumuiya ya Ecowas ni pigo kwa umoja huo ambao ni muhimu kisiasa na kiuchumi.

Amesema nchi hizo tatu ni muhimu kwa usalama wa eneo la Afrika magharibi na hasa usalama wa ukanda wa Sahel.

Naye meneja wa mradi wa Sahel kwenye chuo cha mitaala ya usalama Fahiraman Kone ameeleza kuwa uamuzi wa  Mali, Niger na Burkina Faso kujitoa ECOWAS utaidhoofisha zaidi jumuiya hiyo.

Eneo la Sahel sasa limekuwa kitovu cha ugaidi duniani. Mnamo mwaka 2022, asilimia 43 ya vifo vilivyotokana na vitendo vya kigaidi vilivyotukia kwenye sehemu hiyo.

Afrika magharibi inaathirika na vitendo hivyo hadi kwenye nchi tulivu kama Togo, Benin na Ivory Coast.

Wachambuzi: Mwelekeo wa kitisho cha usalama

Kusambaratika kwa ushirikiano wa kisiasa kwenye jumuiya ya ECOWAS na hatua dhaifu za kukabiliana na magaidi maana yake ni kuwepo hatari kubwa ya kuzorota zaidi kwa usalama kwenye eneo la magharibi mwa Afrika amesema, Fahiraman Kone meneja wa mradi wa Sahel kwenye chuo cha mitaala ya usalama.

Kamati ya Wakuu wa Ulinzi wa ECOWAS walipokutana mjini Accra kujadili hali ya usalama katika kanda, August 18, 2023.Picha: Francis Kokoroko/REUTERS

Ameeleza kuwa hii ni mara ya kwanza tangu kuundwa kwa jumuiya ya ECOWAS miaka karibu 50 iliyopita kwamba baadhi ya wanachama wamejitoa.

Jumuiya ya ECOWAS yenyewe imesema katika tamko kuwa nchi hizo tatu zilizojiondoa zilikuwa wanachama muhimu wa jumuiya hiyo na kwamba yenyewe itaendelea kujizatiti katika juhudi za kutafuta suluhisho kwa njia ya mazungumzo.

Soma pia:Umoja wa Afrika wasema "umefadhishwa" na kujiondoa Niger, Mali na burkina Fasso ndani ya ECOWAS

Uamuzi wa Mali, Niger na Burkina Faso umetokana na hatua ya ECOWAS ya kuzisimamisha uanachama nchi hizo na kuziwekea vikwazwo baada ya viongozi wa kijeshi wa nchi hizo kutwaa mamlaka katika nchi zao.

Jumuiya ya ECOWAS pia ilitishia kuchukua hatua za kijeshidhidi ya nchi hizo ili kuzilazimisha kurejea kwenye demokrasia.

Kutokana na kitisho  hicho Mali,Niger na Burkina Faso zimeunda mfungamano wa ulinzi.  Ni maoni ya wachambuzi kwamba jumuiya ya  ECOWAS ilifanya kosa kutoa kitisho hicho.

Vikwazo vya kiuchumi na tishio la kuivamia Niger havikuleta tija. Badala yake umaarufu wa jumuiya ya ECOWAS   ulianguka.

Mali na Burkia Faso zimesema zimeshawasilisha taarifa rasmi ya kujiondoa.

Haujulikani ni kwa kiasi gani uhuru wa watu kusafiri au kusafirisha mizigo utaathirika baada ya nchi hito tatu kujiengua? 

Ufafanuzi:Kwanini Niger ni muhimu kwa mataifa ya magharibi?

01:26

This browser does not support the video element.