1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroAfrika

ECOWAS ni nini na kwanini mataifa matatu yamejiondoa?

29 Januari 2024

Mvutano wa miezi kadhaa kati ya nchi tatu zilizokumbwa na mapinduzi za Afrika Magharibi na jumuiya ya ECOWAS uliongezeka baada ya mataifa hayo kutangaza kujiotoa mara moja kwenye jumuiya hiyo na kuituhumu kwa kukosa utu.

Nigeria | Mkutano wa Kilele wa ECOWAS
Viongozi wa ECOWAS wakiwa mjini Abuja, Nigeria. Jumuiya hiyo imepata pigo kwa wanachama wake watatu kuamua kujotoa.Picha: Präsidentschaft von Niger

Katika taarifa yao ya pamoja Jumapili, watawala wa kijeshi wa mataifa ya Niger, Mali na Burkina Faso walisema badala ya kuzisaidia nchi zao kupambana na matishio ya usalama yanayowakabili, ECOWAS iliyawekea vikwazo "visivyo halali, vya kinyama na visivyowajibika" walipofanya mapinduzi "ili kuchukua hatima yao" mikononi mwao wenyewe."

Ni mara ya kwanza katika kaŕibu miaka 50 ya kuwepo kwa jumuiya hiyo ambapo wanachama wake wanajiondoa kwa njia hiyo. Wachambuzi wanasema ni pigo kubwa lisilo kifani kwa kundi hilo na ni tishio zaidi kwa uthabiti wa eneo hilo.

ECOWAS ni muhimu kiasi gani?

Jumuiya hiyo ya Kiuchumi ya mataifa 15 ya kikanda ya Afrika Magharibi ilianzishwa mwaka 1975 ikiwa na lengo moja: "Kukuza ushirikiano na ushirikiano ... ili kuinua viwango vya maisha ya watu wake, na kudumisha na kuimarisha utulivu wa kiuchumi. "

Tangu wakati huo imekua na kuwa mamlaka kuu ya kisiasa ya eneo hilo, mara nyingi ikishirikiana na mataifa kutatua changamoto za ndani katika nyanja mbalimbali kuanzia siasa hadi uchumi na usalama.

Watawala wa Kijeshi wa Mali (Assimi Goita), Niger (Abdourahamane Tiani) na Burkina Faso (Ibrahim Traoré), ambao wametangaza kuyatoa mataifa yao kutoka ECOWAS.Picha: Francis Kokoroko/REUTERS; ORTN - Télé Sahel/AFP/Getty; Mikhail Metzel/TASS/picture alliance

Chini ya uongozi wa sasa wa Nigeria, nguvu ya kiuchumi ya Afrika Magharibi, ECOWAS inahitajika zaidi kuliko hapo awali huku uthabiti wa eneo hilo ukitishiwa na mapinduzi na migogoro ya usalama. Inafanya kazi "katika ulimwengu ... ambapo unahitaji kuwa na nguvu katika jumuiya moja na kuungana katika mshikamano," alisema Babacar Ndiaye, kutoka Taasisi ya Mafunzo ya Amani ya Timbuktu yenye makao yake makuu nchini Senegal.

Soma pia: Bola Tinubu apendekeza miezi 9 ya mpito Niger

Tatizo, hata hivyo, ni kwamba baadhi wanaamini ECOWAS inapoteza kwa kasi nia njema na uungwaji mkono kutoka kwa Waafrika wengi wa Magharibi ambao wanaona kuwa inashindwa kuwakilisha maslahi yao katika eneo ambalo wananchi wamelalamika kutonufaika na rasilimali za utajiri katika nchi zao.

"Unapoona wananchi wanarudi nyuma na kuiona ECOWAS kama klabu ya viongozi au viongozi wanaosaidiana kwa gharama ya wananchi, haifanyi kazi vizuri," alisema Oge Onubogu, mkurugenzi wa Mpango wa Afrika katika kituo cha ushauri cha Wilson Center chenye makao yake nchini Marekani.

Ni upi mchakato wa kujitoa kutoka jumuiya hiyo?

Mkataba wa ECOWAS unaeleza kwamba nchi wanachama wake wanaotaka kujiondoa katika jumuiya hiyo wataupa uongozi wake notisi ya maandishi ya mwaka mmoja, ambapo mwisho wake "nchi kama hiyo itakoma kuwa mwanachama wa jumuiya hiyo."

Mkataba unasema kwamba katika mwaka huo, serikali inayopanga kuondoka "hata hivyo itazingatia masharti" na majukumu yake chini ya makubaliano. Hata hivyo, ECOWAS ilisema bado haijajulishwa kuhusu uamuzi wa nchi hizo tatu kujiondoa na kwamba kwa sasa, "wamesalia kuwa wanachama muhimu" wa chombo hicho.

Mataifa ya Mali, Niger na Burkina Faso yaliwahi pia kuzungumzia suala la kuungana na kuwa taifa moja.

Wachambuzi wanasema ECOWAS huenda ikatafuta kuendelea na mazungumzo na viongozi wa kijeshi kuhusu namna bora ya kuhakikisha uthabiti wa eneo hilo huku viongozi wa kijeshi wa mataifa hayo wakizingatia kutafuta ushirikiano mpya.

Je, kujitoa huko kuna umuhimu kiasi gani?

Jambo moja liko wazi. Uhusiano kati ya ECOWAS na nchi hizo tatu umezorota kwa sababu ya chaguo la kanda hiyo la kuweka vikwazo kama chombo muhimu katika kujaribu kubadilisha tawala za mapinduzi huko.

Muungano wa Mataifa ya Sahel ambao watawala hao wa kijeshi waliunda mwezi Novemba pia ulionekana na waangalizi kama jaribio la kuhalalisha serikali zao za kijeshi, kutafuta ushirikiano wa kiusalama na kuwa huru zaidi kutoka kwa ECOWAS.

Soma pia:ECOWAS yaidhinisha uvamizi wa kijeshi dhidi ya Niger 

Lakini kujiondoa kutoka jumuiya hiyo yenye umri wa miaka 49 kwa njia kama hiyo ni jambo ambalo halijawahi kushuhudiwa na inaonekana kama "mabadiliko makubwa katika kanda," alisema Ndiaye wa Taasisi ya Timbuktu ya Mafunzo ya Amani.

"Ni suala gumu zaidi linaloikabili kanda hii tangu kuanzishwa kwake," alisema Ndiaye. "Kazi yote waliyoweka katika kujenga mfumo wa usalama wa pamoja inatokana na itifaki zinazosisitiza kuwa demokrasia, utawala bora na utawala wa sheria ndio msingi wa amani na usalama."

Urusi, utawala wa muda mrefu wa kijeshi na uwezekano wa makosa mengine

ECOWAS imekuwa ikiongoza juhudi za kurudisha utawala wa kiraia kwa nchi zilizoathiriwa na mapinduzi, ikishinikiza tawala za kijeshi kwa vikwazo na kukataa ratiba ndefu za mpito.

Ufafanuzi:Kwanini Niger ni muhimu kwa mataifa ya magharibi?

01:26

This browser does not support the video element.

Wasiwasi umekuwa kwamba kuna ushahidi mdogo kuonyesha kwamba watawala wa kijeshi wamejitolea kufanya uchaguzi wa kidemokrasia ndani ya muda huo. Kwa tangazo la Jumapili, wachambuzi wanasema kuondoa utiifu kwa ECOWAS huenda kukachelewesha kurejeshwa kwa demokrasia katika nchi hizo tatu na kuchochea mapinduzi katika mataifa mengine.

"Kama wao si sehemu tena ya Jumuiya ya ECOWAS, si lazima wafuate ratiba za nyuma za mpito zilizotangazwa kama njia ya kupunguza vikwazo dhidi yao," alisema Ryan Cummings, mkurugenzi wa kampuni ya ushauri ya usalama inayolenga Afrika ya Signal Risk.

Cummings anasema kujiondoa kwao kunaweza kusababisha fursa mpya kwa Urusi kupanua uwepo wake na maslahi yake barani Afrika.

Soma pia: Kwa nini makoloni ya zamani ya Ufaransa Afrika yamekumbwa na mapinduzi

Uhusiano uliokuwa wa kirafiki kati ya nchi hizo tatu na mataifa yaliyoendelea ya Magharibi na Ulaya tayari ulikuwa umeharibika baada ya mapinduzi. Urusi wakati huo huo imekuwa ikizikaribia zaidi na inaendelea kutumia chuki dhidi ya Ufaransa kujiweka sawa na mataifa ya Kiafrika kama nchi ambayo haikuwahi kuwa mkoloni katika bara hilo.

Kundi la mamluki la Urusi Wagner limekuwepo nchini Mali, ambapo linashirikiana na jeshi katika kupambana na waasi wenye silaha. Nchini Burkina Faso, vyombo vya habari vya serikali viliripoti wiki iliyopita kwamba wanajeshi wa Urusi waliwasili "kuimarisha ushirikiano wa kijeshi na wa kimkakati" kati ya nchi hizo mbili. Maafisa wakuu wa Urusi na Niger pia wamekaribishana hivi karibuni.

ECOWAS kuunda kikosi cha dharura kwa ajili ya Niger

02:21

This browser does not support the video element.

"Nchi hizi katika miezi ya hivi karibuni zimeimarisha na kuongeza ushirikiano na Urusi kutoka usalama wa kitaifa hadi uchumi," alisema Cummings wa Signal Risk.

Ni kiasi gani cha msaada ambacho wangeweza kupata kutoka Urusi bado haijawa wazi. Katika nchi za Kiafrika ambako Wagner imekuwepo, mizozo ya usalama huko imeendelea huku kundi hilo la mamluki likishutumiwa kwa ukiukaji wa haki mbalimbali.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW