1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ECOWAS: Jeshi la Afrika Magharibi lipo tayari kuingia Niger.

19 Agosti 2023

Jumuiya ya Kiuchumi ya Mataifa ya Afrika Magharibi, ECOWAS, imeridhia uwezekano wa kuingilia kati kijeshi kurejesha demokrasia nchini Niger, ikiwa juhudi za kidiplomasia zitagonga mwamba.

Ghana Accra | ECOWAS Treffen
Picha: Richard Eshun Nanaresh/AP Photo/picture alliance

Kamishna wa Mambo ya Siasa, Amani na Usalama Abdel-Fatau Musah ameyasema hayo baada ya kuhitimishwa mkutano wa siku mbili wa wakuu wa majeshi wa mataifa hayo ya Afrika Magharibi uliofanyika mjini Accra Ghana.

Katika mkutano huo ambao ulikuwa na lengo la kuharakisha upatikanaji wa vifaa vya kufanikisha uingiliaji wa kijeshi na mikakati yao, hakujwekwa wazi ni lini hasa zoezi hilo linaweza kutekelezwa.

Siku ya jeshi la ECOWAS kuingia Niger imeamuliwa.

Wakuu wa majeshi katika mataifa ya Jumuiya ya Kiuchumi ya Mataifa ya Afrika Magharibi, ECOWAS wakiwa Accra Ghana.Picha: Francis Kokoroko/REUTERS

Abdel-Fatau amesema "Tuko tayari kwenda muda wowote,amri imetolewa,"Na siku husika pia imeamuliwa." Aidha ameongeza kwa kusema tayari wamekubaliana na vitu gani pia vitahitajika katika uvamizi huo, ingawa pia amesisitiza kuwa bado wanatoa fursa ya kushirikiana na utawala wa kijeshi wa Niger katika kufanikisha ufumbuzi wa amani.

Amesema ECOWAS inatarajiwa kutuma ujumbe wa kidiplomasia nchini Niger Jumamosi ya Agosti 19, ingawa ujumbe kama huo uliopita  ulishindwa kukutana na kiongozi huyo wa kijeshi mpya wa nchi hiyo.

Jaribio la kukutana na mamlaka ya kijeshi.

 Abdel-Fatau amesema (19.08.2022) kuna uwezekano wa ujumbe wa ECOWAS kwenda nchini Niger kuendelea kufuata njia ya amani ya kurejesha utulivu wa kikatiba. Wako tayari kutatua suala hilo kwa amani lakini kunahitajika ushiriki wa pande mbili.

Maafisa wa kijeshi walimwondoa madarakani Rais wa Niger Mohamed Bazoum Julai 26 na wamekaidi wito wa Umoja wa Mataifa, ECOWAS na wengine kumrejesha katika kiti chake, jambo lililosababisha jumuiya hiyo kukusanya nguvu za kijeshi kwa lengo la kumrudisha.

Ukimya wa jeshi lenye kushika hatamu ya uongozi.

Mtawala mpya wa kijeshi nchini Niger, Abdourahamane Tiani wakati akizungumza moja kwa moja kupitia televisheni.Picha: Télé Sahel/AFP

Hadu wakati huu hakujawa na jibu lolote la haraka kutoka kwa serikali ya Niger, ambayo hapo awali ilionya dhidi ya uingiliaji wowote wa kijeshi na hata kutishia kumfungulia Rais Bazoum mashtaka ya uhaini. Lakini pia walisikika wakisema wako tayari kwa mazungumzo.

Mataifa mengi katika jumuiya hiyo yenye wanachama 15 yameionesha utayari wa kuchangia kwa jeshi la pamoja isipokuwa wale yalio chini ya utawala wa kijeshi kama Mali, Burkina Faso na Guinea na Cape Verde. Hata hivyo wakuu wa majeshi hawajsema askari wangapi watapelekwa katika uwanja wa vita au maelezo mengine ya kimkakati.

Soma zaidi:Wakuu wa majeshi ya ECOWAS kuhitimisha mipango kuhusu Niger

Kimsingi uingilaji wowote wa kijeshi nchini Niger utavuruga zaidi eneo la maskini la Sahel, ambalo tayari linapambana na uasi wa makundi yenye itikadi kali kwa takribani mwezi mmoja sasa.

Vyanzo:RTR/AFP/DW

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW